Tuesday, June 19, 2012

SOMO KWA WASANII WA FILAMU HILI HAPA

Waigizaji nyota nchini Jacqueline Wolper (kushoto) na Jacob Steven a.k.a JB wakiwa katika pozi la kasha la filamu yao ya "Dereva Taxi". Wasanii hao wanajihusisha pia na uongozaji wa filamu.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na asasi ya Gaba Arts mapema wiki hii wameendesha semina fupi kwa wasanii wa filamu ili kuwajengea weledi katika eneo la uandishi bora wa miswada ya sinema (script writing).

Semina hiyo iliyoendeshwa kupitia programu ya Jukwaa la Sanaa kwenye Ukumbi wa BASATA ilijikita katika maeneo ya namna ya kuendeleza wazo hadi sinema ya kusisimua, namna ya kufikia hisia za watazamaji, ujenzi mzuri wa matukio, kutengeneza wahusika na mfumo wa hadithi, mwanzo, kati na hitimisho.

Akitoa mada kwenye programu hiyo maalum, mkurugenzi wa asasi ya Gaba Arts, James Gayo alisema kuwa muda umefika sasa kwa wasanii wa filamu kusaka maarifa ili kutengeneza sinema zenye visa vipya, zenye weledi na zisizosukumwa na matakwa au maelekezo ya wasambazaji.

"Wenzetu kutoka nje wanatamani sana kupata vitu kutoka Afrika vyenye kuzungumza uhalisia wa maisha ya kwetu, wanataka kuona vitu vipya hivyo, katika uandishi wa muswada wa sinema suala la uhalisia na visa vyenye utofauti ni la msingi sana," alisisitiza Gayo.

Alizidi kueleza kuwa watazamaji wa sinema (filamu) huwa wana kawaida ya kuchoka pale wanapolishwa visa vya aina moja muda wote na akaonya kuwa kama wasanii hawatajikita katika kubuni visa vipya na vyenye kugusa uhalisia wa maisha yao wadau watasusia kununua.

"Ikiwa tutaendelea kutengeneza filamu zisizo na weledi, zenye visa vilevile na zenye kusukumwa na wasambazaji au haja ya kuchuma fedha za haraka tu, watu watatuchoka na baadaye soko litakufa," alionya Gayo.

Gayo ambaye amepitia mafunzo ya utengenezaji filamu katika mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani alitaja sifa za muswada (script) bora kuwa ni pamoja na kubeba wazo linalozalika kwenye jamii, visa vyenye uhalisia na vipya, utengenezaji mzuri wa wahusika na sifa zingine nyingi.

Kwa upande wake msanii wa mashairi Mrisho Mpoto ambaye alikuwa miongoni mwa waliohudhuria semina hiyo alisema kuwa, wasanii wa filamu wanahitaji kusaidiwa kwani kwa sasa soko la filamu limekuwa la kitumwa na lenye kuburuzwa na matakwa ya wasambazaji bila weledi.

Akihitimisha programu hiyo, Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alishauri wasanii wa filamu kujipanga kushirikiana na wasomi wenye weledi katika maeneo yao ili kuzalisha kazi zenye weledi la ubora.

"Tuna wataalam wengi katika Sanaa, wamebanana na mambo mengi lakini ni vema wasanii tukawatumia na kushirikiana nao katika kuboresha kazi zetu," alisisitiza Materego.

No comments:

Post a Comment