Monday, January 28, 2013

MESSI "MTOTO" AIZAMISHA REAL MADRID "B" KWENYE CLASSICO "TOTO"


MAGOLI yake mawili katika mechi ya 'Mini-Clasico' iliyozikutanisha timu za Barcelona "B" na Real Madrid "B", yamemhakikishia yosso Sergio Ezequiel Araujo kuwa mtu anayetajwa sana sasa nchini mwake Argentina.

Kijana huyo alijikuta akipachikwa jina la "Messi B" baada ya kumshuhudia akiwatesa sana mabeki wa Real Madrid "B" katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza Hispania ambayo wenyeji Barca "B" walishinda 3-1 Jumapili.

Timu B ya Real Madrid ajulikanayo kama "Castilla" ilienda mapumziko ikiongoza kwa goli 1-0 lililofungwa Morata, ambaye mara chache pia amekuwa akipewa nafasi katika timu A ya kocha Jose Mourinho.

Lakini kipindi cha pili kiliishuhudia timu ya Barca "B" ikigeuza kibao kupitia magoli mawili kutoka kwa Araujo kabla ya Deulofeu naye kupiga la tatu katika dakika za lala salama na kujihakikishia ushindi wa 3-1 wa 'Mini-Clasico'.

Vyombo vya habari vingi vya Argentina vimeripoti kwamba kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na Sergio Araujo, kimemfanya abebe vichwa vya habari kama 'Ole', na huku wakimuita "Messi B" baada ya kuwanyima kupumzika mabeki wa Madrid katika kiwango ambacho hata Messi mwenyewe atajivunia.

Araujo anapigania kubaki Barcelona ili aweze kucheza na Muargentina mwenzake. Alitua Barcelona Juni 2012 kwa mkopo miaka miwili akitokea Boca Juniors. Akiwa na umri wa miaka 21, mchezaji huyo kijana ana ndoto za kucheza siku moja pamoja na Xavi Hernández na Messi.

Sergio Araujo anatajwa kama moja ya "madini" yaliyoibuliwa na Boca Juniors katika miaka ya karibuni.


Mechi ya El Classico ya wakubwa baina ya Real Madrid na Barcelona ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme itapigwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu na marudiano yatakuwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Nou Camp.

No comments:

Post a Comment