Tuesday, June 19, 2012


BINTI WA BOBBY BROWN AKACHA HARUSI YA BABA YAKE



WAKATI wa mapumziko mafupi ya ziara ya kundi la New Edition, msanii Bobby Brown aliamua kumuoa mpenzi wake wa ‘long taim kitambo’, Alicia Etheredge, tukio lililofanyika Honolulu, juzi Jumatatu.

Cha kusikitisha, ingawa tukio hilo lilikuwa ni la kifamilia, binti wa gwiji huyo, Bobbi Kristina Brown hakushiriki tukio hilo.

Brown, 43, mkali wa muziki wa R&B aliyemchumbia Etheredge tangu mwaka 2010, alisema "Nimekubali" mbele ya ndugu na marafiki, wakiwemo wanawe wakubwa Landon, 23, La'Princia, 22, na Bobby Jr., 19, na kitinda mimba wake aliyezaa na Etheredge: Cassius, 3.

Bobbi Kristina, binti yake aliyezaa marehemu Whitney Houston, hakuonekana katika harusi hiyo.

Taarifa zimedai kwamba Bobbi Kristina anapiga picha za kipindi chake kipya cha luninga jijini New York na hivyo ameamua ‘kuipotezea’ harusi ya baba yake.

Imeelezwa zaidi kuwa hivi sasa, Bobby Brown na binti yake huyo hawapikiki chungu kimoja.

Hata hivyo, licha ya kutokuwepo kwa Bobbi Kristina, sherehe hizo zilifanyika kama zilivyopangwa. Bobby alivalia suti iliyokuwa na rangi nyekundu na shati la rangi ya maziwa.

Cassius, aliyeshika pete ya ndoa, alivalia kama baba yake lakini akaongezea na ‘skafu’ shingoni mwake. Bobby Jr. alipiga picha nyingi za harusi hiyo, ikiwemo ya mabinti wanne walioshikilia maua.

Kabla ya kuchumbiana mwaka 2010 (suala ambalo Bobby alikuwa mkali kila mara alipoulizwa wakati wa maonyesho yake, wapenzi hao ‘walijirusha’ kwa miaka mitatu na kumzaa Cassius mwaka 2009. Uhusiano wake na Etheredge, ambaye pia ni meneja wake, ndio wa kwanza uliodumu zaidi baada ya kutalikiana na Houston mwaka 2007.

"Nimefahamiana na Alicia kwa miaka kadhaa," Bobby aliwahi kusema mwezi uliopita.
"Tulikutana zamani sana, wakati akijifunza unenguaji. Alikuwa ni miongoni mwa wacheza shoo. Tukawa pamoja L.A... tukapotezana baada ya mimi kuoa. Lakini mara tu nilipotalikiana (na Houston), nikaonana naye tena na kuanza naye upya … ni mwanamke bomba. Nampenda sana. Mapenzi yangu kwake ni makubwa zaidi ya niliyo nayo kwa mtu mwingine yeyote," alisema Brown.

-------


CROATIA WAPIGWA FAINI KWA KUMBAGUA BALOTELLI

Mario Baloteli akifunga goli la pili la timu ya taifa ya Italia dhidi ya Jamhuri ya Ireland wakati wa mechi yao ya Kundi C la UEFA EURO 2012 kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Poznan, Poland jana.

WARSAW, Poland
SHIRIKISHO la soka la Croatia limepigwa faini ya Euro 80,000 (sawa na Tsh. milioni 157) na UEFA leo kutoka na nyimbo za kibaguzi zilizoelekezwa na mashabiki wao kwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Italia, Mario Balotelli wakati wa mechi yao ya Kundi C la michuano ya Euro 2012 mjini Poznan Alhamisi iliyopita.

"Shirikisho la soka la Croatia (HNS) limetozwa faini ya euro 80,000 kwa kitendo cha mashabiki wake kuwasha na kurusha mafataki, na matendo yasiyokubalika (nyimbo za kibaguzi, ishara za kibaguzi) wakati wa mechi yao ya Kundi C la UEFA Euro 2012 dhidi ya Italia," UEFA ilisema katika taarifa yake.

Faini hiyo ya fedha ni euro 20,000 pungufu ya faini aliyotozwa mshambuliaji wa Denmark, Nicklas Bendtner kwa kuonyesha nembo ya kampuni ya kubashiri matokeo kwenye chupi yake wakati akishangilia katika mechi ya Euro 2012.

Kitendo hicho kilishambuliwa na beki wa Manchester United, Rio Ferdinand aliyehoji kama UEFA na rais wao Michel Platini wanajielewa kutokana na tofauti kubwa iliyopo baina ya adhabu zinazotolewa kwa wanaofanya vitendo vya kibaguzi na wa makosa mengine mchezoni. "Ni jambo gani lililobaya zaidi -- kutangaza biashara ama kubagua?" alihoji.

UEFA imesema imetoa muda wa siku tatu wa kukataa rufaa kwa Croatia, ambao walitolewa katika michuano hiyo kufuatia kipigo kutoka kwa Hispania katika mechi yao ya mwisho ya kundi jana.

Mtandao wa kupambana na ubaguzi wa rangi katika soka Ulaya wa Football Against Racism in Europe (FARE), ambao unafanya kazi kwa karibu na UEFA na una waangalizi katika mechi zote za Euro 2012, ulisema baina ya mashabiki 300 na 500 wa Croatia walihusika katika kumfanyia vitendo vya kibaguzi Balotelli.

KENYA YAMTIMUA KOCHA KIMANZI, BENCHI LA UFUNDI

Kocha aliyetimuliwa Harambee Stars, Francis Kimanzi.

NAIROBI, Kenya
KENYA imemtimua kocha Francis Kimanzi kutoka ajira yake leo na kutimua pia watu wote wa benchi lake la ufundi kufuatia matokeo mabaya katika mechi zao tatu za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika.

Timu hiyo ilitoka sare dhidi ya Malawi mjini Nairobi Juni 2 na ikalala kwa Namibia siku nane baadaye katika mechi mbili za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.

Kenya kisha walilala 1-0 kwa Togo, na kuzima ndoto zao kucheza fainali za Mataifa ya Afrika 2013.
"Kamati Kuu ya taifa ilifanya mkutano leo na kuamua kuliondoa benchi zima la ufundi mara moja," alisema mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Sam Nyamweya katika taarifa.

"Francis Kimanzi sasa ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa ufundi wa muda kuchukua nafasi ya Patrick Naggi ambaye amekuwa afisa mtendaji waFKF."

JUMA NATURE, ROMA, MWASITI KUPAMBA AIRTEL Supa5 MWANZA


Wasanii wa kundi la kudansi la Kinoko, maarufu kama Comedy Dance, wakifanya vitu vyao wakati wa Tamasha la Airtel Supa5 katika viwanja vya NMC mjini Arusha wiki iliyopita. Wasanii hao watakuwepo pia katika tamasha hilo jijini Mwanza wikiendi hii.

Rapa Juma Nature wa kundi la Wanaume Halisi (kushoto) akitumbuiza mbele ya umati wa mashabiki wakati wa tamasha maalum la kuitambulisha huduma ya Airtel Supa5 kwenye viwanja vya NMC mkoani Arusha mwishoni mwa wiki. Nature atakuwepo mjini Mwanza wikiendi hii katika mwendelezo wa tamasha hilo.

Mwasiti (kulia) akitumbuiza mashabiki wakati wa tamasha maalum la kuitambulisha huduma ya Airtel Supa5 kwenye viwanja vya NMC mkoani Arusha mwishoni mwa wiki. Mwasiti pia atakuwepo mjini Mwanza wikiendi hii katika mwendelezo wa tamasha hilo.

Na Mwandishi Wetu
TAMASHA la burudani maalum kwa ajili ya kuitambulisha huduma ya Airtel Supa5 mikoani litaendelea mwishoni mwa wiki hii kwa burudani ya aina yake katika viwanja vya wazi vya Furahisha vilivyopo jijini Mwanza.

Afisa Uhusiano wa Airtel, Jane Matinde alisema lengo la kuunganisha utambulisho huo na burudani ni kuwavutia vijana na wateja wengi kuhudhuria na kujifunza faida lukuki za SUPA5 ili waitumie zaidi.

"Tamasha linafanyika kwa siku mbili mfululuzizo ambapo siku ya Jumamosi tunatoa fursa kwa wasanii chipukizi kujitokeza kwa wingi kuonyesha vipaji vyao sambamba na  kupata huduma ya Airtel SUPA5.

"Jumapili itakuwa uzinduzi kamili ambapo wasanii wakubwa watatoa burudani bure, akiwemo Juma Nature na kundi zima la Wanaume Halisi, Mwasiti a.k.a Soja, Roma Mkatoliki, watatoa burudani kali kwa wateja watakaohuduria tamasha hilo la bure.

Huduma ya Airtel SUPA5 ilizinduliwa rasmi siku za karibuni jijini Dar es Salaam na kisha kufuatiwa na matamasha ya burudani ya bure katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa, Arusha.

Wasanii nyota waliokwishapamba majukwaa ya Airtel SUPA5 hadi sasa ni Chege,  Temba, Fid Q, Mwasiti, Godzillah, kundi la Tip Top Connection akiwemo Madii, Tundaman, Richard na Dogo Janja na bendi maarufu jijini ya Mashujaa ikiongozwa na muimbaji nyota Chaz Baba.

--------------



VIDEO MPYA YA BANANA Ft. DOGO ASLAY  YATOKA

Banana Zorro (kulia) akiimba pamoja na baba yake mzazi Zahir Ali Zorro wakati wa moja ya maonyesho ya B-Band.

Na Ramadhani Mbwaduke
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini na mkurugenzi wa bendi yake mwenyewe inayokwwenda kwa jina la B-Band, Banana Zahir Zorro, ameachia video ya wimbo wake mpya wa ‘Nunda’ aliouimba akimshirikisha  msanii anayeinukia vyema Dogo Aslay.
Banana ameiambia Blog ya STRAIKA kuwa wimbo huo umerekodiwa na studio ya Soundcrafters wakati video imefanywa na kampuni inayoaminika kuwa bora zaidi nchini ya Visual Lab chini ya muongozaji Adam Juma.  
“Ni wimbo mzuri sana, nina furaha kwamba mashabiki wangu wanaweza kupata kitu kipya baada ya kusubiri kwa muda kidogo,” amesema Banana.
Muimbaji huyo anayetamba na nyimbo kama ‘Nzela’, ‘Mama Kumbena’ na ‘Zoba’, amesema mambo wimbo huo mpya na nyingine zake zote zinapatikana katika maonyesho ya B-Band kila wiki.
B-Band ambayo pia inamjumuisha baba yake mzazi, gwiji wa muziki nchini Zahir Ali Zorro, inatumbuiza  kila Alhamisi hutumbuiza kwenye ukumbi wa Q-Bar uliopo Oysterbay jijini Dar es Salaam,  Ijumaa wanapatikana Arabella, Masaki jijini Dar es Salaam wakati siku ya Jumamosi huitumia kutumbuiza kwenye maeneo mbalimbali kulingana na mialiko.

SOMO KWA WASANII WA FILAMU HILI HAPA

Waigizaji nyota nchini Jacqueline Wolper (kushoto) na Jacob Steven a.k.a JB wakiwa katika pozi la kasha la filamu yao ya "Dereva Taxi". Wasanii hao wanajihusisha pia na uongozaji wa filamu.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na asasi ya Gaba Arts mapema wiki hii wameendesha semina fupi kwa wasanii wa filamu ili kuwajengea weledi katika eneo la uandishi bora wa miswada ya sinema (script writing).

Semina hiyo iliyoendeshwa kupitia programu ya Jukwaa la Sanaa kwenye Ukumbi wa BASATA ilijikita katika maeneo ya namna ya kuendeleza wazo hadi sinema ya kusisimua, namna ya kufikia hisia za watazamaji, ujenzi mzuri wa matukio, kutengeneza wahusika na mfumo wa hadithi, mwanzo, kati na hitimisho.

Akitoa mada kwenye programu hiyo maalum, mkurugenzi wa asasi ya Gaba Arts, James Gayo alisema kuwa muda umefika sasa kwa wasanii wa filamu kusaka maarifa ili kutengeneza sinema zenye visa vipya, zenye weledi na zisizosukumwa na matakwa au maelekezo ya wasambazaji.

"Wenzetu kutoka nje wanatamani sana kupata vitu kutoka Afrika vyenye kuzungumza uhalisia wa maisha ya kwetu, wanataka kuona vitu vipya hivyo, katika uandishi wa muswada wa sinema suala la uhalisia na visa vyenye utofauti ni la msingi sana," alisisitiza Gayo.

Alizidi kueleza kuwa watazamaji wa sinema (filamu) huwa wana kawaida ya kuchoka pale wanapolishwa visa vya aina moja muda wote na akaonya kuwa kama wasanii hawatajikita katika kubuni visa vipya na vyenye kugusa uhalisia wa maisha yao wadau watasusia kununua.

"Ikiwa tutaendelea kutengeneza filamu zisizo na weledi, zenye visa vilevile na zenye kusukumwa na wasambazaji au haja ya kuchuma fedha za haraka tu, watu watatuchoka na baadaye soko litakufa," alionya Gayo.

Gayo ambaye amepitia mafunzo ya utengenezaji filamu katika mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani alitaja sifa za muswada (script) bora kuwa ni pamoja na kubeba wazo linalozalika kwenye jamii, visa vyenye uhalisia na vipya, utengenezaji mzuri wa wahusika na sifa zingine nyingi.

Kwa upande wake msanii wa mashairi Mrisho Mpoto ambaye alikuwa miongoni mwa waliohudhuria semina hiyo alisema kuwa, wasanii wa filamu wanahitaji kusaidiwa kwani kwa sasa soko la filamu limekuwa la kitumwa na lenye kuburuzwa na matakwa ya wasambazaji bila weledi.

Akihitimisha programu hiyo, Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alishauri wasanii wa filamu kujipanga kushirikiana na wasomi wenye weledi katika maeneo yao ili kuzalisha kazi zenye weledi la ubora.

"Tuna wataalam wengi katika Sanaa, wamebanana na mambo mengi lakini ni vema wasanii tukawatumia na kushirikiana nao katika kuboresha kazi zetu," alisisitiza Materego.

HISPANIA, ITALIA ZAPETA EURO 2012
Mario Balotelli wa Italia (wa pili kulia) akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kufunga goli dhidi ya Ireland usiku huu.
Balotelli akifunga goli lake kwa shuti la tik-taka

WARSAW, Poland
MABINGWA watetezi Hispania wamemaliza kileleni mwa Kundi C usiku huu baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Croatia wakati Italia waliungana nao pia kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya Euro 2012 kutokana na ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Ireland.
Hispania walikuwa na hatihati ya kuadhiriwa katika mechi yao mjini Gdansk ambako bao la kutangulia la Croatia lingeweza kuwang'oa katika fainali hizo, lakini Jesus Navas aliwafungia goli la 'usiku' wakati zikiwa zimebaki dakika mbili kabla mechi kumalizika na kuwaweka kileleni mwa msimamo ambapo sasa watacheza dhidi ya timu itakayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D.
Katika mechi ya jana, Hispania walimiliki mpira kwa asilimia 76 na kupiga mashuti 14 dhidi ya mashuti matano ya Croatia.
Waitalia walifunga bao lao la kwanza katika dakika ya 35 mjini Poznan wakati mpira wa kichwa wa Antonio Cassano aliounganisha kutokana na kona ulivuka mstari wa goli na shaka yao ya kushikiliwa na Ireland waliokuwa tayari wameshatolewa ilimalizwa na goli 'kali' la Mario Balotelli muda mfupi baada ya Keith Andrews wa Ireland kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Kwa ushindi huo, Italia sasa watacheza mechi yao ya robo fainali dhidi ya timu itakayomaliza kileleni mwa Kundi D, ambalo hadi sasa linaongozwa na Ufaransa na mechi zake zitahitimishwa leo Jumanne.
Katika mechi za Kundi D leo, Sweden watacheza dhidi ya Ufaransa na wenyeji Ukraine watawavaa England, zote zikichezwa kuanzia saa 3:45 usiku.