Saturday, August 18, 2012

KIJANA 'ALIYEOKOTWA' NA KULELEWA NA WHITNEY, AMBAYE SASA ANATOKA NA BINTI WA BOBBY BROWN, BOBBI KRISTINA

Bobbi Kristina Brown, binti wa muimbaji marehemu Whitney Houston, akionyesha tattoo yake yenye herufi za kwanza "W H" wakati akipungia alipokuwa akiwasili na boifrendi wake Nick Gordon kwenye uzinduzi wa filamu ya "Sparkle" iliyomshirikisha Jordin Sparks na Whitney Houston (filamu yake ya mwisho kabla hajafariki) mjini Hollywood juzi Agosti 16, 2012. Gordon alichukuliwa na Whitney kwa ajili ya kulelewa nyumbani kwa nyota huyo kutokana na matatizo katika familia yao lakini sasa amekuwa boifrendi wa Bobbi Kristina. Picha: REUTERS
Bobbi Kristina Brown, binti wa muimbaji marehemu Whitney Houston, akipungia wakati alipowasili na boifrendi wake Nick Gordon kwenye uzinduzi wa filamu ya "Sparkle" iliyomshirikisha Jordin Sparks na Whitney Houston (filamu yake ya mwisho kabla hajafariki) mjini Hollywood juzi Agosti 16, 2012. Gordon alichukuliwa na Whitney kwa ajili ya kulelewa nyumbani kwa nyota huyo kutokana na matatizo katika familia yao lakini sasa amekuwa boifrendi wa Bobbi Kristina. Picha: REUTERS

NICK Gordon (22) na Bobbi Kristina (19) wameishi pamoja kwa zaidi ya miaka 10 kama kaka na dada kabla ya kifo cha Whitney Houston.

Kwa mujibu wa TMZ, Bobbi na Nick walilelewa pamoja baada ya Whitney kumchukua akiwa na umri wa miaka 12 wakati baba wa Kick alipohukumiwa kwenda gerezani na mama yake kushindwa kumlea.

Nick alikuwa ni mtoto wa kuasili wa Whitney japo hakumuasili rasmi kisheria, na alikuwa akimchukulia kama mwanae mpaka muimbaji huyo alipofariki akiwa na umri wa miaka 48 kutokana na kuzama kwa bahati mbaya bafuni kulikotokana na matatizo ya moyo yaliyosababishwa na utumiaji wa dawa za kulevya.

Lakini Bobbi Kristina Brown sio tu kwamba alionekana akimbusu kimahaba kaka yake huyo aliyegeuka kuwa mpenziwe, bali pia alituma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter akielezea namna anavyompenda mwanaume huyo, huku kidoleni akuonekana na pete ya uchumba.

'Sababu 1 ya mimi kuwa na tabasamu leo.:) nakupendaa booboo, milele & daima. Ni SISI tu sasa"...@Nickdgordon', Bobbi Kristina aliandika katika ukurasa wake wa Twitter huku aki-post na picha inayomuonyesha akimbusu Nick.

Picha iliyotumwa kwenye Twitter na Bobbi Kristina inayomuonyesha akimbusu kaka yake aliyegeuka mchumba wake

Mvulana huyo alichochea uvumi kuhusu mahusiano yao kwa kutuma ujumbe katika Twitter mwezi Machi mwaka huu, akisema: 'Yea tumezidi kuwa karibu sasa nini kinafuata!!!'

Bobbi Kristina akiwa na kaka yake aliyegeuka mpenzi wake Nick Gordon wakati wa kumbukumbu ya kutimiza miaka 49 ya Whitney Houston

Wapenzi hao wameripotiwa kuendelea kuishi pamoja katika jumba la Whitney tangu alipofariki muimbaji huyo lenye thamani ya dola milioni 1.2 lililopo mjini Atlanta.

Bibi wa Bobbi Kristina, Cissy Houston, amepinga mahusiano hayo.


ONA JINSI VAN PERSIE ALIVYOKUWA AKILA BATA NA FAMILIA YAKE KATIKA VISIWA VYA PITIUSIC KABLA YA KUITOSA ARSENAL NA KUTUA MANCHESTER UNITED

Hee...! Nini tena? Van Persie na mkewe Bouchra wakicheza ndani ya maji
Kama dolphin... mke wa Van Persie akionyesha umahiri wa kupiga mbizi huku mumewe akicheza binti yao, Dina. Bikini hii aliyotupia Bouchra ni aina ya Gucci na bei yake dukani ni paundi  za England 280 (Sh. 700,000). Hapa ilikuwa mwaka juzi.

Chu-chu-chuuu...! Van Persie akicheza majini na binti yake, Dina kwenye visiwa vya Pitiusic, mwaka juzi.

Angalia kuleee....! Van Persie akipata maelekezo kutoka kwa mkewe Bouchra kwenye visiwa vya Pitiusic, mwaka juzi.  

Fumba macho...! Van Persie akimsikiliza mkewe Bouchra huku pembeni wakiwa na mpambe aliyembeba mtoto wao wa kiume, Shaquille.  Hii ilikuwa mwaka juzi

Daddy na mie taka piga mbizi...! Van Persie akicheza majini na mkewe Bouchra na watoto zao Dina na Shaquille, kwenye visiwa vya Pitiusic mwaka juzi. Miwani ya jua aliyovaa Bouchra ni aina ya Tom Ford.



Bouchra... mke wa Van Persie
Mmmmwaaaa... ndio kuna mtoto lakini hayakuhusu!!

Van Persie akiwa na binti yake, Dina katika fukwe za visiwa vya Pitiusic 

Daddy nishushe... Van Persie na binti yake Dina wakiwa kwenye fukwe za visiwa vya Pitiusic, Julai 14, 2012

Taratibu...!

Safari imeanza... Van Persie, mkewe Bouchra na watoto wao Shaquille na Dina wakiwa ndani ya boti ndogo kwenye fukwe za visiwa vya Pitiusic, Julai 14, 2012

Sweetie wakubalie Man U tupate mijihela kuliko ya Arsenal...Van Persie, mkewe Bouchra na watoto zao Dina na Shaquille wakiwa ndani ya boti ndogo wakati wakila bata kwenye visiwa vya Pitiusic, Julai 14, 2012

Lazima niondoke Arsenal...Van Persie akionekana mtulivu wakati yeye na familia yake wakiponda maraha kwenye visiwa vya Pitiusic, Julai 14, 2012

Hapa ni Van Persie, familia yake na wapambe.... ndani ya boti kwenye visiwa vya Pitiusic, Julai 14, 2012

Van Persie na mkewe Bouchra

Twenzetu...! Van Persie na mkewe Bouchra wakiwa tayari kwa mtoko
MANCHESTER, England
 Wakati akiwa akiichezea klabu ya Arsenal, Robin van Persie alikuwa amejenga mazoea ya kuambatana na familia yake kwenda kuponda maraha katika visiwa vya Pitiusic vilivyopo nchini Hispania.

Kila alipokuwa katika mapumziko marefu ya msimu, Van Persie na familia yake hawakuwa wakijiweka nyuma. Walikwenda sehemu mbalimbali zenye utulivu na kujiachia kiasi cha kutosha.

Karibu nusu ya mwezi ulipita, straika huyo aliyekamilisha uhamisho wa kwenda Manchester United akitokea Arsenal kwa ada ya paundi za England milioni 24 (Sh. bilioni 60), aliongozana na mkewe Bouchra na watoto wao Shaquille na Dina kwenda kufaidi maisha katika fukwe za visiwa hivyo vya Pitiusic, wakiambatana pia na swahiba zao kadhaa.

Van Persie na familia yake walionekana ufukweni wakitabasamu muda wote; wakila, kunywa, kuchezea maji na kujianika juani kadri walivyotaka.

Uhamisho wa kwenda Man U mwishoni mwa wiki umemhakikishia 'mafweza' zaidi mifukoni mwake na pengine kuwafanya mkewe na wanawe wafaidi zaidi maisha; kwani imeelezwa kuwa katika mkataba wake wa miaka minne, sasa straika huyo wa kimataifa wa Uholanzi atakuwa akilipwa mshahara mnono wa paundi za England 250,000 kwa wiki, sawa na Sh. milioni 615!

Je, kwanini Van Persie na familia yake wasiendelee kufaidi maisha katika maeneo ghali kama ya visiwa vya Pitiusic?

NI FILAMU YA KISA CHA KANUMBA?

Miss Tanzania No. 3, 2009, Julieth William Lugembe nyota wa filamu mpya ya "Sister Julieth"
Miss Tanzania No. 3, 2009, Julieth William Lugembe (kushoto) na Sylvia Shally Miss TZ No.4 2009 ambao wamecheza filamu mpya ya "Sister Julieth"

MISS Tanzania Na.3 wa mwaka 2009, Julieth William amemshirikisha mrembo mwenzake aliyeshika Na.4 mwaka huo, Sylvia Shally, katika filamu mpya inayokwenda kwa jina la "Sister Julieth".

Filamu hiyo ambayo iko katika hatua ya uhariri inaelezea kisa cha kijana ambaye anatuhumiwa kumuua rafikiye wa kike wakati wakiwa peke yao chumbani na kesi mahakamani inamuelemea kijana huyo.

Sister Julieth, nafasi ambayo inachezwa na Sylvia, anakuja kama mzimu na kumtetea kijana huyo, ambaye anakumbana na upinzani mkali kutoka kwa mawakili wa upande wa mashitaka.

Mrembo huyo aliyegeukia katika uigizaji, alisema hii ni filamu yake ya kwanza kucheza, kama ilivyo kwa Sylvia na kwamba ameitunga yeye mwenyewe.

Baada ya mwandishi kuhoji kama filamu hiyo inahusiana na tukio la marehemu Steven Kanumba aliyefariki wakiwa peke yao chumbani na muigizaji Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, aling'aka: "Aaah hapana. Hata kidogo. Ni kisa tofauti kabisa. Ni kisa kinachouhusisha mzimu unaokuja duniani kutoa ushahidi.

"Ni kati ya filamu za hisia kali. Iko katika hatua ya uhariri na wakati wowote itatoka."

Alisema katika filamu hiyo amewashirikisha pia wasanii wengine maarufu akiwamo Dude.

Katika shindano la Miss Tanzania 2009 ambalo Julieth alishika Na.3, Miriam Gerald aliibuka mshindi wa kwanza, Beatrice Lukindo alikuwa wa pili wakati nafasi ya nne ilishikwa na Sylvia na Sia Ndaskoi alikamilisha Top 5.

THEO WALCOTT AIPASUA KICHWA ARSENAL... ALETA POZI KUSAINI MKATABA MPYA, NI KAMA ALIVYOFANYA ROBIN VAN PERSIE KABLA YA KUTIMKIA MAN U

Theo Walcott

Theo Walcott wa Arsenal akimtoka beki mmojawapo wa Kitchee FC wakati wa mechi yao ya kirafiki kujiandaa na msimu mpya kwenye Uwanja wa Hong Kong, Julai 29, 2012.
LONDON, England
KLABU ya Arsenal bado inahaha katika mazungumzo yanayoendelea hadi leo ya kujaribu kumshawishi straika Theo Walcott asaini mkataba mpya utakaofuta uvumi wa kuhama kwake.

Imeelezwa kuwa straika huyo wa timu ya taifa ya England anauchanganya uongozi wa Arsenal kwani hadi sasa bado hajakubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumuikia timu hiyo kaskazini mwa jiji la London.

Gazeti la The Sun limesema kwamba hofu imetawala miongoni mwa viongozi wa Arsenal kuwa straika huyo atakuwa mchezaji mwingine mwenye jina kubwa kuiacha timu hiyo katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi baada ya nahodha wao wa zamani, Robin van Persie kuhamia Manchester United.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri kuwepo kwa hofu ya kumpoteza Walcott na kusema: “Bado tunajaribu kuzungumza naye ili kuongeza mkataba wake.”

Kabla ya kuiacha Arsenal na jana kusaini mkataba wa miaka minne kuichezea Man U, Van Persie pia alikataa kusaini mkataba mpya wa kumuongezea kubaki katika klabu yake ya zamani.

WENGER: TUWE WAKWELI JAMANI... ARSENAL TUSINGEWEZA KUSHINDANA NA MAN U KWA KUMLIPA VAN PERSIE MSHAHARA WA MILIONI 615/- KWA WIKI....!

Kijana hapa utakuwa bilionea kwa mihela tunayokupa kila wiki na pia kabati lako litajaa makombe kwa sababu sisi ni watu wa kazi... ila lazima ukaze msuli, ukilegea nakuchenjia kama Berbatov! Kocha Alex Ferguson akimpa maelekezo straika wake mpya, Robin van Persie wakati wakiwa mazoezini jijini Manchester jana. 
Huyu Ferguson haniwezi kwa lolote.... ila kinachombeba ni kumwaga mapesa tu! Kocha Arsene Wenger wa Arsenal (kushoto) akiwa na Alex Ferguson. 
Asante sana kwa kuniachia hili jembe Van Persie... Ferguson (kulia) akiwa na Wenger
LONDON, England
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema leo kwamba klabu yao haikuweza kushindana na mkataba wa Manchester United uliombatana na mshahara mnono kwa straika na nahodha wao wa zamani, Robin van Persie.

Amesema: “Sisi tunaishi kwa kuzingatia hali halisi kiuchumi lakini klabu nyingine hazizingatii jambo hilo. Kuna baadhi ya vitu hatuwezi kamwe kuvifanya.

“Mnataka kulipa kiasi gani? 250k (Sh. milioni 615)?, 300k (Sh. milioni 740)? Mnasema sisi hatuishi kulingana na uhalisia uliopo duniani halafu bado mnatuhoji tunaposema kwamba hatutalipa mshahara wa 250k (Sh. milioni 615) kwa wiki.”

Wenger pia alifichua kwamba Arsenal hawatawekeza zaidi fedha walizopata kwa kumuuza Van Persie paundi za England milioni 22 (Sh. bilioni 55) kwani tayari wameshawasajili mastraika Lukas Podolski, Olivier Giroud na kiungo Santi Cazorla.

Arsenal walimuuza Van Persie kwa paundi za England milioni 24 (Sh. bilioni 60), huku paundi milioni 22 kati ya fedha hizo zikilipwa taslim na nyingine zikitarajiwa kutolewa ikiwa straika huyo ataonyesha kiwango kizuri na kuipa mafanikio klabu yake mpya ya Man U.     

JINI KABULA: NINA UJAUZITO WA BUSHOKE

Miriam Jolwa a.k.a Jini Kabula
Jini Kabula

MSANII wa filamu nchini, Miriam Jolwa maarufu kama 'Jini Kabula' amesema anajiandaa kupata mtoto wake wa pili kwani tayari ana ujauzito wa msanii Bushoke.

"Nimempenda anajua mambo ndio maana nimebeba ujauzito wake," alisema kimwana huyo wakati akihojiwa na mtangazaji Sam Misago a.k.a Presenters' Prezident katika kipindi cha Friday Night Live cha EATV jana usiku. 

"Napenda watoto, ukiwazaa unakuwa mtamu zaidi... ukitoa mimba unakomaa. Nitawazaa wote hata kama nina mayai 100, nitawazaa wote.

"Mimi siwezi kutoa mimba. Kama mama yangu angenitoa nisingekuwepo leo hii."

Sam Misago akamuuliza: "Kama unasema Bushoke anajua mambo, Mr Chuzi je?"

Kabula akajibu: "Siwezi kumkana. Ni baba wa mtoto wangu wa kwanza. Naye anajua mambo ndio maana nikamzalia."

Jini  Kabula (kushoto) akiwa na Mr Nice.

Sam akampiga swali jingine: "Na Mr Nice je, mbona hukumzalia?"

Kabula akajibu: "Ah! Mir Nice sikumpenda. We unadhani unamzalia kila mtu? Wengine hawajui matunzo ya watoto wao."

Alipoulizwa hahofii kukimbiwa na mwanaume aliyembebea ujauzito, Kabula alisema hahofii jambo hilo kwa sababu yeye ana kipato cha kutosha kumfanya mwanae aishi maisha mazuri.

Alipoulizwa ni nani kati yake na Bushoke aliyehitaji mtoto huyo, Kabula alisema: "Bushoke ndiye aliyeng'ang'ania kuzaa na mimi, alitaka hii mbegu, huoni mi' ni mtoto mkali?"

Jini Kabula alifika katika studio ya EATV kwa ajili ya kupromoti video ya wimbo wa kundi lao jipya la muziki la vimwana watatu la Scorpion Queens. Wengine katika kundi hilo mshiriki wa zamani wa Miss Tanzania, Rashida Wanjara na Isabella Mpanda.

"Hatujavamia fani ya muziki, mimi nilipenda muziki tangu sijawaza kwamba nitakuwa kuwa nyota wa Bongo Movies," alisema Kabula.

Kuhusu sababu ya kujiita Scorpion, Kabula alisema: "Sisi tuna sifa za ng'e, unaweza ukaishi naye hata ndani ya nyumba kama hutamchokoza, lakini ukimkanyaga utakiona cha moto."

Aidha, Kabula alisema video ya wimbo wao mpya imewagharimu Sh. milioni 9.1 na kwamba huo ni mwanzo tu kwani wanajipanga kutoa wimbo wao wa pili kabla ya mwisho wa mwaka huu.


Kwenye kipindi hicho cha Friday Night Live, alikuwapo pia muigizaji Sinta, ambaye alikutana na boifrendi wake wa zamani Juma Nature, ambaye amecheza naye filamu itakayotoka hivi karibuni ya 'Sitaki Demu', wimbo wa Nature ambao aliutunga kumshambulia Sinta wakati walipoachana huku akimpenda mno.