Monday, January 28, 2013

MESSI "MTOTO" AIZAMISHA REAL MADRID "B" KWENYE CLASSICO "TOTO"


MAGOLI yake mawili katika mechi ya 'Mini-Clasico' iliyozikutanisha timu za Barcelona "B" na Real Madrid "B", yamemhakikishia yosso Sergio Ezequiel Araujo kuwa mtu anayetajwa sana sasa nchini mwake Argentina.

Kijana huyo alijikuta akipachikwa jina la "Messi B" baada ya kumshuhudia akiwatesa sana mabeki wa Real Madrid "B" katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza Hispania ambayo wenyeji Barca "B" walishinda 3-1 Jumapili.

Timu B ya Real Madrid ajulikanayo kama "Castilla" ilienda mapumziko ikiongoza kwa goli 1-0 lililofungwa Morata, ambaye mara chache pia amekuwa akipewa nafasi katika timu A ya kocha Jose Mourinho.

Lakini kipindi cha pili kiliishuhudia timu ya Barca "B" ikigeuza kibao kupitia magoli mawili kutoka kwa Araujo kabla ya Deulofeu naye kupiga la tatu katika dakika za lala salama na kujihakikishia ushindi wa 3-1 wa 'Mini-Clasico'.

Vyombo vya habari vingi vya Argentina vimeripoti kwamba kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na Sergio Araujo, kimemfanya abebe vichwa vya habari kama 'Ole', na huku wakimuita "Messi B" baada ya kuwanyima kupumzika mabeki wa Madrid katika kiwango ambacho hata Messi mwenyewe atajivunia.

Araujo anapigania kubaki Barcelona ili aweze kucheza na Muargentina mwenzake. Alitua Barcelona Juni 2012 kwa mkopo miaka miwili akitokea Boca Juniors. Akiwa na umri wa miaka 21, mchezaji huyo kijana ana ndoto za kucheza siku moja pamoja na Xavi Hernández na Messi.

Sergio Araujo anatajwa kama moja ya "madini" yaliyoibuliwa na Boca Juniors katika miaka ya karibuni.


Mechi ya El Classico ya wakubwa baina ya Real Madrid na Barcelona ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme itapigwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu na marudiano yatakuwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Nou Camp.

GHANA, MALI ZATINGA ROBO FAINALI AFCON... BAFANA SASA KUKIPIGA NA MALI

Wanachonga sana... ongeeni sasa... Straika wa Ghana, Asamoah Gyan (kushoto) akishangilia na mwenzake baada ya kufunga goli la kuongoza dhidi ya Niger nchini Afrika Kusini leo. Ghana ilishinda 3-0.
Wachezaji wa akiba wa timu ya taifa ya Mali wakishangilia pamoja na kocha wao (mwenye fulana nyeusi wa pili kulia) baada ya kutinga hatua ya robo fainali ya AFCON leo.


GHANA na Mali zimefuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini baada ya Ghana kushinda 3-0 dhidi ya Niger, huku Mali ikitoka sare ya 1-1 na DRC leo.

Katika mechi hizo za mwisho za Kundi B, Ghana ilipata bao lake la kuongoza kupitia kwa straika wake anayecheza soka Umangani, Asamoah Gyan, katika dakika ya 6.

Niger iliamini kwamba imesawazisha goli hilo dakika 2 tu baadaye lakini uamuzi mbovu wa refa ulilikataa bao hilo safi kwa madai kwamba mchezaji wa Niger alimsukuma kipa wa Ghana wakati ukweli ni kwamba alikuwa ni mchezaji wa Ghana aliyemsukuma kipa wake kabla ya mpira kutumbukizwa wavuni.

Nyota wa mchezo huo, Asamoah Gyan, ambaye alikuwa akisemwa vibaya kwamba anacheza chini ya kiwango tangu michuano hii ianze, aliipikia timu yake bao la pili wakati alipokimbia na mpira upand wa kushoto na kumimina krosi kwa yosso gumzo nchini Ghana, Christian Atsu ambaye wenyewe wanamuita "Messi wa Ghana", ambale alifunga goli la pili.

Asamoah tena ambaye wakati akishangilia goli lake la kwanza alifanya ishara ya mkono mdomoni kwamba watu wanaongeza sana juu yake, alikuwa tena chanzo cha goli la tatu la Ghana wakati mpira wake wa kichwa ulipopanguliwa na kipa wa Niger kabla ya John Boye kuutumbukiza wavuni katika kipindi cha pili.

Ghana, moja ya timu zinazopewa nafasi kutwaa ubingwa huo, wamemaliza hatua ya makundi wakiwa vinara kutokana na pointi zao saba, wakifuatiwa na Mali, ambao nao wametinga robo fainali wakiwa na pointi 4 baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa katika muda mmoja.

DRC na Niger zimeaga michuano hiyo. Wacongo wamemaliza wakiwa katika nafasi ya tatu kutokana na kuwa na pointi 3 huku Niger ikiwa mkiani na pointi moja.

Wenyeji Afrika Kusini, Mali, Ghana, Cape Verde na Ivory Coast tayari zimetinga robo fainali.

LULU ABUBUJIKWA MACHOZI YA FURAHA KORTINI... NI BAADA YA JAJI KUMPA MASHARTI AMBAYO AKIYATIMIZA ATAACHIWA KESHO MARA MOJA NA KUACHANA NA MAUGALI YALIYOMNENEPESHA JELA NA KWENDA KULA UBWABWA SAAAAAAAFI WA NYUMBANI KWAOOOOO....!

Elizabeth Michael a.k.a Lulu akitoka mahakamani leo kuelekea kupanda karandinga



Mwanionaje? Nimenenepa eenh! Lulu akitoka mahakamani kwenda kupanda "karandinga" leo




Msanii  wa filamu Elizabeth Michael 'Lulu' amejikuta akibubujikwa machozi ya furaha leo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumpa masharti ya dhamana ambayo akiyatimiza ataachana na maisha ya rumande kuanzia kesho.

Lulu amekuwa rumande kwa takriban mwaka mmoja sasa kuhusiana na shitaka la kumuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake wa filamu, marehemu Steven Kanumba.

“Naomba Mungu anisaidie nipate dhamana na kurudi nyumbani,” Lulu alisema leo huku akilia kwa furaha katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Jaji Zainabu Mruke ndiye aliyetoa masharti hayo  jana baada ya wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuwasilisha maombi ya dhamana kwa hati ya dharura chini ya kifungu cha 148 kidogo cha (1) na cha (2) cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA).
Upande wa Jamhuri uliongozwa na wakili wa serikali, Joseph Maugo na Kishenyi Mutalemwa.

Jaji Mruke alisema kosa linalomkabili mshitakiwa lina dhamana kisheria na kwamba mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kufuata masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 20 kila mmoja.


Pia amemtaka Lulu atimize sharti la kuwasilisha hati zake za kusafiria, kuripoti kila tarehe mosi ya mwezi kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na asitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha msajili huyo.
Akitimiza masharti hayo kesho, Lulu ataachiwa kwa dhamana na kurejea nyumbani kwao.

Katika kesi ya msingi, Lulu anadaiwa kuwa  Aprili 7, 2012, katika eneo la Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, alimuua Kanumba bila kukusudia.

KLABU BADO ZAAMBULIA KIDUCHU MAKATO UWANJA WA TAIFA... YANGA, PRISONS ZAPATA CHINI YA NUSU YA MILIONI 101/- WALIZOINGIZA

Simon Msuva wa Yanga (kushoto) akimtoka beki wa Prisons wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

LICHA serikali kutangaza kwamba imepunguza makato ya Uwanja wa Taifa, mambo bado ni magumu na klabu zinaendelea kugawana chini ya nusu mapato kamili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirikisho la soka nchini TFF, mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom baina ya Yanga na Tanzania Prisons iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa imeingiza mapato ya jumla ya Sh. 101,016,000.

Hata hivyo, timu hizo kila moja imepata Sh. 24,314,752.45 ambazo jumla yake ni 48,629,504.9. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 48.1 ya mapato yote, jambo linalomaanisha kwamba asilimia 51.9 ya mapato imekwenda kwenye makato.

Katika mechi ya kwanza kuchezwa kwenye uwanja huo tangu Serikali itangaze kupunguza makato viwanjani, timu za Simba na African Lyon zilizocheza hapo Januari 27, 2012 na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ziliingiza Sh. 53,756,000. Hiyo ilikuwa ni takriban nusu ya mapato ya mechi ya Yanga dhidi ya Prisons.

Baada ya makato, Simba na Lyon kila moja ilipata mgawo wa Sh. 12,499,752.45, ambazo jumla yake ni Sh.24,999,504. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 46.5 ya mapato yote, jambo linalomaanisha kwamba asilimia 53.6 ya mapato ilimezwa kwenye makato.

Hata hivyo, Serikali ilionya mapema kwamba makato yatakuwa makubwa kama mahudhurio yatakuwa madogo kutokana na gharama za kudumu (fixed cost) kama za tiketi na ikazitaka klabu kuzitangaza vizuri mechi zao ili mahudhurio yawe makubwa.

Mechi ya Yanga dhidi ya Prisons ilihudhuriwa na watazamaji 17,946 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Watazamaji 16,158 kati ya hao walikata tiketi za sh. 5,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ni 98 waliokata tiketi za sh. 20,000.

Makato yalikuwa kama ifuatavyo:
1. Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Sh. 15,409,220.34.

2. Asilimia 15 iliyokwenda kwenye uwanja baada ya kuondoa VAT na gharama za tiketi ni sh. 12,363,433.45.

3. Tiketi Sh. 3,183,890

4. Gharama za mechi sh. 7,413,060.07

5. Kamati ya Ligi Sh. 7,418,060.07

6. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,709,030.03

7.  Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,884,801.14.


Mechi ya Simba dhidi ya Lyon ilihudhuriwa na watazamaji 9,408 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Makato yalikuwa kama ifuatavyo:
1. Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,200,067.80.

2. Asilimia 15 ya uwanja sh. 6,355,806.33.

3. Tiketi sh. 3,183,890

5. Gharama za mechi sh. 3,813,483.80

6. Kamati ya Ligi sh. 3,813,483.80

7. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,906,741.90

8. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,483,021.48.

TASWA YAANZA MCHAKATO TUZO MWAMICHEZO BORA WA MWAKA

Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando (kulia) akizungumza jambo na waandishi wa habari. Kushoto ni Katibu Msaidizi wa TASWA, George "Poji" John

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeanza mchakato wa Tuzo kwa Wanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2012.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando, Kamati ya Utendaji ya TASWA imeamua kama ilivyokuwa mwaka uliopita kwamba suala la mchakato wa kuwapata wanamichezo hao lifanywe na kamati maalum nje ya Kamati ya Utendaji ya TASWA lengo ikiwa ni kupanua wigo na kuwashirikisha wadau wengi zaidi katika jambo hili nyeti.

Jukumu la Kamati ya Utendaji ya TASWA itakuwa ni kuhangaika na mambo ya wadhamini na masuala mengine yahusuyo sherehe hizo ambazo tunataka ziwe za aina yake.

Kutokana na hali hiyo Kamati ya Utendaji ya TASWA iliyokutana wiki iliyopita iliteua kamati maalum ya watu 11 kusimamia mchakato wa kuwapata wanamichezo hao, ambapo kamati hiyo inayotarajia kuanza vikao vyake Jumatano Januari 30, 2013 itakuwa chini ya uenyekiti wa mwanachama wa TASWA, Haji Manara.

"Kamati ya Utendaji imemkabidhi jukumu Manara baada ya kujiridhisha pasi na shaka uzoefu wake katika masuala ya michezo na pia uzoefu wake katika mambo mbalimbali ya kiutawala, hivyo kuwa na imani kwamba ataendesha vizuri mchakato kama walivyofanya watangulizi wake," ilisema taarifa hiyo.

Wajumbe saba wa kamati hiyo wanatoka nje ya Kamati ya Utendaji ya TASWA ambao ni Jane John, Dina Ismail, Jabir Idrissa, Tullo Chambo, Abdallah Mweri na ofisa mmoja ambaye ataombwa kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), wakati wajumbe wanne wanatoka Kamati ya Utendaji ya TASWA ambao ni Grace Hoka, Zena Chande, Alfred Lucas na Amir Mhando.

RONALDO ATUPIA 3, MESSI APIGA 4.... EL CLASSICO ITAKUWA BALAA KESHOKUTWA

Ronaldo akifunga penalti wakati wa mechi yao dhidi ya Getafe jana.
Messi akifunga goli lake la nne na la tano kwa Barcelona dhidi ya Osasuna jana
Mesut Ozil (kulia) wa Real Madrid akishangilia na Cristiano Ronaldo baada ya Ronaldo kufunga goli la pili la Real wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013. Real walishinda 4-0. 

Mesut Ozil (kulia) wa Real Madrid akishangilia na Cristiano Ronaldo baada ya Ronaldo kufunga goli la pili la Real wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013.

Mesut Ozil (kulia) wa Real Madrid akishangilia na Cristiano Ronaldo baada ya Ronaldo kufunga goli la pili la Real wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013. 

Mesut Ozil (kulia) wa Real Madrid akishangilia na Cristiano Ronaldo baada ya Ronaldo kufunga goli la pili la Real wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013.
Cristiano Ronaldo akishangilia baada ya kufunga goli la pili la Real wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013.
Napita humu... Cristiano Ronaldo (Namba 7) wa Real Madrid akichungwa na Juan Valera wa Getafe wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013.
Cristiano Ronaldo (katikati) wa Real Madrid akifunga goli la tatu la Real wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013.
Cristiano Ronaldo (kushoto) wa Real Madrid akipiga mpira mbele ya Alexis Ruano na Juan Valera wa Getafe wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu  mjini Madrid, Hispania Januari 27, 2013.

Messi akimfungisha tela mtu
Lionel Messi (kushoto) wa FC Barcelona akishangilia na Puyol baada ya kufunga goli la pili la timu yake kwa njia ya penalti wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Osasuna kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania Januari 27, 2013. Barca walishinda 5-1

Lionel Messi wa FC Barcelona akifunga goli la pili la timu yake kwa njia ya penalti wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Osasuna kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania Januari 27, 2013. Barca walishinda 5-1

Lionel Messi wa FC Barcelona akimpiga chenga kipa wa Osasuna (aliyekaa chini) na kufunga goli la kuongoza la timu yake wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Osasuna kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania Januari 27, 2013. 

Lionel Messi (kushoto) wa FC Barcelona akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kufunga goli la kuongoza wakati wa mechi yao ya La Liga dhidi ya Osasuna kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania Januari 27, 2013.

Safari hiyo... Lionel Messi akipita katikati ya wachezaji wa Osasuna
Lionel Messi wa FC Barcelona akiondoka na mpira wake baada ya kufunga magoli manne katika mechi dhidi ya Osasuna kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona Hispania Januari 27, 2013.

MECHI ya El Classico ya nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Mfalme baina Real Madrid na Barcelona kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu Jumatano itakuwa ni balaa kufuatia matokeo ya jana timu hizo mbili kubwa Hispania.

Real Madrid waliianza siku ya Jumapili mapema kwa ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Getafe, ambayo kwa mara nyingine tena ilishuhudia Cristiano Ronaldo akiwa katika kiwango chake cha juu kabisa cha kufunga mabao.

Ronaldo alifunga 'hat trick' dhidi ya mahasimu wao wa mji wa Madrid huku magoli yote matatu yakija katika kipindi cha pili. 

Ulikuwa ni ukurasa mwingine wa msimu mzuri kwa Mreno huyo. Na namna ambayo Ronaldo alifunga 'hat trick' hiyo ni lazima pia izingatiwe: Goli moja alifunga kwa mguu wa kushoto, jingine mguu wa kulia na la tatu kwa kichwa. 'Hat trick' iliyokamilika kabisa kama ilikuwapo nyingine kama hiyo.

Magoli yote matatu ya Ronaldo yalikuja ndani ya dakika 10 tu na ilikuwa ni 'hat trick' yake ya 20 maishani na ya 19 akiwa na Real Madrid.

Idadi hiyo inafanya sasa Ronaldo awe amefunga jumla ya magoli 179 katika mechi 176 tangu alipotua misimu mitatu na nusu iliyopita akitokea Manchester United na imemuweka katika Na.6 ya wafungaji vinara wa zama zote klabuni hapo akiwa amemfikia gwiji wa zamani Francisco Gento. Kwa magoli 10 ambayo tayari ameyafunga mwaka huu pekee wa 2013, Ronaldo yuko katika kasi ya kuyafikia magoli ambayo Lionel Messi alifunga mwaka 2012 na kuvunja rekodi.

Lakini walisema kila Ronaldo analolifanya, Messi hulifanya vizuri zaidi na ilikuwa hivyo pia jana.

Messi jana aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya La Liga kufunga katika mechi 11 mfululizo wakati alipofunga magoli manne katika ushindi wa Barcelona wa 5-1 dhidi ya Osasuna kwenye Uwanja wa Nou Camp baadaye jana.

Muargentina huyo sasa amefikisha magoli 33 katika mbio za kuwania tuzo ya 'Pichichi' ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Hispania akifuatiwa na Ronaldo aliyefikisha magoli 22 baada ya 'hat trick' yake dhidi ya Getafe.

Messi sasa amefikisha jumla ya mabao 202 katika La Liga na kuwa mmoja wa wachezaji saba tu waliovuka magoli 200 katika Ligi Kuu ya Hispania.

Osasuna inaonekana kuwa ni timu ambayo Messi "anapenda" kuifunga baada ya kifunga jumla ya magoli 14 katika mechi 13 aliziocheza dhidi yao.

Hii ni mara ya tatu kwa Messi kufunga magoli manne katika mechi moja ya ligi, mara nyingine mbili zikija katika msimu wa kipekee kwake, alipofunga dhidi ya Valencia na Espanyol.