Thursday, August 9, 2012

MOURINHO: HAKUNA TIMU ITAKAYOTWAA UBINGWA IKIWA NA POINTI 100, MAGOLI ZAIDI YA 120 KAMA TULIVYOFANYA REAL MADRID


Jose Mourinho
NEW YORK, Marekani
JOSE Mourinho anaamini kuwa makali ya klabu yake ya Real Madrid kuelekea ubingwa wa msimu uliomalizika wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania 2011-12 yatabaki kuwa historia isiyovunjwa milele na klabu yoyote ile, wakiwamo wao wenyewe.

"Kwanza kabisa, sidhani kama kuna bingwa atakayefikisha tena pointi 100," Mourinho alisema katika mkutano na waandishi wa habari baada ya timu yake kuishindilia AC Milan mabao 5-1 katika mechi yao ya kirafiki ya maandalizi ya msimu jana jijini New York jana.

"Sidhani pia kama kuna bingwa atakayefunga magoli 120. Nadhani hizi ni takwimu zitakazodumu katika historia kwa muda mrefu sana."

Akizungumzia vita mpya kati ya Real Madrid na Barcelona kuwania taji la La Liga msimu ujao, kocha huyo Mreno alionekana kutambua kuwa mahasimu wao watakuwa wakali kama mbogo kutaka kutwaa ubingwa huo.

"Kila mmoja anajua kwamba kutakuwa na mchuano mkali sana, kwa mtazamo wangu, ni mchuano wa timu mbili zilizo bora zaidi duniani," kocha huyo wa zamani wa Chelsea alisema.

"Kwa sababu katika msimu uliopita tulikuwa na pointi nyingi sana na Barcelona walipata pointi nyingi pia, watu pengine wanaweza kudhania kwamba ligi (La Liga) sio ngumu sana."

Lakini Mourinho aliongeza kwamba watu ni lazima wafikirie zaidi ya timu hizo katika Ligi Kuu ya Hispania, akikumbushia kwamba fainali ya Ligi ya Europa ilizikutanisha timu mbili za Hispania.

"Nakumbuka kwamba fainali ya Europa ilikuwa ni kati ya Atletico Madrid na Atheltic Bilbao. Ligi hii (La Liga) ni ngumu, ngumu sana," alisema.

No comments:

Post a Comment