Monday, August 13, 2012

ALEX SONG AFUNGUKA KUHUSU BARCELONA KWA KUSEMA: NIMEFURAHI KUTAKIWA NA KLABU BORA ZAIDI DUNIANI, LAKINI MIMI NI WA ARSENAL...!

Alex Song
'Jembe' Alex Song wa Arsenal akichuana na Carlos Tevez wa Man City (kulia) wakati wa mechi yao ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Birds Nest jijini Beijing, China Julai 27, 2012.
LONDON, England
Alex Song amekiri kwamba ni kweli Barcelona wamepania sana kumsajili, lakini amepinga vikali uvumi uliozagaa kwamba naye anataka sana kuondoka katika klabu yake ya sasa ili ajiunge na vigogo hao wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

Tetesi kuhusu kuondoka kwa Song zimezidi kuongezeka baada ya taarifa za vyombo vya habari kudai kwamba Barca wametuma ofa ya awali ya paundi za England milioni 11.7 (Sh. bilioni 28) ili kumnasa mchezaji huyo mwenye miaka 24.

Klabu ya Zenit St Petersburg ya Urusi pia inadaiwa kuwa ni miongoni mwa timu nyingi zinazomfukuzia kiungo huyo wa kimataifa wa Cameroon  .

Beki Gerard Pique na kiungo Andres Iniesta wa Barcelona wamekaririwa hivi karibuni wakisema kuwa wamefurahi kusikia Song yuko mbioni kujiunga nao, kauli zinazofanana na zile walizokuwa wakizitoa nyota hao kabla ya kukamilishwa kwa uhamisho wa Cesc Fabregas kutoka Arsenal kwenda Barca.

Kiungo huyo, aliyetokea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha kocha Arsene Wenger, amekiri kwamba anatakiwa na "timu bora zaidi duniani" lakini hapo hapo akakanusha vikali taarifa zinazodai kuwa sasa yuko tayari kuondoka Arsenal.

"Siwezi kudanganya kwa kusema hawanitaki, lakini mimi niko Arsenal na nina furaha tele kuwa hapa Arsenal," Song aliiambia Sky Sports.

"Barcelona ndio timu bora zaidi duniani, na uvumi utaendelea kuwepo hadi dirisha la usajili litakapofungwa."

Song, aliyehamia Arsenal akitokea SC Bastia kwa ada ya uhamisho ya paundi za England milioni moja (Sh. bilioni 2.4) mwaka 2006, amebakiza miaka miwili kabla ya kumaliza mkataba wake wa sasa, ingawa ripoti zinadai kwamba yuko tayari kusaini mkataba mwingine wa kuendelea kuichezea klabu hiyo ya jiji la London.

No comments:

Post a Comment