Tuesday, June 19, 2012

CROATIA WAPIGWA FAINI KWA KUMBAGUA BALOTELLI

Mario Baloteli akifunga goli la pili la timu ya taifa ya Italia dhidi ya Jamhuri ya Ireland wakati wa mechi yao ya Kundi C la UEFA EURO 2012 kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Poznan, Poland jana.

WARSAW, Poland
SHIRIKISHO la soka la Croatia limepigwa faini ya Euro 80,000 (sawa na Tsh. milioni 157) na UEFA leo kutoka na nyimbo za kibaguzi zilizoelekezwa na mashabiki wao kwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Italia, Mario Balotelli wakati wa mechi yao ya Kundi C la michuano ya Euro 2012 mjini Poznan Alhamisi iliyopita.

"Shirikisho la soka la Croatia (HNS) limetozwa faini ya euro 80,000 kwa kitendo cha mashabiki wake kuwasha na kurusha mafataki, na matendo yasiyokubalika (nyimbo za kibaguzi, ishara za kibaguzi) wakati wa mechi yao ya Kundi C la UEFA Euro 2012 dhidi ya Italia," UEFA ilisema katika taarifa yake.

Faini hiyo ya fedha ni euro 20,000 pungufu ya faini aliyotozwa mshambuliaji wa Denmark, Nicklas Bendtner kwa kuonyesha nembo ya kampuni ya kubashiri matokeo kwenye chupi yake wakati akishangilia katika mechi ya Euro 2012.

Kitendo hicho kilishambuliwa na beki wa Manchester United, Rio Ferdinand aliyehoji kama UEFA na rais wao Michel Platini wanajielewa kutokana na tofauti kubwa iliyopo baina ya adhabu zinazotolewa kwa wanaofanya vitendo vya kibaguzi na wa makosa mengine mchezoni. "Ni jambo gani lililobaya zaidi -- kutangaza biashara ama kubagua?" alihoji.

UEFA imesema imetoa muda wa siku tatu wa kukataa rufaa kwa Croatia, ambao walitolewa katika michuano hiyo kufuatia kipigo kutoka kwa Hispania katika mechi yao ya mwisho ya kundi jana.

Mtandao wa kupambana na ubaguzi wa rangi katika soka Ulaya wa Football Against Racism in Europe (FARE), ambao unafanya kazi kwa karibu na UEFA na una waangalizi katika mechi zote za Euro 2012, ulisema baina ya mashabiki 300 na 500 wa Croatia walihusika katika kumfanyia vitendo vya kibaguzi Balotelli.

No comments:

Post a Comment