Monday, August 13, 2012

MASKINI KAJALA....! WAKILI WAKE APATA UDHURU, HAKIMU ALAZIMIKA KUAHIRISHA KESI NA KUMRUDISHA TENA RUMANDE HADI JUMATANO IJAYO

Kajala... hapa ni kabla hajakumbana na matatizo yanayomkabili sasa.
Kesi inayomkabili msanii wa filamu Kajala Masanja na mumewe Faraja Chambo kuhusiana na mashtaka ya kula njama, kuhamisha umiliki wa nyumba na utakatishaji wa fedha itaanza kusikilizwa Jumatano ijayo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imefahamika leo. 

Awali, ushahidi wa upande wa Jamhuri ulitakiwa kuanza kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo. Hata hivyo, wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa alikuwa na udhuru wa kikazi na ndipo ilipopangiwa Jumatano ya Agosti 22.

Leonard Swai ambaye ni Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), alisema kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa na shahidi mmoja aliyekuwa awasilishe ushahidi wake.

Baada ya kuiahirisha kesi hiyo hadi Jumatano ya wiki ijayo, Hakimu Fimbo akasema kuwa washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Kajala na mumewe Chambo wanakabiliwa na shtaka la kula njama ya kuhamisha umiliki wa nyumba iliyoko Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007. huku wakijua wazi kwamba kufanya hivyo ni kosa kwani tayari Mwanasheria Mkuu wa serikali alishazuia kuuzwa kwa nyumba hiyo.

Imedaiwa katika shitaka la pili kuwa Aprili 14,2010, Kajala na Chambo walihamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kwenda kwa Emiliana Rwegarura huku wakijua imepatikana kwa rushwa, kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Shitaka la tatu linadai kuwa siku na mahali hapo (Kunduchi), washitakiwa Kajala na Chambo walitakatisha fedha huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.


Kwa nyakati tofauti, washtakiwa hao walikana mashtaka yote na kuendelea kusota mahabusu kwavile mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

No comments:

Post a Comment