Friday, May 10, 2013

VODA KUIJAZA YANGA MIL. 70, KIPRE TCHETCHE ZAKE MIL.5/-

Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalim (katikati) akizungumza katika mkutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu zawadi mbalimbali za Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kushoto ni Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura na kulia ni Meneja Mahusiano wa Vodacom, Matina Nkurlu.
Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalim (katikati) akizungumza katika mkutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu zawadi mbalimbali za Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kushoto ni Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura na kulia ni Meneja Mahusiano wa Vodacom, Matina Nkurlu.

WADHAMINI wa Ligi Kuu ya soka Tanzana Bara, Kampuni ya Vodacom imetangaza kutumia kiasi cha Sh. milioni 200 kwa ajili ya kutoa zawadi ya fedha taslimu katika ligi inayomalizika Mei 18 ambapo sasa mabingwa wa msimu huu, Yanga, watajinyakulia Sh. milioni 70, huku zawadi ya mfungaji bora inayotarajiwa kutua kwa Kipre Tcheche wa Azam ni Sh. milioni 5.

Mbali ya bingwa, Vodacom pia itatoa fedha kwa timu inayomaliza nafasi ya pili, ya tatu na  ya nne katika msimamo wa ligi ambazo ni Sh. milioni 35, Sh. milioni 25 na Sh. milioni 20 zote zikiwa na ongezeko ikilinganishwa na zawadi za fedha zilizotolewa katika msimu wa 2012 / 2013.

Zawadi hizo zimetangazwa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kampuni hiyo kupitia Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalim, ikiwa ni pamoja na kuainisha zawadi za washindi wa mchezaji mmoja mmoja pamoja na timu iliyoonyesha nidhamu kwa msimu huu.

"Mwaka huu tutatumia kiasi cha Sh. milioni 200 kwa ajili ya zawadi za fedha taslimu kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom huku bingwa akinyakua kitita cha Sh. milioni 70 ikilinganishwa na Sh. milioni 50 za msimu uliopita," alisema Mwalim.

Mwalimu amesema lengo la kuongeza zawadi ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya wadhamini wa ligi na wadau wengine wa soka na kwa pamoja kuwa na dhamira ya dhati katika kuendeleza soka nchini.

"Kila mmoja ni shahidi wa namna ambavyo soka letu limekua na namna ambavyo tunakabiliana hatua kwa hatua na changamoto zinazohusiana na ligi. Ni matumaini yetu kwamba tunapiga hatua na tuna matumaini ya kufikia kiwango cha juu zaidi cha maendeleo ya soka nchini yanaonekana," aliongeza Mwalim.

"Kwetu sisi kama wadhamini tutajitahidi kadri inavyowezekana kuhakiksha tunaleta mabadiliko katika soka la Tanzania, tunaangalia mpira wa miguu nchini kwa upana zaidi kama mchezo unaopendwa, unaotuleta pamoja kama taifa na kuitangaza nchi yetu. Falsafa yetu hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa utulivu na ushirikiano mzuri miongoni mwa wadau na hivyo kutuletea mafanikio," alisema Mwalim.

Zawadi nyingine zilizotangazwa ni pamoja na zawadi ya Mchezaji Bora wa Mwaka, Kipa Bora na Mfugaji Bora, ambao kila mmoja  atajinyakulia Sh. milioni 5.

Mwamuzi Bora na Kocha Bora kila mmoja atajipatia Sh. milioni 7.5 wakati timu yenye nidhamu itazawadiwa fedha taslimu ya Sh. milioni 15.

"Tumekuwa na msimu mzuri uliojaa ushindani na hamasa, tunatarajia timu zitajipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao na hivyo kuendelea kuipa ubora ligi yetu," alisema Mwalim huku akiwashukuru wadau wa mpira wa miguu nchini ikiwamo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi,  Kamati ya Ligi Kuu, Chama cha Waamuzi (FRAT), klabu shiriki, wachezaji na kipekee mashabiki.

Alisema bila ya ushirikiano wa wadau hao na wengine ikiwamo Serikali, ligi kuu ya Vodacom isingeweza kufikia maendeleo iliyoyafikia katika msimu unaomalizika ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na mpira wa uwanjani na si vinginevyo
.

No comments:

Post a Comment