Thursday, August 9, 2012

NEYMAR: BRAZIL TUNABAHATI SANA GIOVANI DOS SANTOS HATACHEZA FAINALI OLIMPIKI

Neymar

LONDON, England
TAARIFA za kuwa majeruhi kwa Giovani dos Santos zimeifikia kambi ya Brazil, na uwezekano wa mchezaji huyo wa Tottenham kukosa mechi ya fainali ya Olimpiki ukawa ndio mjadala mkuu.

"Tutakuwa na bahati sana (kama hatacheza)", alisema Neymar kuiambia ESPN leo, saa chache kabla timu ya madaktari wa Mexico kuthibitisha kwamba ni kweli Dos Santos atakosa fainali.
 
Neymar ataingia katika fainali yake ya kwanza akiwa na Brazil katika ngazi yoyote, jambo linalomaanisha kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 atakuwa na jukumu la ziada la kuwa mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kuipa Brazil medali ya kwanza ya dhahabu.

"Itakuwa ni fainali yangu ya kwanza na Brazil na najivunia kuwa hapa kuiwakilisha nchi yangu katika kipindi muhimu kama hiki, fainali yetu ya kwanza ya Olimpiki katika miaka 24," alisema mshambuliaji huyo wa klabu ya Santos.

Kukiwa na kuongezeka kwa presha kutoka katika vyombo vya habari vya Brazil, medali ya fedha inachukuliwa kama haina maana yoyote na wachezaji na makocha kwa kipindi chote cha michuano hiyo, huku Neymar akikiri jambo hilo lakini pia akisema timu yao imepata mafanikio kufikia sasa.

"Ni lazima tuendelee kufanya tunayofanya katika michuano hii. Inazaa matunda," alisema.

Pamoja na Lucas Moura na Leandro Damiao, Neymar amekuwa mmoja wa nyota ambao Brazil inawategemea si tu kuleta dhahabu, bali pia kuirejesha timu ya wakubwa ya Brazil kileleni wakati watakapoandaa fainali za Kombe la Dunia 2014.

Huku Kombe la Dunia likiwa miaka miwili mbele, macho ya Neymar yako kwenye medali ya dhahabu.

"Hakuna Mbrazili aliyewahi kushinda taji hili katika soka na najiandaa kuisaidia timu yangu kuondoka na dhahabu," alimalizia.

No comments:

Post a Comment