Friday, July 12, 2013

MOURINHO ATHIBITISHA KUVUTIWA NA ROONEY


KOCHA wa Chelsea, Jose Mourinho amebainisha jinsi anavyomkubali straika wa Manchester United, Wayne Rooney.

Ilibainishwa mapema Mei kwamba Chelsea, pamoja na Arsenal, walikuwa wakimhitaji straika huyo wa zamani wa Everton, ambaye Sir Alex Ferguson alianika kuwa ameomba kuondoka klabuni hapo mwisho wa msimu.

Baada ya kumkosa kumsajili Falcao, ambaye alitua Monaco katika uhamisho wa pesa nyingi mapema katika kipindi hiki cha usajili, Mourinho yuko sokoni akisaka straika wa "maana" wa kuongoza safu yake ya ushambuliaji msimu ujao.

Na akizungumza mjini Bangkok mwanzoni ziara ya klabu hiyo ya kujiandaa na msimu mpya barani Asia, kocha huyo wa Chelsea amesisitiza kwamba yeye ni shabiki mkubwa wa Rooney.

Alisema: "Rooney ni mchezaji ninayemkubali sana siwezi kusema zaidi ya hapo. Kwa kuwa ana kasi na anacheza soka la moja kwa moja, napenda hivyo, lakini ni mchezaji wa Manchester United."

David Moyes na kikosi cha Manchester United pia wako Thailand kujiandaa na msimu ingawa Rooney amelazimika kurudi England baada ya kupata maumivu ya misuli ya nyuma ya paja ambayo yanatarajiwa kumweka nje ya uwanja kwa mwezi mzima.

Hatma ya straika huyo mwenye umri wa miaka 27 klabuni Old Trafford bado haijafahamika, na licha ya kukataa kuthibitisha kama Rooney ameahidi kubaki klabuni hapo, Moyes alishasisitiza kuwa mshambuliaji huyo hataruhusiwa kuondoka.

--------------------

No comments:

Post a Comment