Thursday, August 9, 2012

NEYMAR: BRAZIL TUNABAHATI SANA GIOVANI DOS SANTOS HATACHEZA FAINALI OLIMPIKI

Neymar

LONDON, England
TAARIFA za kuwa majeruhi kwa Giovani dos Santos zimeifikia kambi ya Brazil, na uwezekano wa mchezaji huyo wa Tottenham kukosa mechi ya fainali ya Olimpiki ukawa ndio mjadala mkuu.

"Tutakuwa na bahati sana (kama hatacheza)", alisema Neymar kuiambia ESPN leo, saa chache kabla timu ya madaktari wa Mexico kuthibitisha kwamba ni kweli Dos Santos atakosa fainali.
 
Neymar ataingia katika fainali yake ya kwanza akiwa na Brazil katika ngazi yoyote, jambo linalomaanisha kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 atakuwa na jukumu la ziada la kuwa mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kuipa Brazil medali ya kwanza ya dhahabu.

"Itakuwa ni fainali yangu ya kwanza na Brazil na najivunia kuwa hapa kuiwakilisha nchi yangu katika kipindi muhimu kama hiki, fainali yetu ya kwanza ya Olimpiki katika miaka 24," alisema mshambuliaji huyo wa klabu ya Santos.

Kukiwa na kuongezeka kwa presha kutoka katika vyombo vya habari vya Brazil, medali ya fedha inachukuliwa kama haina maana yoyote na wachezaji na makocha kwa kipindi chote cha michuano hiyo, huku Neymar akikiri jambo hilo lakini pia akisema timu yao imepata mafanikio kufikia sasa.

"Ni lazima tuendelee kufanya tunayofanya katika michuano hii. Inazaa matunda," alisema.

Pamoja na Lucas Moura na Leandro Damiao, Neymar amekuwa mmoja wa nyota ambao Brazil inawategemea si tu kuleta dhahabu, bali pia kuirejesha timu ya wakubwa ya Brazil kileleni wakati watakapoandaa fainali za Kombe la Dunia 2014.

Huku Kombe la Dunia likiwa miaka miwili mbele, macho ya Neymar yako kwenye medali ya dhahabu.

"Hakuna Mbrazili aliyewahi kushinda taji hili katika soka na najiandaa kuisaidia timu yangu kuondoka na dhahabu," alimalizia.

RONALDO AJIPA MOYO TUZO MWANASOKA BORA WA DUNIA

Cristiano Ronaldo
NEW YORK, Marekani
Cristiano Ronaldo amekuwa akishinda tuzo nyingi akiwa na Real Madrid hadi kufikia mwaka huu 2012, lakini amekiri kwamba kuna tuzo moja tu ambayo anataka kuiona kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Nayo ni tuzo nyingine ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia (FIFA Ballon d'Or).
"Itakuwa safi sana (kuwa mshindi wa tuzo hiyo)," Ronaldo amesema leo.


Straika huyo amekiri kwamba mwanzoni mwa msimu uliopita alipania kutwaa tuzo nyingi kadri itakavyowezekana kwa ajili ya klabu yake ya Real Madrid na yeye mwenyewe. Hadi sasa mambo si mabaya sana kwa nyota huyo wa Ureno, aliyeiongoza klabu yake kutwaa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania na pia kuibuka kinara kati ya wacheaji 50 waliokuwa wakiwania Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa mtandao wa habari za soka wa Goal.com (Goal.com 50).

Lakini, baada ya kupoteza tuzo ya Ballon d'Or kwa straika wa  Barcelona, Lionel Messi katika miaka mitatu iliyopita, Ronaldo sasa ana matarajio makubwa ya kutunukiwa tuzo hiyo yenye hadi kubwa zaidi duniani.

"Itakuwa na maana kubwa sana kwangu, nimejituma sana katika msimu wote uliopita ili kutwaa tuzo za pamoja na zangu binafsi," alisema.

Real Madrid hivi sasa iko katika ziara ya maandalizi ya msimu nchini Marekani ambako inacheza mechi kadhaa za kirafiki. Hadi sasa imeshacheza mechi tatu na kushinda zote dhidi ya LA Galaxy, Santos Laguna na AC Milan.

Baada ya kufunga mabao mawili jana na kuisaidia Real kuibuka na ushindi wa 5-1 dhidi ya Milan, kwenye Uwanja wa Yankee, Ronaldo alitajwa kuwa ndiye Mchezaji Bora wa Mechi.

Straika huyo alishangiliwa na maelfu ya mashabiki waliojazana uwanjani kila mara alipogusa mpira na alionekana kufurahia sana tuzo ya kuwa mcheaji bora wa mechi.

Ronaldo alishinda tuzo yake ya kwanza ya FIFA Ballon d'Or mwaka 2008 baada ya kuisaidia Manchester Untied kutwaa makombe mawili kwa mpigo, wakibeba taji la Ligi Kuu ya England na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.


OKWI AGOMBEWA SIMBA WAKITEMBELEA KITUO CHA YATIMA KINONDONI

Tupige picha mjukuu wangu... Babu na wadau wengine wakipiga picha na mshambuliaji nyota wa Simba, Emmanuel Okwi (katikati) wakati klabu hiyo ilipotembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo. PICHA: SANULA ATHANAS
Emmanuel Okwi akipiga picha na mtoto wakati klabu hiyo ilipotembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo. PICHA: SANULA ATHANAS

Okwi (katikati) akipozi na wadau wakati klabu hiyo ilipotembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo. PICHA: SANULA ATHANAS
Wachezaji wa Simba, Uhuru Selemani, Emmanuel Okwi na beki Juma Nyosso (kulia) wakipozi na wazee na watoto wakati klabu hiyo ilipotembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo. PICHA: SANULA ATHANAS
Okwi wa Simba akipozi na wadau wakati klabu hiyo ilipotembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo. PICHA: SANULA ATHANAS


Mashabiki wa Simba wakiwa katika picha ya pamoja na Okwi (wa pili kushoto),  Uhuru (wa nne) na Juma Nyosso wakati wahezaji na viongozi wa Simba walipotembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo . PICHA: SANULA ATHANAS

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' akiwa katika picha na Mlezi na Mwenyekiti wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Maunga, Bi. Zainab Bakari 'Maunga' na katibu wa kituo hicho, Rashid Mpinda wakati wahezaji na viongozi wa Simba walipotembelea kituo chao kilichopo Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo . PICHA: SANULA ATHANAS. PICHA: SANULA ATHANAS

Geofrey Nyange 'Kaburu'  akiwa katika kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo . PICHA: SANULA ATHANAS

Kaburu katikati akiwa na katibu wa kituo, Rashid Mpinda (kushoto) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Swedy Mkwabi wakati wahezaji na viongozi wa Simba walipotembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam leo . PICHA: SANULA ATHANAS
MSHAMBULIAJI Mganda Emmanuel Okwi alikuwa kivutio leo kwa watoto, vijana hadi wazee waliokuwa wakigombea kupiga picha naye wakati klabu yake ya Simba ilipotembelea kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Maunga Centre cha Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam.

Okwi, ambaye juzi alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Simba katika tamasha la klabu hiyo la Simba Day, aligombewa na mashabiki kituoni hapo ambapo watoto kwa wazee walitaka japo kupeana naye mikono au kupiga picha naye.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema wakati akizungumza na viongozi wa kituo hicho kuwa klabu yake imeanzisha utaratibu wa kuwa karibu na jamii na imeanzisha wiki maalum iitwayo 'Simba Week', ambayo itakuwa ikifanyika kila mwaka kuanzia Agosti 5-10.

Alisema Wiki ya Simba itakuwa ikihusisha nyota na viongozi wa klabu hiyo kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo kutembelea watu wenye mahitaji ambayo itakuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Simba Day. Siku ya Siomba hufanyika Agosti 8 kila mwaka.

Katika ziara hiyo Simba ilitoa msaada wa mchele Kg.310, mafuta ya kupikia lita 100, dawa za meno, sabuni na fedha taslimu Sh. 500,000 kwa ajili ya kusaidia watoto wanaolelewa kituoni hapo.

Juzi Jumanne, Simba walifanya ziara kama hiyo katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa hasa wodi ya akinamama na wajawazito.

CHELSEA WAMTAKA LLORENTE AMRITHI DIDIER DROGBA

Hili jamaa kupiga mabao nd'o zake.... hapa Llorente akishangilia baada ya kuwaliza Barcelona katika mechi ya Bilbao dhidi ya Barcelona kuwania Kombe la Mfalme,  Januari 5, 2011. Ilimalizika kwa sare ya 1-1.

Llorente hazuiliki kirahisi... hapa Gerard Pique wa Barcelona (kushoto) akijaribu kumkwatua bila mafanikio huku Eric Abidal akitazama. Llorente aling'ara sana katika mechi hii ya Kombe la Mfalme iliyochezwa Januari 5, 2011 na kuifungia Bilbao katika sare ya 1-1

Llorente ni 'tolu' kwelikweli... yaani hata Gerard Pique hampati kwa kwenda hewani na sifa hii pia inawavutia Chelsea katika harakati zao za kumpata straika wa kurithi nafasi ya Drogba.
LONDON, England
CHELSEA wameanza harajati za kumnasa straika nyota wa klabu ya Athletic Bilbao, Fernando Llorente ili atwae nafasi ya mshambuliaji wao aliyeondoka, Didier Drogba.

Gazeti la jioni jijini London, Evening Standard, limesema kuwa Llorente amekataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kumbakiza Athletic Bilbao.

Straika huyo mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5 anataka kuongezwa mshahara wake mara mbili ya ule anaoupata sasa na tayari amekataa ofa ya kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu baada ya Bilbao kumkatalia ombi lake.

Mkataba wa sasa wa mshambuliaji huyo unamalizika katika kipindi kijacho cha usajili wa majira ya kiangazi na inaelezwa kuwa anataka alipwe mshahara wa paundi za England 80,000 kwa wiki (Sh. nilioni 190) , wakati Bilbao wako tayari kumlipa paundi za England 60,000 tu kwa wiki (Sh. milioni 145)

Chelsea wanasaka mbadala wa Drogba na straika huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Hispania ana umbile kubwa na pia ni mpachikaji mzuri wa mabao, sifa ambazo zinafanana na za nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast aliyehamia klabu ya Shanghai Shenhua ya China.

Inaelezwa kuwa Bilbao wako tayari kumuachia Llorente kwa dau la takriban paundi za England milioni 15 (Sh. bilioni 36), hivyo kumpa nafasi kocha Roberto Di Matteo kufikiria kumsajili katika kipindi hiki anachojaribu kujenga kikosi kitakachoendeleza makali yaliyowapa mafanikio ya kutwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita.

MAN U WAKUBALI KUMLIPA ROBIN VAN PERSIE MSHAHARA WA KILA WIKI WA MILIONI 530/-

Van Persie akiwa mazoezini jana katika kambi ya Arsenal iliyopo Ujerumani kujiandaa na msimu mpya.  
LONDON, England
Man U wamekubali kumlipa straika Robin van Persie mshahara unolingana na Wayne Rooney ili kumsajili nahodha huyo wa mahasimu wao katika Ligi Kuu ya England, klabu ya Arsenal.

Gazeti la The Telegraph limesema leo kwamba utayari wa Man U kumlipa Van Persie mshahara wa wiki wa paundi za England 220,000 (Sh. milioni 533) kama anaoupata Rooney umetokana na nia yao ya kuhakikisha kwamba wawili hao wanakuwa na umuhimu unalingana.

Imeelezwa kuwa 'ofa' ya msharahara mnono kwa straika huyo wa kimataifa wa Uholanzi ambaye hivi sasa ana miaka 29, inaweza kumchanganya  Van Persie na kumuongezea kasi katika kutimiza dhamira yake ya kuondoka Arsenal.

KOCHA BARCELONA AKATAA KUZUNGUMZIA USAJILI WA ALEX SONG AKIHOFIA KUICHANGANYA ARSENAL

Alex Song
Tito Vilanova
STOCKHOLM, Sweden
KOCHA wa Barcelona, Tito Vilanova amekataa kuzungumzia mipango ya klabu yake katika kumsajili kiungo Alexandre Song kutokana na kile alichosema kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuivunjia heshima klabu inayommiliki kwa sasa ya Arsenal.

Hivi karibuni, Sergio Busquets na Andres Iniesta walisema kwamba wanavutiwa na kiungo huyo wa kimataifa wa Cameroon wakati walipulizwa kuhusiana na uwezo wake, lakini Vilanova ambaye ni kocha mpya wa Barca, aliamua kujiepusha na mjadala kuhusiana na mchezaji wa wapinzani wao hao barani Ulaya.

"Nipendi kuzungumzia wachezaji ambao si sheemu ya Barca. Nadhani ni ukosefu wa heshima kwa timu nyingine ikiwa nitazungumzia wachezaji ambao si mali ya Barcelona," Vilanova aliwaambia waandishi wa habari. "Yeyote atakayekuja kwetu ni lazima awe mchezaji mzuri, hilo ndio jambo muhimu kulitambua. Hakuna haraka."

Song, sasa akiwa na miaka 24, amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza cha Arsenal tangu alipojiunga nao Agosti, 2005 akitokea Bastia.

Mkataba wake na Arsenal unamalizika katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2015.

FERGUSON AKERWA LUCAS MOURA KUWATOSA NA KUFUATA MIJIHELA KIBAO PSG, ASEMA KLABU HIYO YA UFARANSA SASA INAHARIBU SOKA KWA KUMWAGA PESA KIWENDAWAZIMU....!!!

Kwa dau hilo mie basi... ! Kocha Alex Ferguson wa Man U
Lucas Moura... mijihela inayolipwa na PSG imemchanganya Ferguson 
MANCHESTER, England
KOCHA Alex Ferguson ameelezea mshangao wake baada ya Paris Saint-Germain kuishinda Manchester United katika mbio za kutaka kumsajili nyota wa Sao Paulo, Lucas Moura.

Kwa muda mrefu, Man U walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kumnasa yosso huyo mwenye miaka 19, lakini mwishowe mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil akakubali kujiunga na timu hiyo inayosifika kwa kumwaga fedha Ufaransa kwa mkataba wa miaka minne baada ya PSG kukubali kulipa dau nono walilotajiwa la euro milioni 45 (Sh. bilioni 86)

PSG tayari imeshamwaga fedha nyingi kusajili wachezaji kadhaa ghali katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, huku Thiago Silva, Zlatan Ibrahimovic na Ezequiel Lavezzi wote wakikubali kutua kwenye kikosi hicho cha kocha Carlo Ancelotti kinachopigania kutwaa taji lake la kwanza la Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa tangu mwaka 1994 na pia kutaka kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Ferguson anaamini kwamba matumizi makubwa ya PSG yanaharibu mchezo wa soka, hata hivyo, akikubali kwamba vigogo hao wa Ufaransa sasa ni wa kuchungwa sana kwani ni miongoni mwa klabu tishio katika soka la Ulaya.

Ameiambia tovuti rasmi ya klabu yake: "Nimeshangazwa kuona kwamba klabu inaweza kulipa hadi euro milioni 45 (Sh. bilioni 86) ili kumsajili mvulana wa miaka 19.

"IIli kumstua kila mmoja, ili kumfahamisha kila mtu kwamba PSG wapo, wamemsajili Thiago Silva na Zlatan Ibrahimovic kutoka AC Milan.

"Lazima watakuwa wameshatumia takriban paundi za England milioni 150 mwezi uliopita. Kma mjuavyo, kikwazo pekee kwa matumizi kama hayo ni UEFA.

"Katika masharti ya soka la Ulaya, hamtafuzu katika michuano ya Ulaya kwa kutwaa ubingwa wa ligi au kumaliza katika nafasi ya pili, mnashiriki pale tu mnapopata mwaliko.

"Hapa ndipo, natumaini iko hivyo, kwamba walau UEFA ina nguvu fulani. Wakati mtu anapolipa euro milioni 45 (Sh. bilioni 86)kwa ajili ya mvulana wa miaka 19, mnapaswa kusema tu kwamba sasa mchezo huu umekuwa wa kiuwendawazimu."

MOURINHO AKIRI KUBORONGA KWA KUMTIA KIDOLE CHA MACHO KOCHA TITO VILANOVA WA BARCELONA

Mourinho
NEW YORK, Marekani
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho amekiri kwamba alifanya makosa kumtia kidole cha macho kocha wa sasa wa Barcelona, Tito Vilanova wakati zilipoibuka vurugu za pembeni mwa mstari wa uwanja katika mechi yao ya kuwania taji la Hispania la Super Cup msimu uliopita.

Tukio hilo lilijiri mwanzoni mwa msimu uliopita wakati Vilanova akiwa msaidizi waPep Guardiola, ambapo mwishowe Real Madrid walichapwa kwa kipigo cha jumla cha mabao 5-4. Kufuatia tukio hilo, Mourinho alifungiwa mechi mbili, adhabu  ambayo hata hivyo ilifutwa hivi karibuni.

"Ni wazi kwamba sikupaswa kufanya vile nilivyofanya," alisema Mourinho wakati akiwa katika ziara ya klabu yake nchini Marekani.

"Hata hivyo, kulikuwa na sababu iliyonilazimisha kwa kiasi fulani kufikia hatua ya kushindwa kujizuia.

"Mtu aliyechemsha ni mimi, na siku hizi nimekuwa nikiwaeleza sana wachezaji wangu kwamba wao waendelee tu kucheza na kujizuia hasira zao."

Mreno huyo muongeaji amesema kwamba hakuna tena 'bifu' kati yake na Vilanova.

"Hakuna tena tatizo kati ya Tito na mimi," alisema.
"Tunasalimiana kila mmoja... shukrani, suala hilo limekwisha na lazima tuwe na matumaini ya kutotokea tena kwa matatizo kama hayo katika siku za usoni."

Huku fikra zake akizielekeza msimu ujao, kocha huyo mwenye miaka 49 alikuwa mwepesi kueleza kwamba malengo ya klabu yake ni kutwaa tena ubingwa wa La Liga na mwishowe kubeba taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

"Mwaka uliopita, tulitolewa Ulaya kwa penati tu. Tulikaribia, na kama tutaendelea kulipigania, siku moja tutalibeba," alisema.

Real Madrid walitolewa kwa penati katika hatua ya nusu fainali na waliokuja kuwa washindi wa pili, Bayern Munich.

BALOZI PROF. COSTA MAHALU ASHINDA KESI YAKE LEO NA KUACHIWA HURU

Prof. Mahalu (kushoto) akizungumza na Mwanasheria Alex Mgongolwa kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Balozi Prof. Mahalu (katikati) akitoka nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akiwa ameongozana na mdogo wake Mirasi Rama (kulia) na Wakili wa kujitegemea, Mabere Nyaucho Marando.(Picha: fatherkidevu.blogspot.com)
Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Prof.Costa Ricky Mahalu (63), ameachiwa huru mchana huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo baada ya kuonekana kuwa hana hatia katika kesi iliyokuwa ikimkabili yeye na afisa ubalozi Grace Martin, ya kuisababishia serikali hasara ya euro 2,065,827.60.

Akitoa hukumu yake,
Hakimu Mkazi Mfawidhi Illivin Mgeta amesema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutoa ushahidi wa kutosha kiasi cha kuwatia hatiani washtakiwa Mahalu na Grace.

Awali, hukumu ya kesi hiyo iliahirishwa mwezi uliopita na Hakimu Katemana, kwa maelezo kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mgeta aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo kukosekana kwavile alikuwa akikabiliwa na majukumu mengine.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na mawakili waandamizi wa serikali, Ponsiano Lukosi, Vincent Haule na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Linkolin, uliita mashahidi saba na vielelezo tisa vikiwemo mikataba miwili ya ununuzi wa jengo la ubalozi jijini Rome, Italia na upande wa utetezi uliita mashahidi watatu, akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.

MOURINHO: HAKUNA TIMU ITAKAYOTWAA UBINGWA IKIWA NA POINTI 100, MAGOLI ZAIDI YA 120 KAMA TULIVYOFANYA REAL MADRID


Jose Mourinho
NEW YORK, Marekani
JOSE Mourinho anaamini kuwa makali ya klabu yake ya Real Madrid kuelekea ubingwa wa msimu uliomalizika wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania 2011-12 yatabaki kuwa historia isiyovunjwa milele na klabu yoyote ile, wakiwamo wao wenyewe.

"Kwanza kabisa, sidhani kama kuna bingwa atakayefikisha tena pointi 100," Mourinho alisema katika mkutano na waandishi wa habari baada ya timu yake kuishindilia AC Milan mabao 5-1 katika mechi yao ya kirafiki ya maandalizi ya msimu jana jijini New York jana.

"Sidhani pia kama kuna bingwa atakayefunga magoli 120. Nadhani hizi ni takwimu zitakazodumu katika historia kwa muda mrefu sana."

Akizungumzia vita mpya kati ya Real Madrid na Barcelona kuwania taji la La Liga msimu ujao, kocha huyo Mreno alionekana kutambua kuwa mahasimu wao watakuwa wakali kama mbogo kutaka kutwaa ubingwa huo.

"Kila mmoja anajua kwamba kutakuwa na mchuano mkali sana, kwa mtazamo wangu, ni mchuano wa timu mbili zilizo bora zaidi duniani," kocha huyo wa zamani wa Chelsea alisema.

"Kwa sababu katika msimu uliopita tulikuwa na pointi nyingi sana na Barcelona walipata pointi nyingi pia, watu pengine wanaweza kudhania kwamba ligi (La Liga) sio ngumu sana."

Lakini Mourinho aliongeza kwamba watu ni lazima wafikirie zaidi ya timu hizo katika Ligi Kuu ya Hispania, akikumbushia kwamba fainali ya Ligi ya Europa ilizikutanisha timu mbili za Hispania.

"Nakumbuka kwamba fainali ya Europa ilikuwa ni kati ya Atletico Madrid na Atheltic Bilbao. Ligi hii (La Liga) ni ngumu, ngumu sana," alisema.

ONA CAZORLA, GIROUD, PODOLSKI WAKIJIFUA NA ARSENAL UJERUMANI

"Jembe" jipya la Gunners, Santiago Cazorla likishiriki mazoezi na timu yake ya Arsenal nchini Ujerumani ambako wameenda kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Ngoja nipashe ya mwisho mwisho kabla sijaenda Man United... Robin van Persie naye pia ameambatana na timu Ujerumani licha ya Sir Alex Ferguson kuthibitisha leo kwamba Manchester United imetuma ofa ya paundi milioni 15 kwa ajili ya kumsajili. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema Mholanzi huyo anauzwa paundi milioni 20.

Huyu naye anatakiwa na Barcelona... Alex Song akipozi kwa picha wakati wa mazoezi ya Arsenal nchini Ujerumani
Sijui nibaki hapa.....!?  RVP akishiriki mazoezi nchini Ujerumani

Msimu mpya si uanze tu, nina usongo.... Kiungo mpya wa Arsenal, Santiago Cazorla akiwa mazoezini na Arsenal nchini Ujerumani

Ngoja nipozi kwa picha... huyu ni Theodore Walcott
Mashine nyingine mpya... Lukas Podolski (kulia) akisimama jirani na Oxlade-Chamberlain
Pasha baba.... Cazorla akipasha
Ngoja nijipumzikie mie sina haja ya kujitesa kujua mbinu zake yule babu Wenger, maana sitarajii kuzitumia nikiwa Man United... RVP akipumzika
Yule RVP yaani nimemvumiliaaa wakati akisumbuliwa na majeraha kila mwaka, leo kapona ananiletea pozi, ntamnyima "razi" akafulie kama Hleb... Kocha Arsene Wenger akishiriki mazoezi ya Arsenal nchini Ujerumani.
Van Persie wewe ondoka tu mi nipate namba ya uhakika, nisije nikawa kama Chamakh bureee... Mshambuliaji mpya wa Arsenal, Olivier Giroud akishiriki mazoezi ya timu hiyo nchini Ujerumani
Ha ha haaaa.... Anatuchekesha sana RVP na hizo "nataka-sitaki" zake... Mabeki wa Arsenal, Laurent Koscielny (kushoto) na Verminator wakifurahia jambo wakati wa mazoezi ya timu yao nchini Ujerumani 
Kama Usain Bolt kudadadeki... Verminator akitoka nduki wakati wa mazoezi ya Arsenal nchini Ujerumani
Lazima uwe ngangari hapa, hata wakisvuta shati wewe uwe unakimbia tu... Cazorla (kulia) akikimbia huku akivutwa nyuma wakati wa mazoezi ya Arsenal nchini Ujerumani
Sijatwaa makombe miaka kibao, mwaka huu nikikosa tena naona watanitimua... Babu Wenger akiondoka uwanjani baada ya kumalizika kwa mazoezi
Santi Cazorla akipasha
Wachezaji wa Arsenal nchini Ujerumani
Mwenzenu hapa niko kwetu.... Lukas Podolski akifurahi wakati wa mazoezi ya Arsenal nchini kwao Ujerumani
RVP
Santiago Cazorla
Kiberenge cha Arsenal hiki... Alex Oxlade Chamberlain

MAJERUHI WANNE AJALI YA BASI LILILOPINDUKA HALI ZAO MBAYA, POLISI WASEMA LILIJAZA ABIRIA ZAIDI YA 110 WAKATI LIKIPINDUKA NA KUUA WATU 17, KUJERUHI 78.... MAITI SABA WATAMBULIWA...!

Basi la Sabena linavyoonekana baada ya kupinduka.
Abiria wanne kati ya majeruhi 78 walioumia katika ajali ya basi lililopinduka mkoani Tabora la Sabena wako katika hali mbaya huku hadi sasa waliothibitika kufariki dunia wakibaki kuwa 17.

Basi hilo aina ya Scania, lenye namba za usajili T 570 AAM, lilipinduka juzi mishale ya saa 6:30 mchana katika eneo la Kitunda, wilaya ya  Sikonge mkoani Tabora.

Akizungumzia ajali hiyo leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,  Anthony Rutta, amekaririwa akisema kuwa basi hilo lilijaza abiria kupita kiasi na kwamba, wakati likipinduka, ndani yake lilikuwa na abiria zaidi ya 110.

Majeruhi waliobaki bado wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Kitunda na jitihada za kuwahamishia katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete zinaendelea, lakini abiria 54 waliruhusiwa na kuendelea na safari yao.

Hadi kufikia leo, miili ya watu saba ilikuwa imetambuliwa, ambao ni askari Polisi PC Kheri wa Kituo Kikuu Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora, Vitus Tulumanye, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) tawi la Tabora; Farah Inga; raia wa Zimbabwe aliyekuwa akifanya kazi Tabora; Ikamba Thadeo; Damalu Goma;  Beatrice Kalinga, mwalimu wa Shule ya Msingi Igoko wilayani Uyui mkoani Tabora na aliyetambuliwa kwa jina moja la Madirisha ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi katika Wilaya ya Kaliua.


Mwalimu Madirisha anadaiwa alifuatana na watoto wanne na mkewe ambao bado hawajatambuliwa.

MANCHESTER UNITED HATIMAYE YATUMA MAOMBI RASMI ARSENAL YA KUMSAJILI ROBIN VAN PERSIE


Straika Van Persie
LONDON, England
MANCHESTER United wanajaribu kumsajili straika wa kimataifa wa Uholanzi, Robin Van Persie kutoka kwa mahasimu wao katika Ligi Kuu ya England, klabu ya Arsenal, amesema leo kocha Alex Ferguson.

"Tayari tumetuma maombi yetu," Ferguson ameiambia tovuti ya klabu yake (www.manutd.com).

"Tunajitahidi kumpata kadri inavyowezekana, lakini hadi kufikia wakati huu bado hatujapiga hatua.

"Hatutaki kuwasemea Arsenal. Sijui wanafikiria nini kwa sababu hawajatujibu chochote."

Van Persie alitangaza mwezi uliopita kwamba hataongeza mkataba wa kuendelea kuichezea Arsenal kwa sababu hakuwa akifurahishwa na mwelekeo wa klabu hiyo.

Straika huyo mwenye miaka 29, ambaye amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake, amekuwa na klabu ya Arsenal tangu mwaka 2004.

Van Persie alikuwa ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita katika Ligi Kuu ya England baada ya kufikisha mabao 30, matatu zaidi ya straika wa Man U, Wayne Rooney aliyemfuatia katika nafasi ya pili.

Msimu mpya utaanza Agosti 18.