Monday, August 13, 2012

YANGA KUMTAMBULISHA TWITE DAR JUMAMOSI

Beki mpya wa Yanga, Mbuyi Twite (kulia) akipewa jezi ya klabu hiyo na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah bin Kleb baada ya kusaini kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Mbuyi Twite (kushoto) akisaini kuichezea Yanga huku akishuhudiwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah bin Kleb. Bin Kleb ndiye pia aliyemsajili Haruna Niyonzima.

Shindilia na dole kabisa.... Mbuyi akitia saini dole gumba katika mkataba wa kuichezea Yanga.
Hapa Bin Kleb (kushoto) siku alipomtambulisha Haruna Niyonzima baada ya kumsajili kuichezea Yanga
Weka na dole kabisa.... Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati Bin Kleb alivyomsainisha Niyonzima kama alivyofanya sasa kwa Mbuyi Twite

Kelvin Yondani alinaswa kwa kuwekewa 'muzigo munene' mezani na sio longolongo... si unaona mwenyewe hiyo mijihela... mchezaji gani akatae kusaini? Chezea Yanga wewe...! 
YANGA inajiandaa kumpokea beki wake mpya Mbuyi Twite aliyejiunga na klabu hiyo akitokea APR ya Rwanda Jumamosi hii, Afisa Habari wa Yanga, Loius Sendeu ameiambia STRAIKA leo.

Twite aliyejiunga na Yanga baada ya "kuchana" fomu alizosaini mapema za kuichezea Simba kutokana na kupewa donge nono zaidi na klabu hiyo ya Jangwani, kwa sasa ameenda kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kuaga ndugu zake kabla ya kuja rasmi kujiunga na klabu yake mpya, alisema Sendeu.

“Mbuyi Twite atatua nchini Jumamosi au Jumapili akitokea Kongo. Tulitaka aje mapema ili ajiunge na wenzake katika mazoezi lakini yuko katika mapumziko ya wiki moja,” aliongeza Sendeu.

Beki huyo wa kati ambaye atalazimika kupigania namba dhidi ya Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kelvin Yondani wa kikosi cha kwanza pamoja na Ladislaus Mbogo, amezua gumzo kubwa kutokana na namna alivyowakacha Simba na kutua Yanga.

Baada ya kuonyesha kiwango katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) akiichezea APR ya Rwanda, Simba ilimsajili kwa dau linalotajwa la dola 30,000 (sawa na Sh. milioni 46) lakini Yanga wamedaiwa kuingilia sherehe kwa kumpa dola 45,000 (sawa na Sh. milioni 70), jambo lililomfanya Twite kurudisha fedha za Wekundu wa Msimbazi na kusaini kuicheza Yanga.

Hata hivyo, Yanga ilijibu tuhuma kwamba iliwavamia Simba katika kumsajili mchezaji huyo wakati uongozi wake ulipodai kwamba Wanajangwani ndio waliokuwa wa kwanza kumfuatilia mchezaji huyo huku wakiwasema Simba kwamba "walipeleka posa kwa mchumba wa watu, matokeo yake wamekuta harusi." 

No comments:

Post a Comment