Sunday, June 16, 2013

NEYMAR AFUNGA LA UFUNGUZI MABARA BRAZILI IKIUA 3-0

Neymar akishangilia goli lake alilofunga dhidi ya Japan katika mechi ya ufunguzi wa Kombe la Mabara nchini Brazil jana usiku
Kitu "kunyavu"... Kipa wa Japan,Kawashima akiruka bila ya mafanikio kujaribu kuokoa shuti la Neymar lisitinge wavuni
Golden Boy kipenzi cha walimbwende akishangilia goli lake jana usiku

NEYMAR alifunga goli la kwanza la michuano ya Kombe la Mabara usiku wa kuamkia leo wakati wenyeji Brazil walipoanza na ushindi wa 3-0 dhidi ya Japan katika mechi ya ufunguzi.

Goli kali la Neymar katika dakika ya tatu liliwajengea Brazil kujiamini kabla ya Paulinho kuongeza la pili katika dakika ya tatu ya kipindi cha pili. Mtokea benchi Jo, ambaye aliwahi kuichezea Manchester City, alikamilisha ushindi katika dakika ya tatu ya majeruhi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada yamechi hiyo, Neymar (21) alielezea furaha yake kwa kiwango chake binafsi na kwamba anaona timu sasa inazidi kukomaa.

"Nina furaha nimefunga," alisema Neymar ambaye alifunga goli lake la kwanza katika mechi 10 zilizopita za klabu na taifa. "Daima huwa nasema nataka kuboresha kiwango changu, na nataka timu icheze kama kikundi."

Neymar, ambaye sasa ameifungia timu yake ya Brazil magoli 21 katika mechi 35 alizocheza, alipumzishwa kuelekea mwishoni mwa mechi baada ya kupata maumivu kidogo na mashabiki uwanja mzima wakasimama kumpigia makofi kwa heshima lakini alisisitiza kwamba hakuna cha kuhofia.

"Niko fiti na niko tayari kwa mechi ijayo, na nyingine zote," alisema. "Daima nafikiria kuhusu familia yangu na napata mizuka ya kucheza."

Mashabiki 67,000 waliohudhuria walishuhudia polisi wakilipua mabamu ya machozi kwa waandamanaji wenye hasira wakipinga gharama kubwa zilizotumika kujenga viwanja kwa ajili ya michuano hiyo na ya fainali za Kombe la Dunia mwakani badala ya kutumika kutatua matatizo ya kijamii.

Kikosi cha kocha Luiz Felipe Scolari kinafukuzia ubingwa wa tatu mfululizo wa Kombe la Mabara baada ya kuutwaa katika michuano iliyopita ya 2005 na 2009.

Brazil watatinga nusu fainali kama watashinda dhidi ya Mexico Jumatano.
----------------

No comments:

Post a Comment