Monday, August 13, 2012

MASKINI KAJALA....! WAKILI WAKE APATA UDHURU, HAKIMU ALAZIMIKA KUAHIRISHA KESI NA KUMRUDISHA TENA RUMANDE HADI JUMATANO IJAYO

Kajala... hapa ni kabla hajakumbana na matatizo yanayomkabili sasa.
Kesi inayomkabili msanii wa filamu Kajala Masanja na mumewe Faraja Chambo kuhusiana na mashtaka ya kula njama, kuhamisha umiliki wa nyumba na utakatishaji wa fedha itaanza kusikilizwa Jumatano ijayo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imefahamika leo. 

Awali, ushahidi wa upande wa Jamhuri ulitakiwa kuanza kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo. Hata hivyo, wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa alikuwa na udhuru wa kikazi na ndipo ilipopangiwa Jumatano ya Agosti 22.

Leonard Swai ambaye ni Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), alisema kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa na shahidi mmoja aliyekuwa awasilishe ushahidi wake.

Baada ya kuiahirisha kesi hiyo hadi Jumatano ya wiki ijayo, Hakimu Fimbo akasema kuwa washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Kajala na mumewe Chambo wanakabiliwa na shtaka la kula njama ya kuhamisha umiliki wa nyumba iliyoko Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007. huku wakijua wazi kwamba kufanya hivyo ni kosa kwani tayari Mwanasheria Mkuu wa serikali alishazuia kuuzwa kwa nyumba hiyo.

Imedaiwa katika shitaka la pili kuwa Aprili 14,2010, Kajala na Chambo walihamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kwenda kwa Emiliana Rwegarura huku wakijua imepatikana kwa rushwa, kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Shitaka la tatu linadai kuwa siku na mahali hapo (Kunduchi), washitakiwa Kajala na Chambo walitakatisha fedha huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.


Kwa nyakati tofauti, washtakiwa hao walikana mashtaka yote na kuendelea kusota mahabusu kwavile mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

WACHEKI AKINA MESSI, NEYMAR WAKIJIFUA LEO NA TIMU ZAO ZA TAIFA KWA AJILI YA MECHI ZAO ZA KIRAFIKI ZA JUMATANO

Mshambuliaji wa Argentina, Lionel Messi akipiga mpira wakati wa mazoezi ya timu yake ya taifa mjini Frankfurt leo Agosti 13, 2012. Argentina watacheza dhidi ya Ujerumani katika mechi ya soka ya kirafiki mjini Frankfurt Jumatano. Picha: REUTERS
Mshambuliaji wa Argentina, Lionel Messi akipiga mpira wakati wa mazoezi ya timu yake ya taifa mjini Frankfurt leo Agosti 13, 2012. Argentina watacheza dhidi ya Ujerumani katika mechi ya soka ya kirafiki mjini Frankfurt Jumatano. Picha: REUTERS
Mshambuliaji wa Argentina, Lionel Messi akipiga mpira wakati wa mazoezi ya timu yake ya taifa mjini Frankfurt leo Agosti 13, 2012. Argentina watacheza dhidi ya Ujerumani katika mechi ya soka ya kirafiki mjini Frankfurt Jumatano. Picha: REUTERS
Wachezaji wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar (kushoto) na Thiago Silva wakipasha wakati wa mazoezi yao leo ya kujiandaa na mechi yao ya kirafiki dhidi ya Sweden kwenye Uwanja wa Soderstadion mjini Stockholm leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS
Beki wa timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves akishiriki mazoezi yao leo ya kujiandaa na mechi yao ya kirafiki dhidi ya Sweden kwenye Uwanja wa Soderstadion mjini Stockholm leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS
Beki wa timu ya taifa ya Brazil, Thiago Silva akishiriki mazoezi yao leo ya kujiandaa na mechi yao ya kirafiki dhidi ya Sweden kwenye Uwanja wa Soderstadion mjini Stockholm leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS
Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Brazil, ambao walitwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya London 2012, wakisalimia mashabiki katika gari la zimamoto mjini Sao Paulo leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS
Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Brazil, ambao walitwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya London 2012, wakisalimia mashabiki katika gari la zimamoto mjini Sao Paulo leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS
Mabingwa na washindi wa medali za dhahabu wa timu ya Michezo ya Olimpiki ya Ufaransa wakipungia mashabiki kutokea katika basi la wazi mjini Paris wakati wakirejea nyumbani kutoka kushiriki Michezo ya Olimpiki ya London 2012 leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS
Mabingwa na washindi wa medali za dhahabu wa timu ya Michezo ya Olimpiki ya Ufaransa wakipungia mashabiki kutokea katika basi la wazi mjini Paris wakati wakirejea nyumbani kutoka kushiriki Michezo ya Olimpiki ya London 2012 leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS
Mabingwa na washindi wa medali za dhahabu wa timu ya Michezo ya Olimpiki ya Ufaransa wakipungia mashabiki kutokea katika basi la wazi mjini Paris wakati wakirejea nyumbani kutoka kushiriki Michezo ya Olimpiki ya London 2012 leo Agosti 13, 2012. Picha: REUTERS

FABREGAS AMCHANA PEP GUARDIOLA, ADAI MFUMO WAKE ULIMSHINDA ND'O MANA AKAONEKANA NYANYA

Cesc Fabregas
Fabregas akisindikizwa na kocha Guardiola kuingia uwanjani akitokea benchi katika mechi yao ya kuwania taji la 'Super Cup' dhidi ya Real Madrid iliyochezwa Agosti 17, 2011. 
Kocha Guardiola akiwapongeza wachezaji wake Fabregas na Javier Mascherano baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 4-3 katika mechi yao ya marudiano ya kuwania taji la 'Super Cup' dhidi ya Real Madrid Agosti 17, 2011. 
MADRID, Hispania
CESC Fabregas amekiri kwamba alipata wakati mgumu sana kuzoea uchezaji wa Barcelona msimu uliopita kwa sababu ya mfumo wa uchezaji uliokuwa ukitumiwa na kocha Pep Guardiola.

"Chini ya Guardiola sikuwahi hata mara moja kuuzoea mfumo wa uchezaji," kiungo huyo mwenye miaka 25 alikaririwa akisema kwenye gazeti la Marca leo.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania alihama Arsenal na kutua Barca katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2011, lakini alikuwa na wakati mgumu kuonyesha kiwango alichotarajiwa ambapo sasa amesema kwamba kutocheza kwa uhuru kutokana na mfumo wa Guardiola ndiko kulikomponza na kumfanya aonekane 'amechemsha'.

"Nilikuwa nikicheza mtindo mwingine wa soka na hivyo kuzoea mfumo mwingine kwa haraka ilikuwa kazi ngumu sana kwangu, hasa kwa vile wenzangu wote walikuwa wameshauelewa," Fabregas alieleza.

Aliongeza, "Kucheza katika nafasi ya kiungo ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu nahitaji kuzunguka zaidi na mimi sio mwepesi sana kiasi cha kucheza katika eneo la mita chache kunizunguka.

"Sihitaji chochote, lakini hiyo ndiyo aina yangu ya kucheza. Ni kweli kwamba kwa kiasi fulani sina mpangilio maalum, lakini huo nd'o uchezaji wangu. Baadhi ya watu walisema kwamba kuna kitu nilikikosa msimu uliopita, akiwemo Guardiola."

Fabregas amekiri kwamba alianza msimu uliopita kwa kujaribu kucheza kama viungo wengine aliowakuta Barcelona.

"Kwakweli hilo lilikuwa kosa langu kwa sababu nilijaribu kuonekana kwa namna isiyoendana na mimi; mimi sio Xavi, (Andres) Iniesta, au Thiago (Alcantara). Mimi ni mimi na ninahitaji kuzunguka huku na kule uwanjani, kucheza zaidi ya eneo moja."

Fabregas alifunga mabao tisa katika mechi 28 za La Liga alizocheza msimu uliopita. Hivi sasa, Barca inaongozwa na kocha Tito Vilanova aliyerithi mikoba ya Pep Guardiola aliyeamua kutosaini mkataba mwingine baada ya kumalizika kwa msimu uliopita.

YANGA KUMTAMBULISHA TWITE DAR JUMAMOSI

Beki mpya wa Yanga, Mbuyi Twite (kulia) akipewa jezi ya klabu hiyo na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah bin Kleb baada ya kusaini kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Mbuyi Twite (kushoto) akisaini kuichezea Yanga huku akishuhudiwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah bin Kleb. Bin Kleb ndiye pia aliyemsajili Haruna Niyonzima.

Shindilia na dole kabisa.... Mbuyi akitia saini dole gumba katika mkataba wa kuichezea Yanga.
Hapa Bin Kleb (kushoto) siku alipomtambulisha Haruna Niyonzima baada ya kumsajili kuichezea Yanga
Weka na dole kabisa.... Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati Bin Kleb alivyomsainisha Niyonzima kama alivyofanya sasa kwa Mbuyi Twite

Kelvin Yondani alinaswa kwa kuwekewa 'muzigo munene' mezani na sio longolongo... si unaona mwenyewe hiyo mijihela... mchezaji gani akatae kusaini? Chezea Yanga wewe...! 
YANGA inajiandaa kumpokea beki wake mpya Mbuyi Twite aliyejiunga na klabu hiyo akitokea APR ya Rwanda Jumamosi hii, Afisa Habari wa Yanga, Loius Sendeu ameiambia STRAIKA leo.

Twite aliyejiunga na Yanga baada ya "kuchana" fomu alizosaini mapema za kuichezea Simba kutokana na kupewa donge nono zaidi na klabu hiyo ya Jangwani, kwa sasa ameenda kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kuaga ndugu zake kabla ya kuja rasmi kujiunga na klabu yake mpya, alisema Sendeu.

“Mbuyi Twite atatua nchini Jumamosi au Jumapili akitokea Kongo. Tulitaka aje mapema ili ajiunge na wenzake katika mazoezi lakini yuko katika mapumziko ya wiki moja,” aliongeza Sendeu.

Beki huyo wa kati ambaye atalazimika kupigania namba dhidi ya Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kelvin Yondani wa kikosi cha kwanza pamoja na Ladislaus Mbogo, amezua gumzo kubwa kutokana na namna alivyowakacha Simba na kutua Yanga.

Baada ya kuonyesha kiwango katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) akiichezea APR ya Rwanda, Simba ilimsajili kwa dau linalotajwa la dola 30,000 (sawa na Sh. milioni 46) lakini Yanga wamedaiwa kuingilia sherehe kwa kumpa dola 45,000 (sawa na Sh. milioni 70), jambo lililomfanya Twite kurudisha fedha za Wekundu wa Msimbazi na kusaini kuicheza Yanga.

Hata hivyo, Yanga ilijibu tuhuma kwamba iliwavamia Simba katika kumsajili mchezaji huyo wakati uongozi wake ulipodai kwamba Wanajangwani ndio waliokuwa wa kwanza kumfuatilia mchezaji huyo huku wakiwasema Simba kwamba "walipeleka posa kwa mchumba wa watu, matokeo yake wamekuta harusi." 

TUMEKOSA MEDALI OLIMPIKI LAKINI KWA SARAKASI TUMETESA

Watanzania wa kikundi cha sarakasi cha Black Eagles wakibeba mwenge wa Olimpiki wakati wa shamrashamra za Michezo ya Olimpiki ya London 2012.
Wacheza sarakasi wa kikundi cha Black Eagles wakifanya mambo nchini Uingereza

Wacheza sarakasi wa kikundi cha Black Eagles wakifanya mambo nchini Uingereza

Wacheza sarakasi wa kikundi cha Black Eagles wakipozi kwa picha
WAKATI timu ya Olimpiki ya Tanzania imeshindwa vibaya katika Michezo ya London 2012, faraja pekee inaweza kuwa ni kundi la sanaa Black Eagles Acrobatics linaloundwa na Watanzania waishio Chatham Kent, Uingereza, ambalo liliakwa kutumbuiza kwenye shamrashamra za michezo hiyo ya London.

Mkurugenzi wa kundi hilo Ally Kasele alisema kuwa ni fahari Black Eagles kualikwa na kufanya sarakasi mbele ya maelfu ya watu waliomiminika nchini Uingereza kuhudhuria Michezo ya Olimpiki.


"Walialikwa wasanii zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali na sisi kutoka Tanzania tulikuwa miongoni mwao… hii ilikuwa ni fahari kwetu kuitangaza nchi yetu," alisema Kasele.


Alisema kuwa walipangiwa kufanya vitu vyao kila kona ya eneo la Olimpiki Park na kushangiliwa sana na maelfu ya watu kwa maajabu waliyokuwa wakiyafanya huku waandaji nao wakibaki wameduwaa kwa vitu vyao.
"Waandaji hao walisikika wakisema kuwa Black Eagles tumekuwa wa kwanza kwa kuwapagawisha mashabiki hadi wakaturuhusu kwenda kushika Mwenge wa Olimpiki," alisema.


Aidha, alisema mwaka huu kundi hilo limefanya maonyesho mbalimbali yakiwamo ya kukimbiza Mwenge wa Olimpiki kwenye maeneo ya Kennington, London, Derby, Newbur Berkshire, City Centre Cardiff, Dulston London na Hackney na kujizolea umaarufu.


"Mbali na maonyesho hayo, tulishashiriki pia Jubilee ya Malkia ya Uingereza ambayo inajulikana kama Queen's Jubilee hali ambayo ilichangia kutuongezea umaarufu na kutufanya tujulikane zaidi hapa Uingereza," alisema.
Kasele alisema kuwa kundi hilo lina wasanii 16 na kuwataja baadhi yao kuwa ni yeye (Kasele) mkurugenzi, Simon Thobias, Mohamed Idd, Hilary Majaliwa na Shaban.


Alifafanua kuwa The Black Eagles Acrobatics lilianzishwa mwaka 1996 na limekuwa pia likipokea wasanii mbalimbali kutoka Tanzania ambao hufika Uingereza kushiriki maonyesho mbalimbali yakiwemo ya Sikukuu ya Krismasi.

ALEX SONG AFUNGUKA KUHUSU BARCELONA KWA KUSEMA: NIMEFURAHI KUTAKIWA NA KLABU BORA ZAIDI DUNIANI, LAKINI MIMI NI WA ARSENAL...!

Alex Song
'Jembe' Alex Song wa Arsenal akichuana na Carlos Tevez wa Man City (kulia) wakati wa mechi yao ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Birds Nest jijini Beijing, China Julai 27, 2012.
LONDON, England
Alex Song amekiri kwamba ni kweli Barcelona wamepania sana kumsajili, lakini amepinga vikali uvumi uliozagaa kwamba naye anataka sana kuondoka katika klabu yake ya sasa ili ajiunge na vigogo hao wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

Tetesi kuhusu kuondoka kwa Song zimezidi kuongezeka baada ya taarifa za vyombo vya habari kudai kwamba Barca wametuma ofa ya awali ya paundi za England milioni 11.7 (Sh. bilioni 28) ili kumnasa mchezaji huyo mwenye miaka 24.

Klabu ya Zenit St Petersburg ya Urusi pia inadaiwa kuwa ni miongoni mwa timu nyingi zinazomfukuzia kiungo huyo wa kimataifa wa Cameroon  .

Beki Gerard Pique na kiungo Andres Iniesta wa Barcelona wamekaririwa hivi karibuni wakisema kuwa wamefurahi kusikia Song yuko mbioni kujiunga nao, kauli zinazofanana na zile walizokuwa wakizitoa nyota hao kabla ya kukamilishwa kwa uhamisho wa Cesc Fabregas kutoka Arsenal kwenda Barca.

Kiungo huyo, aliyetokea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha kocha Arsene Wenger, amekiri kwamba anatakiwa na "timu bora zaidi duniani" lakini hapo hapo akakanusha vikali taarifa zinazodai kuwa sasa yuko tayari kuondoka Arsenal.

"Siwezi kudanganya kwa kusema hawanitaki, lakini mimi niko Arsenal na nina furaha tele kuwa hapa Arsenal," Song aliiambia Sky Sports.

"Barcelona ndio timu bora zaidi duniani, na uvumi utaendelea kuwepo hadi dirisha la usajili litakapofungwa."

Song, aliyehamia Arsenal akitokea SC Bastia kwa ada ya uhamisho ya paundi za England milioni moja (Sh. bilioni 2.4) mwaka 2006, amebakiza miaka miwili kabla ya kumaliza mkataba wake wa sasa, ingawa ripoti zinadai kwamba yuko tayari kusaini mkataba mwingine wa kuendelea kuichezea klabu hiyo ya jiji la London.

ARSENAL WATAKA BILIONI 50/- WAMUACHIE WALCOTT KWA MAN CITY, CHELSEA, LIVERPOOL AU INTER MILAN

Theo Walcott ... akichomoka na mpira kwa kasi kama ya Usain Bolt kuelekea lango la wapinzani. Pamoja na makali yake yote, bado Arsenal ya kocha Arsene Wenger iko tayari kumuuza kwa timu yoyote itakayokuwa tayari kuweka mezani 'bulungutu' la Sh. bilioni 50!
Hapa Theo Walcott akimlamba chenga beki wa timu ya Kitchee FC ya Hong Kong kabla ya kufyatuka kwa mibio yake ya kasi ya umeme wakati wa mechi yao ya kirafiki kujiandaa na msimu mpya iliyochezwa jijini Hong Kong Julai 29, 2012 .  

LONDON, England
Arsenal wanataka walipwe mabilioni ya pesa ili kumuachia straika wao Theo Walcott aende kuichezea klabu yoyote kati ya zile zilizoonyesha dhamira ya kumuhitaji.

Taarifa kutoka ndani ya Arsenal zimefichua jioni hii kwamba Arsenal wako tayari kumuachia winga huyo mwenye kasi anayeichezea pia timu ya taifa ya England kwa dau lisilopungua paundi za England milioni 20, ambazo ni sawa na takriban Sh. bilioni 50.

Walcott yuko katika mwaka wa mwisho wa kumalizia mkataba wake wa sasa na tayari klabu kadhaa kubwa za Ulaya zimekuwa zikimfukuzia kwa udi na uvumbi ili kumng'oa kutoka mikononi mwa kocha Arsene Wenger, baadhi ya klabu hizo zikiwa ni za Chelsea, Liverpool, Manchester City na Inter Milan ya Italia.

Vyanzo vimedai kuwa tayari Inter wameshaiendea Arsenal na kuuliza bei ya nyota huyo ambapo jibu walilopewa ni hilo la kutakiwa 'kukata mkwanja' wa Sh. bilioni 50.

XABI ALONSO AGOMEA MAZUNGUMZO MKATABA MPYA REAL MADRID



Xabi Alonso
MADRID, Hispania
KUNA taarifa zilizopatikana leo zinazodai kuwa kiungo Xabi Alonso ametishia kutofanya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea klabu yake ya Real Madrid.

Gazeti la Sport limesema kwamba  sasa Xabi anafikiria kuhitimisha kipindi chake cha kuichezea Real baada ya kumalizika kwa msimu ujao.

Mkataba wa sasa wa kiungo huyo mchezeshaji aliyewahi kuichezea pia Liverpool unamfunga Real  hadi mwaka 2014 na licha ya kufurahia maisha kwa vigogo hao wa Hispania, lakini anaamini kwamba sasa kipindi chake cha kung'ara kwenye klabu hiyo kinaelekea ukingoni.

Juventus na Inter Milan zimedaiwa kuanza kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mazungumzo ya nyota huyo wa timu ya taifa ya Hispania na klabu yake ili ikibidi zianze harakati za kumtwaa.

HATIMAYE TOTTENHAM WAKUBALI LUKA MODRIC AENDE REAL MADRID KWA BIL. 60/-


Luka Modric
MADRID, Hispania
REAL Madrid wamesema kuwa tayari wameshafikia makubaliano na Tottenham kuhusiana na usajili wa kiungo wa kimataifa wa Croatia, Luka Modric ili aichezee kuanzia msimu ujao wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

Gazeti la AS limeripoti leo kuwa mwafaka umefikiwa baina ya klabu hizo mbili na kitu pekee kinachosubiriwa sasa ni ombi la Tottenham la kutaka wapewe muda wa kusaka kiungo mwingine mbadala kabla ya kumruhusu Modric.

Kwa mujibu wa makubaliano yao, ada ya uhamisho ya Modric itakuwa euro milioni 32 (Sh. bilioni 60) pamoja na 'bonasi' zitakazotokana na idadi ya mechi atakazocheza akiwa Real Madrid na mafanikio atakayopata.

Awali, mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy alitaka bei ya mwisho ya kumuuzia Modric kuwa euro milioni 38 (Sh. bilioni 72), lakini sasa amelainika na kukubali kupunguza kiwango hicho.

Ikiwa makubaliano hayo yatatekelezwa yataipa nafuu kubwa Real, ambayo ilishuhudia 'ofa' ya PSG ya Ufaransa kutaka kumtwaa Modric kwa euro milioni 45 (Sh. bilioni 86) ikikataliwa na mchezaji huyo aliyesisitiza kwamba hataki kwenda kokote isipokuwa kwa mabingwa hao wa La Liga, Real Madrid

JOE HART, STURRIDGE WATEMWA TAIFA ENGLAND


Daniel Sturridge

Joe Hart
LONDON, England
KIPA Joe Hart na straika Daniel Sturridge hawatakuwamo katika kikosi cha timu ya taifa ya England kitakachocheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Italia keshokutwa kutokana na majeraha.

Hart, kipa wa Manchester City ambaye ni chaguo la kwanza katika timu ya taifa, hakuwamo pia katika kikosi cha klabu yake kilichoshinda 3-2 dhidi ya Chelsea jana na kutwaa Ngao ya Jamii kutokana na maumivu ya mgongo.

Hata hivyo, kocha wake Roberto Mancini alisema kuwa tatizo alilo nalo "sio kubwa sana."

Straika wa Chelsea, Sturridge aliumia kidole gumba cha mguu wakati alipoingia akitokea benchi kwenye uwanja wa Villa Park.

Kocha wa timu ya taifa ya England, Roy Hodgson hajaita mchezaji mwingine yeyote kuziba nafasi za wawili hao, na hivyo John Ruddy wa Norwich City atakuwa akipigania nafasi ya kuitwa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa mjini Berne, pamoja na kipa Na.1 wa timu ya England iliyoshiriki michezo ya Olimpiki, Jack Butland.

Andy Carroll, Jermain Defoe na Theo Walcott ndio washambuliaji waliobaki kikosini. Mechi hiyo itakayochezwa kwenye uwanja huru ni marudio ya robo fainali ya michuano ya Euro 2012 iliyoandaliwa na nchi za Poland na Ukraine, ambapo kikosi cha kocha Cesare Prandelli kiliifunga England kwa penati kabla na kutinga fainali.

USAIN BOLT: CRISTIANO RONALDO NI MKALI KULIKO LIONEL MESSI

Ronaldo (kushoto) na Messi wakiwa hoi baada ya mechi mojawapo ya el clasicco kati ya timu zao za Real Madrdi na Barcelona.

Ronaldo akifurahia baada ya kuifungia bao Real Madrid

Messi akishangilia baada ya kuifungia Barca bao.
Usain Bolt
LONDON, England
MWANARIADHA nyota wa Jamaica, Usain Bolt amesema leo kuwa straika wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ana kiwango cha juu zaidi cha soka na kwamba amemuacha mbali sana straika wa Barcelona, Lionel Messi.

Bolt na Ronaldo wana urafiki binafsi, ambao ulianza wakati Bolt alipokuwa akimpa Ronaldo mafunzo ya kukimbia wakati alipokuwa akiichezea Manchester United.

"Hakuna swali, Cristiano ni mkali kuliko Messi. Yeye ni mchezaji aliyekamilika zaidi," anasema Bolt. 


"Cristiano ni mcheshi na pia ni mtu safi sana," anaongeza Bolt.

MAREKANI WATETEA MEDALI YA DHAHABU KIKAPU OLIMPIKI

LeBron James wa timu ya kikapu ya Marekani akiwapa shughuli wachezaji timu ya Hispania wakati wa fainali yao ya Olimpiki jana.

LONDON, Marekani
MAREKANI walitwaa medali yao ya 14 ya kikapu ya Olimpiki baada ya kuifunga Hispania 107-100 na kutetea taji lao.

Timu hiyo iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo waliongoza kwa pointi nyingi katika robo ya kwanza lakini Hispania walizinduka na kupunguza pengo la pointi hadi kufikia moja wakati wa mapumziko.

Hata hivyo, Hispania hawakuweza kuidhibiti safu inayotisha ya mashambulizi ya marekani na LeBron James na Kevin Durant walifunga pointi muhimu katika dakika za lala salama.

Durant aliongoza safu ya mashambulizi ya Marekani akifunga pointi 30, wakati Pau Gasol aliongoza Hispania kwa kufunga pointi 24 kwenye Uwanja wa North Greenwich Arena mjini London.

Hispania waliipa presha safu ya ulinzi ya Marekani kwa muda mwingi wa mchezo lakini kutokana na utajiri wa uzoefu wa wachezaji wa ligi ya NBA Wamarekani walikuwa na kikosi kipana zaidi.

Marekani walifunga pointi zaidi ya pointi 100 katika mechi tano kati ya saba walizocheza na kuwapeleka kwenye fainali, zikiwepo pointi 158 dhidi ya Nigeria zilizoweka rekodi ya michuano hiyo, na wakaendelea kiwango chao kisichopingika wakati wakati walipoongiza kwa pointi 35-27 kufikia mwisho wa robo ya kwanza.

Hata hivyo, Hispania walidhamiria kujitoa kwa kila kitu na wakapambana kupunguza tofauti ya pointi, huku mechi ikiwa ya kibabe zaidi na kumaliza nusu ya mchezo wakiwa wamefungwa 59-58.

Huku mashabiki 13,000 wakishuhudia, akiwamo muigizaji wa Marekani Arnold Schwarzenegger na Meya wa London Boris Johnson, Marekani wakaanza kuwa watulivu na pointi tatu walizozihitaji mno kutoka kwa Durant zikawaweka mbele kwa 93-86 huku muda uliobaki ukiwa ni dakika 06:25.

Pointi tatu nyingine muhimu kutoka kwa James, ambaye alifikisha pointi 19 katika mechi hiyo, ilifanya tofauti ya pointi tisa huku zikiwa zimebaki chini ya dakika mbili mechi kumalizika na licha Marc Gasol kufunga katika sekunde za mwisho, Wamarekani walishinda kwa kujiamini.

Kobe Bryant alisema: "Ilikuwa ni safari nzuri kwetu. Ilikuwa ngumu lakini. Hivyo ili kusimama hapa katika wakati kama huu baada ya kucheza na wapinzani wakali kama Hispania, tukiwa na medali ya dhahabu, ni mafanikio makubwa.

"Tuna vipaji vingi vinaibukia. Tunatumai tutaendelea kujenga programu yetu, kuendelea kuwahamasisha vijana wanaoinukia, walioko vyuoni na wengine wote wanaochipukia ili kudumisha utamaduni."