Monday, January 28, 2013

GHANA, MALI ZATINGA ROBO FAINALI AFCON... BAFANA SASA KUKIPIGA NA MALI

Wanachonga sana... ongeeni sasa... Straika wa Ghana, Asamoah Gyan (kushoto) akishangilia na mwenzake baada ya kufunga goli la kuongoza dhidi ya Niger nchini Afrika Kusini leo. Ghana ilishinda 3-0.
Wachezaji wa akiba wa timu ya taifa ya Mali wakishangilia pamoja na kocha wao (mwenye fulana nyeusi wa pili kulia) baada ya kutinga hatua ya robo fainali ya AFCON leo.


GHANA na Mali zimefuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini baada ya Ghana kushinda 3-0 dhidi ya Niger, huku Mali ikitoka sare ya 1-1 na DRC leo.

Katika mechi hizo za mwisho za Kundi B, Ghana ilipata bao lake la kuongoza kupitia kwa straika wake anayecheza soka Umangani, Asamoah Gyan, katika dakika ya 6.

Niger iliamini kwamba imesawazisha goli hilo dakika 2 tu baadaye lakini uamuzi mbovu wa refa ulilikataa bao hilo safi kwa madai kwamba mchezaji wa Niger alimsukuma kipa wa Ghana wakati ukweli ni kwamba alikuwa ni mchezaji wa Ghana aliyemsukuma kipa wake kabla ya mpira kutumbukizwa wavuni.

Nyota wa mchezo huo, Asamoah Gyan, ambaye alikuwa akisemwa vibaya kwamba anacheza chini ya kiwango tangu michuano hii ianze, aliipikia timu yake bao la pili wakati alipokimbia na mpira upand wa kushoto na kumimina krosi kwa yosso gumzo nchini Ghana, Christian Atsu ambaye wenyewe wanamuita "Messi wa Ghana", ambale alifunga goli la pili.

Asamoah tena ambaye wakati akishangilia goli lake la kwanza alifanya ishara ya mkono mdomoni kwamba watu wanaongeza sana juu yake, alikuwa tena chanzo cha goli la tatu la Ghana wakati mpira wake wa kichwa ulipopanguliwa na kipa wa Niger kabla ya John Boye kuutumbukiza wavuni katika kipindi cha pili.

Ghana, moja ya timu zinazopewa nafasi kutwaa ubingwa huo, wamemaliza hatua ya makundi wakiwa vinara kutokana na pointi zao saba, wakifuatiwa na Mali, ambao nao wametinga robo fainali wakiwa na pointi 4 baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa katika muda mmoja.

DRC na Niger zimeaga michuano hiyo. Wacongo wamemaliza wakiwa katika nafasi ya tatu kutokana na kuwa na pointi 3 huku Niger ikiwa mkiani na pointi moja.

Wenyeji Afrika Kusini, Mali, Ghana, Cape Verde na Ivory Coast tayari zimetinga robo fainali.

No comments:

Post a Comment