Friday, July 12, 2013

ALIYEIUA TAIFA STARS HATIMAYE ATUA SWANSEA

Wilfried Bony
Msuli mnene... Mshambuliaji Wilfried Bony (katikati) akiwapa "shughuli" wachezaji wa timu ya ADO 20 wakati wa mechi ya KNVB Dutch Cup kwenye Uwanja wa Gelredome mjini Arnhem, Uholanzi.Desemba 19, 2012.

Wilfried Bony

MSHAMBULIAJI wa Ivory Coast, Wilfried Bony, ambaye alifunga goli la nne wakati miamba hao wa Afrika walipoifunga Taifa Stars magoli 4-2 katika mechi iliyozima ndoto za Tanzania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2013 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, amejiunga na Swansea kwa ada ya uhamisho iliyoweka rekodi klabuni hapo ya paundi milioni 12.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alitwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uholanzi msimu uliopita akifunga magoli 31 katika mechi 30 akiwa na klabu ya Vitesse, amevunja rekodi ya uhamisho kwa klabu hiyo ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Pablo Hernandez aliyesajiliwa kwa paundi milioni 5.55 msimu uliopita.

"Uhamisho huu ulikuwa ukizunguzwa kwa muda mrefu, hivyo nina furaha kwamba hatimaye umekamilika," Bony aliiambia tovuti rasmi ya klabu hiyo.

"Hivi sasa ni muhimu kuweka akili katika changamoto zilizopo mbele kwa sababu ninatumai nitawapa furaha mashabiki wa Swansea."

Magoli ya nyota huyo mwenye misuli yaliisaidia Vitesse kumaliza katika nafasi ya nne ya Ligi kuu ya Uholanzi msimu uliopita, jambo linalomaanisha kwamba wanaweza kukumbana na Swansea katika hatua ya mchujo ya Ligi ya Europa.

Bony alibainisha kwamba usongo wa kucheza michuano ya Ulaya ndiyo uliochangia katika maamuzi yake ya kujiunga na kikosi hicho cha kocha Michael Laudrup, akiwa alishawahi kumaliza mfungaji bora wa Ligi ya Europa kwa kupachika mabao tisa wakati akiichezea Sparta Prague katika msimu wa 2010-11.

“Ligi ya Europa ndiyo lengo langu ya kwanza," alisema. “napenda kucheza michuano ya Ulaya; nimeizoea."

"Najiandaa kujiunga na kambi ya mazoezi hapa Uholanzi kama mchezaji wa Swansea na kujenga mawasiliano mazuri na timu na benchi la ufundi haraka iwezekanavyo."

Bony amekuwa mchezaji wa sita kusajiliwa na mabingwa hao wa Kombe la Ligi (Capital One Cup), ambao wako 'bize' sokoni baada ya kuwanasa Jonjo Shelvey, Jordi Amat, Jose Canas na Alejandro Pozuelo, wakati pia uhamisho wa mkopo wa Jonathan de Guzman pia ukifanywa kuwa mkataba wa kudumu.

No comments:

Post a Comment