Erasto Nyoni (kulia) akimiliki mpira huku akichungwa na Frank Domayo (wa pili kulia), Kelvin Yondani na Mrisho Ngassa (kushoto) wakati wa mazoezi ya Taifa Stars |
Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) imewasili Dar es Salaam leo tayari kwa mechi ya kwanza ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati yake na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
The Cranes inayofundishwa na Mserbia Sredojvic Micho imetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 5.30 asubuhi kwa ndege ya Air Uganda, na imefikia hoteli ya Sapphire.
Timu hiyo leo (Julai 11 mwaka huu) itafanya mazoezi saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Karume, wakati kesho saa 9 alasiri itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, kabla ya kuipisha Taifa Stars itakayoanza mazoezi saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen, na kudhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, leo kwa mujibu wa program yake haitakuwa na mazoezi.
Wachezaji wanaounda The Cranes ni makipa Ismail Watenga, Kimera Ali na Muwonge Hamza. Mabeki ni Guma Dennis, Kasaaga Richard, Kawooya Fahad, Kisalita Ayub, Magombe Hakim, Malinga Richard, Mukisa Yusuf, Savio Kabugo na Wadada Nicholas.
Viungo ni Ali Feni, Birungi Michael, Frank Kalanda, Hassan Wasswa, Kyeyune Said, Majwega Brian, Mpande Joseph, Muganga Ronald, Ntege Ivan, Owen Kasule, wakati washambuliaji ni Edema Patrick, Herman Wasswa na Tonny Odur.
No comments:
Post a Comment