Tuesday, June 19, 2012


BINTI WA BOBBY BROWN AKACHA HARUSI YA BABA YAKEWAKATI wa mapumziko mafupi ya ziara ya kundi la New Edition, msanii Bobby Brown aliamua kumuoa mpenzi wake wa ‘long taim kitambo’, Alicia Etheredge, tukio lililofanyika Honolulu, juzi Jumatatu.

Cha kusikitisha, ingawa tukio hilo lilikuwa ni la kifamilia, binti wa gwiji huyo, Bobbi Kristina Brown hakushiriki tukio hilo.

Brown, 43, mkali wa muziki wa R&B aliyemchumbia Etheredge tangu mwaka 2010, alisema "Nimekubali" mbele ya ndugu na marafiki, wakiwemo wanawe wakubwa Landon, 23, La'Princia, 22, na Bobby Jr., 19, na kitinda mimba wake aliyezaa na Etheredge: Cassius, 3.

Bobbi Kristina, binti yake aliyezaa marehemu Whitney Houston, hakuonekana katika harusi hiyo.

Taarifa zimedai kwamba Bobbi Kristina anapiga picha za kipindi chake kipya cha luninga jijini New York na hivyo ameamua ‘kuipotezea’ harusi ya baba yake.

Imeelezwa zaidi kuwa hivi sasa, Bobby Brown na binti yake huyo hawapikiki chungu kimoja.

Hata hivyo, licha ya kutokuwepo kwa Bobbi Kristina, sherehe hizo zilifanyika kama zilivyopangwa. Bobby alivalia suti iliyokuwa na rangi nyekundu na shati la rangi ya maziwa.

Cassius, aliyeshika pete ya ndoa, alivalia kama baba yake lakini akaongezea na ‘skafu’ shingoni mwake. Bobby Jr. alipiga picha nyingi za harusi hiyo, ikiwemo ya mabinti wanne walioshikilia maua.

Kabla ya kuchumbiana mwaka 2010 (suala ambalo Bobby alikuwa mkali kila mara alipoulizwa wakati wa maonyesho yake, wapenzi hao ‘walijirusha’ kwa miaka mitatu na kumzaa Cassius mwaka 2009. Uhusiano wake na Etheredge, ambaye pia ni meneja wake, ndio wa kwanza uliodumu zaidi baada ya kutalikiana na Houston mwaka 2007.

"Nimefahamiana na Alicia kwa miaka kadhaa," Bobby aliwahi kusema mwezi uliopita.
"Tulikutana zamani sana, wakati akijifunza unenguaji. Alikuwa ni miongoni mwa wacheza shoo. Tukawa pamoja L.A... tukapotezana baada ya mimi kuoa. Lakini mara tu nilipotalikiana (na Houston), nikaonana naye tena na kuanza naye upya … ni mwanamke bomba. Nampenda sana. Mapenzi yangu kwake ni makubwa zaidi ya niliyo nayo kwa mtu mwingine yeyote," alisema Brown.

-------


No comments:

Post a Comment