Monday, January 28, 2013

KLABU BADO ZAAMBULIA KIDUCHU MAKATO UWANJA WA TAIFA... YANGA, PRISONS ZAPATA CHINI YA NUSU YA MILIONI 101/- WALIZOINGIZA

Simon Msuva wa Yanga (kushoto) akimtoka beki wa Prisons wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

LICHA serikali kutangaza kwamba imepunguza makato ya Uwanja wa Taifa, mambo bado ni magumu na klabu zinaendelea kugawana chini ya nusu mapato kamili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirikisho la soka nchini TFF, mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom baina ya Yanga na Tanzania Prisons iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa imeingiza mapato ya jumla ya Sh. 101,016,000.

Hata hivyo, timu hizo kila moja imepata Sh. 24,314,752.45 ambazo jumla yake ni 48,629,504.9. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 48.1 ya mapato yote, jambo linalomaanisha kwamba asilimia 51.9 ya mapato imekwenda kwenye makato.

Katika mechi ya kwanza kuchezwa kwenye uwanja huo tangu Serikali itangaze kupunguza makato viwanjani, timu za Simba na African Lyon zilizocheza hapo Januari 27, 2012 na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ziliingiza Sh. 53,756,000. Hiyo ilikuwa ni takriban nusu ya mapato ya mechi ya Yanga dhidi ya Prisons.

Baada ya makato, Simba na Lyon kila moja ilipata mgawo wa Sh. 12,499,752.45, ambazo jumla yake ni Sh.24,999,504. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 46.5 ya mapato yote, jambo linalomaanisha kwamba asilimia 53.6 ya mapato ilimezwa kwenye makato.

Hata hivyo, Serikali ilionya mapema kwamba makato yatakuwa makubwa kama mahudhurio yatakuwa madogo kutokana na gharama za kudumu (fixed cost) kama za tiketi na ikazitaka klabu kuzitangaza vizuri mechi zao ili mahudhurio yawe makubwa.

Mechi ya Yanga dhidi ya Prisons ilihudhuriwa na watazamaji 17,946 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Watazamaji 16,158 kati ya hao walikata tiketi za sh. 5,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ni 98 waliokata tiketi za sh. 20,000.

Makato yalikuwa kama ifuatavyo:
1. Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Sh. 15,409,220.34.

2. Asilimia 15 iliyokwenda kwenye uwanja baada ya kuondoa VAT na gharama za tiketi ni sh. 12,363,433.45.

3. Tiketi Sh. 3,183,890

4. Gharama za mechi sh. 7,413,060.07

5. Kamati ya Ligi Sh. 7,418,060.07

6. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,709,030.03

7.  Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,884,801.14.


Mechi ya Simba dhidi ya Lyon ilihudhuriwa na watazamaji 9,408 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Makato yalikuwa kama ifuatavyo:
1. Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,200,067.80.

2. Asilimia 15 ya uwanja sh. 6,355,806.33.

3. Tiketi sh. 3,183,890

5. Gharama za mechi sh. 3,813,483.80

6. Kamati ya Ligi sh. 3,813,483.80

7. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,906,741.90

8. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,483,021.48.

No comments:

Post a Comment