Thursday, August 9, 2012

BALOZI PROF. COSTA MAHALU ASHINDA KESI YAKE LEO NA KUACHIWA HURU

Prof. Mahalu (kushoto) akizungumza na Mwanasheria Alex Mgongolwa kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Balozi Prof. Mahalu (katikati) akitoka nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akiwa ameongozana na mdogo wake Mirasi Rama (kulia) na Wakili wa kujitegemea, Mabere Nyaucho Marando.(Picha: fatherkidevu.blogspot.com)
Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Prof.Costa Ricky Mahalu (63), ameachiwa huru mchana huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo baada ya kuonekana kuwa hana hatia katika kesi iliyokuwa ikimkabili yeye na afisa ubalozi Grace Martin, ya kuisababishia serikali hasara ya euro 2,065,827.60.

Akitoa hukumu yake,
Hakimu Mkazi Mfawidhi Illivin Mgeta amesema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutoa ushahidi wa kutosha kiasi cha kuwatia hatiani washtakiwa Mahalu na Grace.

Awali, hukumu ya kesi hiyo iliahirishwa mwezi uliopita na Hakimu Katemana, kwa maelezo kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mgeta aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo kukosekana kwavile alikuwa akikabiliwa na majukumu mengine.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na mawakili waandamizi wa serikali, Ponsiano Lukosi, Vincent Haule na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Linkolin, uliita mashahidi saba na vielelezo tisa vikiwemo mikataba miwili ya ununuzi wa jengo la ubalozi jijini Rome, Italia na upande wa utetezi uliita mashahidi watatu, akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.

No comments:

Post a Comment