Tuesday, June 19, 2012


HISPANIA, ITALIA ZAPETA EURO 2012
Mario Balotelli wa Italia (wa pili kulia) akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kufunga goli dhidi ya Ireland usiku huu.
Balotelli akifunga goli lake kwa shuti la tik-taka

WARSAW, Poland
MABINGWA watetezi Hispania wamemaliza kileleni mwa Kundi C usiku huu baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Croatia wakati Italia waliungana nao pia kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya Euro 2012 kutokana na ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Ireland.
Hispania walikuwa na hatihati ya kuadhiriwa katika mechi yao mjini Gdansk ambako bao la kutangulia la Croatia lingeweza kuwang'oa katika fainali hizo, lakini Jesus Navas aliwafungia goli la 'usiku' wakati zikiwa zimebaki dakika mbili kabla mechi kumalizika na kuwaweka kileleni mwa msimamo ambapo sasa watacheza dhidi ya timu itakayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D.
Katika mechi ya jana, Hispania walimiliki mpira kwa asilimia 76 na kupiga mashuti 14 dhidi ya mashuti matano ya Croatia.
Waitalia walifunga bao lao la kwanza katika dakika ya 35 mjini Poznan wakati mpira wa kichwa wa Antonio Cassano aliounganisha kutokana na kona ulivuka mstari wa goli na shaka yao ya kushikiliwa na Ireland waliokuwa tayari wameshatolewa ilimalizwa na goli 'kali' la Mario Balotelli muda mfupi baada ya Keith Andrews wa Ireland kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Kwa ushindi huo, Italia sasa watacheza mechi yao ya robo fainali dhidi ya timu itakayomaliza kileleni mwa Kundi D, ambalo hadi sasa linaongozwa na Ufaransa na mechi zake zitahitimishwa leo Jumanne.
Katika mechi za Kundi D leo, Sweden watacheza dhidi ya Ufaransa na wenyeji Ukraine watawavaa England, zote zikichezwa kuanzia saa 3:45 usiku.

No comments:

Post a Comment