Thursday, August 9, 2012

CHELSEA WAMTAKA LLORENTE AMRITHI DIDIER DROGBA

Hili jamaa kupiga mabao nd'o zake.... hapa Llorente akishangilia baada ya kuwaliza Barcelona katika mechi ya Bilbao dhidi ya Barcelona kuwania Kombe la Mfalme,  Januari 5, 2011. Ilimalizika kwa sare ya 1-1.

Llorente hazuiliki kirahisi... hapa Gerard Pique wa Barcelona (kushoto) akijaribu kumkwatua bila mafanikio huku Eric Abidal akitazama. Llorente aling'ara sana katika mechi hii ya Kombe la Mfalme iliyochezwa Januari 5, 2011 na kuifungia Bilbao katika sare ya 1-1

Llorente ni 'tolu' kwelikweli... yaani hata Gerard Pique hampati kwa kwenda hewani na sifa hii pia inawavutia Chelsea katika harakati zao za kumpata straika wa kurithi nafasi ya Drogba.
LONDON, England
CHELSEA wameanza harajati za kumnasa straika nyota wa klabu ya Athletic Bilbao, Fernando Llorente ili atwae nafasi ya mshambuliaji wao aliyeondoka, Didier Drogba.

Gazeti la jioni jijini London, Evening Standard, limesema kuwa Llorente amekataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kumbakiza Athletic Bilbao.

Straika huyo mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5 anataka kuongezwa mshahara wake mara mbili ya ule anaoupata sasa na tayari amekataa ofa ya kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu baada ya Bilbao kumkatalia ombi lake.

Mkataba wa sasa wa mshambuliaji huyo unamalizika katika kipindi kijacho cha usajili wa majira ya kiangazi na inaelezwa kuwa anataka alipwe mshahara wa paundi za England 80,000 kwa wiki (Sh. nilioni 190) , wakati Bilbao wako tayari kumlipa paundi za England 60,000 tu kwa wiki (Sh. milioni 145)

Chelsea wanasaka mbadala wa Drogba na straika huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Hispania ana umbile kubwa na pia ni mpachikaji mzuri wa mabao, sifa ambazo zinafanana na za nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast aliyehamia klabu ya Shanghai Shenhua ya China.

Inaelezwa kuwa Bilbao wako tayari kumuachia Llorente kwa dau la takriban paundi za England milioni 15 (Sh. bilioni 36), hivyo kumpa nafasi kocha Roberto Di Matteo kufikiria kumsajili katika kipindi hiki anachojaribu kujenga kikosi kitakachoendeleza makali yaliyowapa mafanikio ya kutwaa taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment