Friday, July 19, 2013

MOYES ATARAJIA HABARI NJEMA KWA FABREGASKOCHA wa Manchester United, David Moyes amesema anatarajia "habari njema" kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa Barcelona, Cesc Fabregas.

Iliripotiwa Jumatatu kwamba mabingwa wa Ligi kuu ya England, Man United walituma ofa ya paundi milioni 25.9 kwa ajili ya kutaka kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania, baada ya Thiago Alcantara kuchagua kuungana na kocha wake wa zamani Pep Guardiola kwenye klabu ya Bayern Munich kuliko kutua Old Trafford.

Licha ya kocha wa Barcelona, Tito Vilanova kusisitiza kwamba Fabregas anataka kubaki Camp Nou, Moyes amebainisha kwamba Man United wanakomalia kuhakikisha wanamsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 26.

"Siwezi kukwambia wapi hasa tumefikia kuhusu Fabregas. Ninawasiliana na makamu mwenyekiti (Ed Woodward), ambaye ndiye anayeshughulikia jambo hilo hivi sasa.

"Natumai kupata taarifa zaidi kesho. Kwa Uingereza sasa hivi ni usiku hivyo taarifa zaidi nitazipata kesho," alisema Moyes ambaye yuko pamoja na timu yake ziarani Asia.
Moyes pia alisisitiza kwamba Wayne Rooney, ambaye alitumiwa ofa kutoka Chelsea wiki hii, HAUZWI.

"Msimamo wa klabu kuhusu Wayne Rooney haujabadilika."

No comments:

Post a Comment