Friday, April 26, 2013

NILIJUA YANGA BINGWA, ASEMA KOCHA AZAM

Kocha wa Azam, Stewart Hall (kulia)

KOCHA wa Azam, Stewart Hall amesema alifahamu kwamba Yanga lazima watakuwa mabingwa msimu huu ndiyo maana akawapumzisha nyota wake watano katika mechi yao waliyolazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union leo jioni.

Muingereza huyo alisema baada ya mechi ya leo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwamba ilikuwa ni vigumu kwa Yanga kutotwaa ubingwa kutokana na timu nzuri waliyonayo.

"Nilisema awali ili sisi tuwe mabingwa ilikuwa ni lazima Yanga wafungwe mechi zao tatu za mwisho. Na kwa timu nzuri waliyonayo na kocha mzuri waliyenaye nilijua hawawezi kufungwa mechi tatu. Ndiyo maana leo nikawaacha nje wachezaji watano. Nilimuacha nje Kipre Tchetche, Sure Boy, Khamis Mcha hakucheza kwakuwa ni mgonjwa... niliona ni vyema wapumzike kwa ajili ya mechi ya (FAR Rabat) Morocco," alisema Hall. 


Kocha huyo aliwaanzisha nyota wake wawili, Aggrey Morris na Erasto Nyoni, kwa mara ya kwanza tangu waliposimamishwa kwa tuhuma za kupokea rushwa katika mechi dhidi ya Simba. Nyota wengine wawili waliosimamishwa kwa tuhuma hizo ni kipa Deogratius Munishi 'Dida' na Said Morad. TAKUKURU iliwasafisha nyota hao wote. Nahodha wa zamani, Morris alilipa fadhila za kuanzishwa kwa kufunga goli la kuongoza la Azam kwa njia ya penalti kabla ya Daniel Lyanga wa Coastal kuisawazishia timu yake akitokea benchi. 

Kati ya mechi tatu, ambazo Hall aliona ni lazima Yanga wapoteze ili wao wawe mabingwa ni dhidi ya JKT Ruvu, ambayo Yanga ilishinda 3-0 wiki iliyopita na sasa mabingwa hao wamebakiza mechi mbili dhidi ya Coastal na Simba.

Hall, ambaye mwaka jana aliiwezesha Azam kumaliza katika nafasi ya pili ya michuano ya klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) walilokuwa wakishiriki kwa mara ya kwanza ambapo walilala 2-0 katika fainali dhidi ya Yanga, aliwasifu Coastal Union kwamba walicheza vizuri sana leo.

No comments:

Post a Comment