Monday, April 1, 2013

NYOTA WA ZAMANI STARS AFARIKI TANGA


SHIRIKISHO la soka nchini (TFF) limesema limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Coastal Union, TPC na Taifa Stars, Behewa Ali Sembwana (72) kilichotokea juzi usiku mkoani Tanga.

Taarifa iliyotolewa leo na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, ilisema msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Sembwana akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake utakumbukwa daima.

Sembwana aliyekuwa akicheza wingi ya kulia alidumu katika Taifa Stars kwa miaka kumi, kama ilivyokuwa kwa kombaini ya Mkoa wa Tanga (Tanga Stars) aliyoiwakilisha katika michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup).

"TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Sembwana, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Maziko yalitarajiwa kufanyika leo kijijini kwake Lusanga, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana mahali pema peponi. Amina

No comments:

Post a Comment