Friday, April 26, 2013

YANGA YATWAA UBINGWA WA 24 LIGI KUU BARA...

Wachezaji wa Yanga wakishangilia katika moja ya mechi zao za Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

YANGA imetwaa bila ya kutoka jasho leo ubingwa wa 24 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya wapinzani wao katika mbio hizo, Azam FC kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga jioni ya leo.

Matokeo ya sare kwenye Uwanja wa Mkwakwani leo yamemaanisha kwamba Azam imefikisha pointi 48, nane nyuma ya Yanga, hivyo hawataweza kuwafikia vinara hata kama watashinda mechi zao mbili zilizobaki.

Yanga sasa itacheze mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Coastal Union na Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha ratiba tu na wanatarajiwa kukabidhiwa mwali wao katika mechi ya mwisho dhidi ya mahasimu wao Simba.

Simba ambayo imekuwa na msimu mbaya mwaka huu ikikabiliwa migogoro ya kiuongozi iko katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 36, nne nyuma ya Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu. Hata hivyo, Kagera Sugar imecheza mechi 23 na Simba imecheza 22.

Azam wanaweza kumaliza katika nafasi ya pili kwa mwaka wa pili mfululizo kama watapata pointi mbili (na kufikisha pointi 50) katika mechi zao mbili zilizosalia, baada ya mwaka jana pia kumaliza wa pili nyuma ya waliokuwa mabingwa Simba, na Yanga ilimaliza ikiwa ya tatu. Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu sasa, inaweza kufikisha pointi 49 kama itashinda mechi zake zote zilizobaki wakati Simba ikishinda zote nne zilizosalia itafikisha pointi 48.


Kwa kutwaa ubingwa wa 24, Yanga wameendelea kuboresha rekodi yao hiyo ya kuubeba mara nyingi zaidi wakifuatiwa na mahasimu wao wa jadi Simba walioutwaa mara 16. Yanga imelibeba taji hilo mara 6 katika miaka 9 iliyopita.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara mwaka huu imeshirikisha timu 14 za Yanga, Azam FC, Kagera Sugar, Simba SC, Coastal Union, Mtibwa Sugar, African Lyon FC, JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, Toto African, Polisi Morogoro, Mgambo Shooting, Prison FC na JKT Oljoro.

Ligi hiyo ya juu zaidi Tanzania Bara ilianzishwa mwaka 1965 chini ya jina la Ligi ya Taifa na baadaye ikabadilishwa jina na kuitwa Ligi Daraja la Kwanza. Jina hilo lilibadilishwa na kuitwa Ligi Kuu mwaka 1997 wakati ilipopata udhamini wa kwanza wa ligi kutoka kwa kampuni ya Tanzania Breweries LTD (TBL), kupitia bia yao ya Safari Larger.

Mkataba wa Safari Larger ulivunjwa mwaka 2001 baada ya kutokea kutoelewana baina ya chama cha soka, wakati huo kikiitwa FAT na TBL. Kisha mwaka 2002 Vodacom waliingia kuidhamini.

Yanga imeutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara 24 wakifuatiwa na mahasimu wao Simba walioutwaa mara 16.

Klabu nyingine ambazo zimewahi kutwaa taji hilo ni Cosmopolitan (1967), Mseto SC, (1975) Pan African (1982), Mtibwa Sugar (1999 na 2000) Tukuyu Stars (1986) na Coastal Union (1988).

Orodha kamili ya mabingwa wa taji hilo tangu ligi ilipoanzishwa mwaka 1965:

    1965 Sunderland (Sasa Simba SC)
    1966 Sunderland
    1967 Cosmopolitan
    1968 Yanga
    1969 Yanga
    1970 Yanga
    1971 Yanga
    1972 Yanga
    1973 Simba SC
    1974 Yanga
    1975 Mseto SC
    1976 Simba SC
    1977 Simba SC
    1978 Simba SC
    1979 Simba SC
    1980 Simba SC
    1981 Yanga
    1982 Pan Africans
    1983 Yanga
    1984 Simba SC
    1985 Yanga
    1986 Tukuyu Stars
    1987 Yanga
    1988 Coastal Union
    1989 Yanga
    1990 Simba SC
    1991 Yanga
    1992 Yanga
    1993 Yanga
    1994 Simba SC
    1995 Simba SC
    1996 Yanga
    1997 Yanga
    1998 Yanga
    1999 Mtibwa Sugar
    2000 Mtibwa Sugar
    2001 Simba SC
    2002 Yanga
    2003 Simba SC
    2004 Simba SC
    2005 Yanga
    2006 Yanga
    2007 Simba SC
    2007/08 Yanga
    2008/09 Yanga
    2009/2010 Simba SC
    2010/2011 Yanga
    2011/2012 Simba SC
    2012/2013 Yanga

No comments:

Post a Comment