Thursday, August 9, 2012

MOURINHO AKIRI KUBORONGA KWA KUMTIA KIDOLE CHA MACHO KOCHA TITO VILANOVA WA BARCELONA

Mourinho
NEW YORK, Marekani
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho amekiri kwamba alifanya makosa kumtia kidole cha macho kocha wa sasa wa Barcelona, Tito Vilanova wakati zilipoibuka vurugu za pembeni mwa mstari wa uwanja katika mechi yao ya kuwania taji la Hispania la Super Cup msimu uliopita.

Tukio hilo lilijiri mwanzoni mwa msimu uliopita wakati Vilanova akiwa msaidizi waPep Guardiola, ambapo mwishowe Real Madrid walichapwa kwa kipigo cha jumla cha mabao 5-4. Kufuatia tukio hilo, Mourinho alifungiwa mechi mbili, adhabu  ambayo hata hivyo ilifutwa hivi karibuni.

"Ni wazi kwamba sikupaswa kufanya vile nilivyofanya," alisema Mourinho wakati akiwa katika ziara ya klabu yake nchini Marekani.

"Hata hivyo, kulikuwa na sababu iliyonilazimisha kwa kiasi fulani kufikia hatua ya kushindwa kujizuia.

"Mtu aliyechemsha ni mimi, na siku hizi nimekuwa nikiwaeleza sana wachezaji wangu kwamba wao waendelee tu kucheza na kujizuia hasira zao."

Mreno huyo muongeaji amesema kwamba hakuna tena 'bifu' kati yake na Vilanova.

"Hakuna tena tatizo kati ya Tito na mimi," alisema.
"Tunasalimiana kila mmoja... shukrani, suala hilo limekwisha na lazima tuwe na matumaini ya kutotokea tena kwa matatizo kama hayo katika siku za usoni."

Huku fikra zake akizielekeza msimu ujao, kocha huyo mwenye miaka 49 alikuwa mwepesi kueleza kwamba malengo ya klabu yake ni kutwaa tena ubingwa wa La Liga na mwishowe kubeba taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

"Mwaka uliopita, tulitolewa Ulaya kwa penati tu. Tulikaribia, na kama tutaendelea kulipigania, siku moja tutalibeba," alisema.

Real Madrid walitolewa kwa penati katika hatua ya nusu fainali na waliokuja kuwa washindi wa pili, Bayern Munich.

No comments:

Post a Comment