Thursday, July 26, 2012

SOMA TAARIFA MPYA KWA WANACHAMA WA MIFUKO KUHUSU FAO LA KUJITOA


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUSITISHWA KWA FAO LA KUJITOA

Irene Isaka, Mkurugenzi wa SSRA
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), inapenda kutoa ufafanuzi juu ya mafao ya kujitoa. Ufanunuzi huu unakwenda sambamba na taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na vyombo vya habari na kuleta mkanganyiko miongoni mwa Wanachama na Wadau wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.

Kufuatia hali hiyo, Mamlaka inatoa ufafanuzi ufuatao:
-   Marekebisho kuhusu kusitisha fao la kujitoa yamefanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha uzeeni.
-     Ni kweli kuwa Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Sheria ya Mamlaka zimefanyiwa marekebisho. Mchakato wa marekebisho hayo ulihusisha wadau kwa kuzingatia utatu yaani wawakilishi kutoka Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha waajiri pamoja na Serikali.
-     Kwa kutambua tofauti ya ajira, tofauti ya mazingira ya kazi, tofauti ya sababu za ukomo wa ajira, na umuhimu wa Mwanachama kunufaika na michango yake wakati angali katika ajira, Mamlaka inaendelea na mchakato wa kuandaa miongozo na kanuni za mafao ambazo lengo lake ni kuboresha maslahi ya Wanachama. Miongozo na kanuni hizo zitajadiliwa na Wadau wakiwemo Wafanyakazi, Waajiri na Serikali kabla ya kuanza kutumika.

-    Kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuiwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau.

-    Tangazo hili halitowahusu Wanachama waliojitoa kabla ya tarehe 20/07/2012.
-   Mamlaka inakanusha vikali kwamba, sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu za Kiserikali au kwa sababu mifuko imefilisika. Tunapenda kuwahakikishia kwamba Mifuko yote ipo thabiti na michango yote ya Wanachama ipo salama.

-    Hivyo, Mamlaka inawaomba Wanachama na Wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kuwa na utulivu wakati mchakato huu ukiendelea kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya Mwanachama.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji
SSRA-Makao Makuu

VIJANA NIGERIA HATIMAYE WATUA KUWAVAA NGORONGORO HEROES


HATIMAYE timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Nigeria (Flying Eagles) imewasili nchini leo mchana (Julai 26 mwaka huu) kwa ndege ya RwandAir ikiwa na msafara wa watu 32 wakiwemo wachezaji 18.

Awali timu hiyo ilikuwa iwasili jana jioni (Julai 25 mwaka huu) ikitokea Kigali, Rwanda lakini ikashindwa baada ya kuchelewa ndege. Flying Eagles itapambana na Ngorongoro Heroes katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili itakayofanyika Jumapili (Julai 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mechi hiyo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za 18 za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazochezwa mwakani nchini Algeria itachezeshwa na waamuzi kutoka Kenya wakati Kamishna ni Charles Masembe kutoka Uganda.

Flying Eagles ambayo iko chini ya kocha John Obuh, Julai 24 mwaka huu ilicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali na kufungwa bao 1-0.

Msafara wa timu hiyo unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF), Chris Green umefikia hoteli ya Rungwe iliyoko Mtaa wa Livingstone, maeneo ya Kariakoo.

Baadhi ya wachezaji walioko katika kikosi cha Flying Eagles ni Chidi Osuchukwu, Alhaji Gero, Shehu Abdullahi, Aminu Umar, Aliyu Mohamed, Uche Agbo, Jonah Usman, Harrison Egbune, Hassan Abubakar na Yahya Adamu.

Makocha wote, Jakob Michelsen wa Ngorongoro Heroes na Obuh wa Flying Eagles wakiwa na manahodha wao, Jumamosi (Julai 28 mwaka huu) saa 4 asubuhi watazungumza na waandishi wa habari juu ya walivyoviandaa vikosi vyao kwa ajili ya mechi hiyo. Mkutano huo utafanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A itakuwa sh. 10,000.

TFF, BENKI ABC ZAREJESHA KOMBE LA MUUNGANO

Benki ya ABC imesaini mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kudhamini michuano ya BancABC Super 8 inayoshirikisha timu nane, nne kutoka Tanzania Bara na nyingine nne kutoka Zanzibar.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo (Julai 26 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam ambapo Katibu Mkuu Angetile Osiah amesaini kwa niaba ya shirikisho wakati kwa upande wa ABC, saini yake iliwekwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo kwa Tanzania, Boniface Nyoni.

Mashindano hayo yataanza Agosti 4-18 mwaka huu yakichezwa katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar ambapo timu zote shiriki zitacheza katika vituo hivyo.

Uzinduzi rasmi wa mashindano hayo utafanywa Agosti 2 mwaka huu na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa benki ya ABC yenye makao yake makuu nchini Botswana, na ina matawi katika nchi za Msumbiji, Zambia, Tanzania, Zimbabwe.

Katika uzinduzi huo, CEO ataelezea thamani ya mkataba huo ambapo utahusisha gharama za malazi, usafiri, vifaa na uendeshaji wa mashindano hayo.

Akizungumza baada ya kutia saini, Osiah amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya TFF kuwa na mashindano mengi yatakayosaidia kuziandaa timu kabla ya kuanza Ligi Kuu.

Naye Nyoni amesema ABC imekubali kuingia kudhamini mpira wa miguu ikiwa ni lengo la kuchangia ustawi wa mchezo huo na kutoa sehemu ya faida wanayopata kwa kupitia michezo.

Timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni zile zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Ligi Kuu ya Zanzibar. Nyingine ni timu iliyoshika nafasi ya kwanza kwenye Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza ya Zanzibar ambazo nazo kwa kushika nafasi hizo zimeshaingia katika Ligi Kuu.

USALAMA WA TAIFA WAKANA KUMTEKA DK. ULIMBOKA


Mhe. George Mkuchika, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora)
Idara ya Usalama wa Taifa imekanusha taarifa zinazowahusisha na tukio la kutekwa, kuteswa na kumtupa kwenye msitu wa Mabwepande jijini Dar es Salaam kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka.

Taarifa iliyotolewa leo na idara hiyo imeeleza kuwa habari zinazodai kwamba ndio waliohusika kumteka Dk. Ulimboka ambaye hivi sasa anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini na nyingine zinazodai kuwa wana mpango wa kuwadhuru watu mbalimbali si za kweli, na kwamba wanaozisambaza wana lengo la kuichafua taasisi hiyo nyeti kwa usalama wa taifa.

Kwa sababu hiyo, taarifa hiyo imewataka wananchi kupuuza taarifa hizo, na kuwahakikishia Watanzania kuwa 'uzushi' huo hautawavunja moyo.

Imeeleza zaidi kwamba badala yake, Idara ya Usalama wa Taifa itaendelea kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya usalama katika kuhakikisha kuwa wakati wote nchi inakuwa salama.

Taarifa hiyo imetolewa leo ikiwa ni siku moja tu baada ya gazeti la Mwanahalisi la jana Jumatano (Julai 25, 2012) kuwatuhumu watu wa usalama wa taifa kuhusika na tukio la kumteka Dk. Ulimboka.
Katika habari hiyo, Mwanahalisi liliwataja kwa majina baadhi ya watu waliodaiwa kuwa ni maafisa wa idara hiyo waliohusika kumteka Dk. Ulimboka.

Dk. Ulimboka aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za mgomo wa madaktari uliotokea hivi karibuni, alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na kuumizwa vibaya kabla ya kukutwa kwenye msitu wa Mbawepande.

Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Slaam, Suleiman Kova alimtaja Mkenya Joshua Mhindi kuwa ndiye mtuhumiwa aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, akieleza kwamba walimtia mbaroni baada ya kubaini kuwa alikwenda katika Kanisa la Wokovu na Uzima la Mchungaji Gwejima lililopo Kawe jijini Dar es Salaam kwa nia ya kuungama huku akikiri kufanya tukio hilo na wenzake wa kundi la Gun Star.

Idara ya Usalama wa Taifa iko chini ya Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), ambayo inaongozwa na Mhe. George Mkuchika.

TUTAMLETA MSAIDIZI WA SUNZU - KABURU

Geofrey Nyange 'Kaburu'

Na Somoe Ng'itu
UONGOZI wa klabu ya Simba umewataka mashabiki wa timu yake kutokata tamaa baada ya kuondolewa katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na sasa wanajipanga kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaoanza Septemba Mosi.


Mabingwa hao wa Bara waliiaga michuano ya Kombe la Kagame Jumanne baada ya kufungwa magoli 3-1 na Azam katika mchezo wa robo fainali uliochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na STRAIKA leo, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kuwa Kamati ya Ufundi ya klabu hiyo inakutana kufanya tathmini ya timu yao na kikubwa ni kujaza nafasi ambazo zimeonekana zina mapungufu kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi.


Kaburu alisema kuwa kikosi cha Simba kina wachezaji wapya ambao walikuwa wakihitaji muda wa kujiandaa zaidi, jambo ambalo ndio lililowasumbua wakiwa kwenye michuano hiyo.


"Tunajipanga na tutahakikisha makosa yaliyoonekana katika mashindano ya Kagame yanafanyiwa kazi. Tusikate tamaa, Simba itakuwa bora msimu ujao licha ya kikosi kuondokewa na wachezaji muhimu," alisema kiongozi huyo.


Alisema katika usajili wao, watahakikisha wanaongeza beki mwingine wa kati aliye na uwezo pamoja na mshambuliaji ambaye atasadiana na Felix Sunzu katika ufungaji.


Wakati huo huo, tawi la Simba la Mpira Pesa lililoko Magomeni jijini Dar es Salaam, Jumapili litakuwa na mkutano wa wanachama wake ambapo wamepanga kujadili ushiriki wa timu yao kwenye mashindano ya Kombe la Kagame.

CAPELLO AWA KOCHA WA URUSI, AAHIDI MAKUBWA


Fabio Capello
MOSCOW, Urusi
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya England, Fabio Capello ameapa kubadili soka la Urusi na kuifanya timu ya taifa hilo kuwa moja ya timu kali duniani ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu hiyo leo.

Muitalia Capello anachukua nafasi ya Mholanzi Dick Advocaat, ambaye kibarua chake kiliota mbawa kufuatia matokeo mabaya waliyopata Urusi katika fainali za Euro 2012, ambazo waliishia katika hatua ya makundi.

Kocha huyo mwenye miaka 66, alionekana akiwa amevalia suti ya kijivu na tai ya bluu nyeusi. Hakuchelewa kuahidi mbele ya waandishi wa habari jijini Moscow kwamba atafanya kazi yake kwa ukamilifu.

"Najivunia kuwa kocha wa timu ya taifa ya Urusi. Kuna vipaji vingi Urusi. Nitaishi na kufanya kazi jijini Moscow," alisema.

Taarifa za vyombo vya habari vya Urusi zimedai kuwa atakuwa akilipwa mshahara wa euro milioni 10 kwa mwaka (Sh. bilioni 20)

NI YANGA NA AZAM FAINALI KAGAME, NGASSA ABUSU JEZI YA YANGA

Wachezaji wa Yanga wakishangilia baada ya kuifunga APR leo jioni.

Godfrey Taita (kushoto) wa Yanga akiukosa mpira mbele ya wachezaji wa APR kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni.

Ni raha tuuu.... Mashabiki wa Yanga wakisherehekea kutinga fainali baada ya kuilaza APR kwenye Uwanja wa Taifa leo jioni

Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet (kushoto) akizungumza na kocha wa APR, Arnie Brandts, wakati wa mechi ya timu zao leo jioni.

Winga Kipre Tchetche (kulia) akizuiwa na beki wa AS Vita wakati wa mechi yao iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa leo saa 8:00 mchana. Azam walishinda 2-1.

Hazuiliki huyu..... beki wa AS Vita akitafakari namna ya kumdhibiti mdunguaji  wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' katika mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.


Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga, watacheza fainali itakayokutanisha timu za Tanzania tupu dhidi ya Azam Jumamosi baada ya timu hizo kushinda mechi zao za nusu fainali kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.


Azam, ambao wanashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, walitangulia fainali baada ya kuifunga AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali iliyochezwa uwanjani hapo mapema leo mchana.


John Bocco alifunga bao lake la tano katika michuano hiyo kwa kichwa katika dakika ya 67, akisawazisha bao walilotanguliwa mapema dakika ya 35 kupitia kwa Alfred Mfongang, lakini winga aliyeingia kutokea benchi Mrisho Ngassa alifunga la ushindi katika dakika ya 88.


Mshambuliaji Hamis Kiiza 'Diego' aliifungia Yanga bao pekee la ushindi katika dakika ya 100 kufuatia krosi ya kiungo Haruna Niyonzima na kuwapeleka Yanga katika fainali ya pili mfululizo baada ya kurejeshwa katika michuano hiyo kufuatia kusamehemewa adhabu yao ya kifungo cha miaka mitatu wakiwa tayari wametumikia miaka miwili.


Hata hivyo, Yanga ambao katika kipindi cha pili walitawala mchezo hadi kwa asilimia 63 dhidi ya 37 za APR, walilalazimika kupambana kiume ili kujilinda baada ya kubaki 10 uwanjani kufuatia kutolewa kwa kadi ya pili ya njano kwa beki wao wa kulia, Godfrey Taita, kwa kuchelewesha mpira wakati tayari wakiwa mbele kwa bao 1-0.


Ngassa, ambaye anaonekana kukosa furaha katika kikosi hicho cha Azam kutokana na kusota benchi kufuatia nafasi yake uwanjani kuchukuliwa na winga mwenye nguvu wa Ivory Coast, Kipre Tchetche, alichochea tena uvumi kwamba anataka kurejea Yanga kufuatia kuvaa na kisha kuibusu jezi ya klabu yake ya zamani ya Yanga.


Hata hivyo, Kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall alipoulizwa na mtangazaji Thomas Mlambo wa kituo cha televisheni cha Supersport cha Afrika Kusini sababu za kutomuanzisha Ngassa, alisema: “Najua ni mchezaji mzuri, ninamuhitaji, lakini nataka ajitume zaidi.”


Kocha wa APR, Ernie Brandts, ambaye alishuhudia timu yake ikifungwa mechi ya pili na Yanga ndani ya wiki moja baada ya kulala 2-0 katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C Ijumaa iliyopita, alimlalamikia mwamuzi wa mechi hiyo akisema: “Hii ni Afrika. Mchezaji analala uwanjani kwa dakika sita lakini mwisho wa mechi zinaongezwa dakika tatu.”
Brandts alionekana kukerwa na mbinu za kupoteza muda za kipa wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’, aliyekuwa akilala chini mara kwa mara wakati wakiwa 10 uwanjani huku mechi ikielekea ukingoni.
“Goli limepatikana baada refa kuruhusu mechi iendelee wakati kulikuwa na faulo. Hii ni Afrika. Hii ni Afrika,” alilalamika Brandts.
Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet, hata hivyo, alimshangaa Brandts kudai timu yake ilionewa ilhali refa alifanya makosa kwa pande zote.


"Kama anadai kwamba kulikuwa na faulo kabla ya Yanga kurusha haraka mpira na kufunga goli, basi wachezaji wawili wa APR walipaswa kutolewa kwa kadi nyekundu katika tukio hilo.


"Mchezaji wangu katolewa kwa kadi nyekundu nyepesi wakati wachezaji wa APR wamecheza rafu nyingi, wamemuimiza beki wangu wa kulia (Juma Abdul aliyetoka dakika ya 27) na hawakufanywa kitu. Kama makosa refa alifanya na aliyafanya kwa pande zote.


“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri, lakini tulirejea vyema katika kipindi cha pili tukatawala mechi na hata katika dakika 30 za nyingeza, ni vizuri kumpongeza mshindi,” alisema Saintfiet, ambaye anaiongoza Yanga katika mechi zake za kwanza za kimashindano tangu akabidhiwe mikoba hivi karibuni kutoka kwa kocha Mserbia Kostadin Papic aliyemaliza mkataba wake.  


Kikosi cha Yanga kilikuwa: Ali Mustapha 'Barthez', Juma Abdul/ Shamte Ali (dk.27)/ Rashid Gumbo (dk.86), Godfrey Taita, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Oscar Joshua, Athuman Idd 'Chuji', Stephano Mwasika, Haruna Niyonzima, Said Bahanuz na Hamis Kiiza 'Diego'.


Kikosi cha Azam kilikuwa: Deogratias Munishi, Ibrahim Shikala, Erasto Nyoni, Said Moradi, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Tchetche/Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco 'Adebayor', Ibrahim Mwaipopo na Ramadhani Chombo 'Redondo'.

BOTI MV SEPIDEH NAYO YAPIGWA STOP ZANZIBAR


Boti ya Mv Sepideh ikiwa katika bandari ya Zanzibar tayari kwa kuanza safari.
Boti maarufu ya kusafirisha abiria ya Mv Sepideh nayo imefutiwa rasmi hati ya kufanya kazi visiwani Zanzibar leo na kuungana na boti nyingine za Mv Kalama na Mv Skagit zinazomilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Company Limited, imefahamika.  

Hatua hiyo imetangazwa leo na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar baada ya kubaini kwamba boti hizo hazikidhi vigezo vya kujihusisha na shughuli za kusafirisha abiria.

Boti ya Mv Sepideh ni miongoni vya vyombo maarufu kwa usafirishaji wa abiria kati ya jiji la Dar es Salaam na Zanzibar. 

Hatua ya kusimamishwa kwa boti hiyo na nyingine imekuja ikiwa ni siku chache tu baada ya tukio la kuzama kwa Mv. Skagit inayomilikiwa na Kampuni ya Seagull Sea Transport Company Limited katika eneo la Chumbe ikitokea jijini Dar es Salaam na kusababisha upotevu wa mali na vifo vya watu 123 hadi kufikia leo.

Kabla ya kuzama, boti ya Mv Skagit inadaiwa kwamba ilikuwa na watu 340.   

MAITI MV SKAGIT ZAFIKIA 123, LEO ZIMEPATIKANA MAITI 17 ZIKIWEMO TANO ZILIZOKUTWA ZIKIELEA BAGAMOYO


Zoezi la kuopoa miili zaidi ya watu waliokufa katika ajali ya kuzama kwa boti ya Mv Skagit Zanzibar bado limekuwa likiendelea
Idadi ya miili ya watu waliokufa baada ya kuzama kwa boti ya Mv Skagit katika eneo la Chumbe visiwani Zanzibar wakati ikitokea jijini Dar es Salaam wiki iliyopita sasa imefikia 123 baada ya miili mingine 17 kupatikana leo.

Taarifa zimeeleza kuwa katika miili iliyopatikana leo, wapo wanaume 13 na wanawake wanne, huku mmoja kati yao akiwa ni binti wa miaka 15.

Imeelezwa zaidi kwamba miili ya watu watano kati ya hao ilipatikana katika fukwe za Bagamoyo mkoani Pwani na tayari imeshazikwa wilayani humo.

Boti ya Mv Skagit inayomilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Company Limited ilipata ajali Julai 18 katika eneo la Chumbe visiwani Zanzibar, mishale ya saa 7:00 mchana huku ikiwa na watu zaidi ya 340.

Inadaiwa kwamba ilikumbwa na tukio hilo baada ya kupigwa na dhoruba kali, kupinduka na kisha kuzama yote baharini.

Juhudi za kuifikia boti hiyo ili kupata miili zaidi ya watu wanaoweza kuwa walinasia ndani yake zinaelezwa kuwa ngumu kwani imezama chini kabisa kwa umbali unaokadiriwa kuwa ni wa kina cha zaidi ya mita 60 wakati uwezo uliopo ni wa binadamu kuzamia kwa kina cha mita 30 pekee.




NYOTA WAWILI WAPYA BARCA NJE MIEZI MITATU, SITA

Kiungo mpya wa Barcelona, Edgar le akiwa na magongo baada ya kuumia.

BARCELONA imekiri kwamba kiungo wao mpya waliyemsajili wiki iliyopita kutoka  Sporting Lisbon, Edgar Ie, atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu.

Klabu hiyo imesema kuwa Edgar Ie atakuwa nje ya uwanja kutokana na kufanyiwa upasuaji wa mguu.

Edgar alitua Barcelona wiki iliyopita pamoja na Agostinho Ca wote wakitokea Sporting kwa mkataba wa miaka minne kila mmoja.

Aidha, kiungo mwingine wa Barca, Marc Muniesa huenda akakaa nje ya uwanja kwa miezi sita baada ya kuumia goti katika mechi ya kirafiki waliyoshinda 2-1 dhidi ya Hamburg juzi.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Hispania ya vijana wa umri chini ya miaka 21, alipata majeraha hayo mwanzoni mwa kipindi cha pili cha mechi hiyo na vipimo vimethibitisha kwamba ameumia kwa ndani goti lake la kulia.

Itaamuliwa ndani ya siku chache ni lini kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 ataenda kufanyiwa upasuaji lakini anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa miezi sita, Barca ilitangaza katika tovuti yao.

DANI ALVES HAUZWI - VILANOVA

Dani Alves

KOCHA wa Barcelona, Tito Vilanova amesisitiza kwamba bado anamtegemea beki wa kulia Daniel Alves.

Beki huyo aliishangaza menejimenti wiki iliyopita kwa kudai kwamba "anakosa sapoti" wakati uvumi kwamba atauzwa ukiwa juu.

"Hatujawahi kufikiria kumpoteza Alves," alisisitiza Vilanova.

"Ilikuwa ni juu ya mjadala ndani ya klabu.

"Yeye ndiye beki wa kulia bora zaidi duniani, mmoja wa wachezaji bora kabisa waliopata kusajiliwa na Barcelona katika miaka ya karibuni na mmoja wa wachezaji ambao ni muhimu zaidi katika kuchezesha timu yetu."

TAZAMA RATIBA YA SAA ZA KUANZA KUFUNGA NA KUFUTURU MWEZI HUU MTUKUFU WA RAMADHANI ILIYOIDHINISHWA NA BAKWATA

N.B: Ratiba hii imepitishwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Mida iliyoonyeshwa ni kwa ukanda wa Pwani. Unakumbushwa kuhakiki muda wa mji uliopo.