Monday, April 1, 2013

MCHEZAJI POLISI TABORA AFA AJALI YA PIKIPIKI


SHIRIKISHO la soka nchini (TFF) limeelezea masikitiko yake kufuatia kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ya Polisi Tabora, Regan Mbuta kilichotokea jana usiku kwa ajali ya pikipiki mjini Tabora.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA), Yusuf Kitumbo, marehemu alisafirishwa leo kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema leo katika taarifa yake kuwa msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mbuta alikuwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao lake la mwisho aliloifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu huu dhidi ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, hivyo mchango wake utakumbukwa daima.

"TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta, TAREFA na klabu ya Polisi Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito," ilisema taarifa hiyo.
Mungu aiweke roho ya marehemu Mbuta mahali pema peponi. Amina

No comments:

Post a Comment