Monday, August 13, 2012

MAREKANI WATETEA MEDALI YA DHAHABU KIKAPU OLIMPIKI

LeBron James wa timu ya kikapu ya Marekani akiwapa shughuli wachezaji timu ya Hispania wakati wa fainali yao ya Olimpiki jana.

LONDON, Marekani
MAREKANI walitwaa medali yao ya 14 ya kikapu ya Olimpiki baada ya kuifunga Hispania 107-100 na kutetea taji lao.

Timu hiyo iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo waliongoza kwa pointi nyingi katika robo ya kwanza lakini Hispania walizinduka na kupunguza pengo la pointi hadi kufikia moja wakati wa mapumziko.

Hata hivyo, Hispania hawakuweza kuidhibiti safu inayotisha ya mashambulizi ya marekani na LeBron James na Kevin Durant walifunga pointi muhimu katika dakika za lala salama.

Durant aliongoza safu ya mashambulizi ya Marekani akifunga pointi 30, wakati Pau Gasol aliongoza Hispania kwa kufunga pointi 24 kwenye Uwanja wa North Greenwich Arena mjini London.

Hispania waliipa presha safu ya ulinzi ya Marekani kwa muda mwingi wa mchezo lakini kutokana na utajiri wa uzoefu wa wachezaji wa ligi ya NBA Wamarekani walikuwa na kikosi kipana zaidi.

Marekani walifunga pointi zaidi ya pointi 100 katika mechi tano kati ya saba walizocheza na kuwapeleka kwenye fainali, zikiwepo pointi 158 dhidi ya Nigeria zilizoweka rekodi ya michuano hiyo, na wakaendelea kiwango chao kisichopingika wakati wakati walipoongiza kwa pointi 35-27 kufikia mwisho wa robo ya kwanza.

Hata hivyo, Hispania walidhamiria kujitoa kwa kila kitu na wakapambana kupunguza tofauti ya pointi, huku mechi ikiwa ya kibabe zaidi na kumaliza nusu ya mchezo wakiwa wamefungwa 59-58.

Huku mashabiki 13,000 wakishuhudia, akiwamo muigizaji wa Marekani Arnold Schwarzenegger na Meya wa London Boris Johnson, Marekani wakaanza kuwa watulivu na pointi tatu walizozihitaji mno kutoka kwa Durant zikawaweka mbele kwa 93-86 huku muda uliobaki ukiwa ni dakika 06:25.

Pointi tatu nyingine muhimu kutoka kwa James, ambaye alifikisha pointi 19 katika mechi hiyo, ilifanya tofauti ya pointi tisa huku zikiwa zimebaki chini ya dakika mbili mechi kumalizika na licha Marc Gasol kufunga katika sekunde za mwisho, Wamarekani walishinda kwa kujiamini.

Kobe Bryant alisema: "Ilikuwa ni safari nzuri kwetu. Ilikuwa ngumu lakini. Hivyo ili kusimama hapa katika wakati kama huu baada ya kucheza na wapinzani wakali kama Hispania, tukiwa na medali ya dhahabu, ni mafanikio makubwa.

"Tuna vipaji vingi vinaibukia. Tunatumai tutaendelea kujenga programu yetu, kuendelea kuwahamasisha vijana wanaoinukia, walioko vyuoni na wengine wote wanaochipukia ili kudumisha utamaduni."


No comments:

Post a Comment