Friday, April 26, 2013

DIEGO LOPEZ AMFUNIKA RONALDO KIWANGO DHIDI YA BORUSSIA

Chati ya utafiti uliofanywa kwa mashabiki wa Real Madrid nchini Hispania kupima viwango vyao katika mechi waliyolala 4-1 dhidi ya Borussia Dortmund

Kipa wa Real Madrid, Diego Lopez

KWA mujibu wa utafiti uliofanywa nchini Hispania, Diego Lopez ndiye mchezaji wa Real Madrid aliyeepuka lawama katika kikosi kilichosambaratishwa na Borussia Dortmund kwa kipigo cha 4-1.
Mashabiki wamempa kipa huyo alama  6.6. Waliomfuatia ni Varane na Ronaldo, ambaye amepata alama 4.3. Pepe ndiye aliyepata alama ndogo zaidi, akiambulia alama 1.4.

Ingawa Diego Lopez alitunguliwa magoli manne na mshambuliaji raia wa Poland, Robert Lewandowski, aliificha aibu zaidi Real kwa kuokoa mashuti mengine ya hatari, likiwamo la Reus wakati matokeo yakiwa 0-0. Katika dakika za mwisho wa mechi aliokoa kwa ncha ya vidole shuti kali la Gundogan ambalo lilidhaniwa lingetinga wavuni.

Haukuwa usiku mzuri kwa Pepe na hakuweza kumdhibiti Lewandowski, ambaye alikuwa nyota wa siku asiye na ubishi akithibitisha uwezo wake wa kutupia kambani magoli. Hicho ndicho kilichomfanya beki huyo Mreno kupata alama ndogo zaidi.

Mashabiki hawakumuacha Mourinho pia. Kocha huyo Mreno alipewa alama kiduchu, 2.2 tu kwa kutumia takriban dakika 90 zote za mechi hiyo akiwa amepigwa ganzi kwenye benchi la ufundi ilhali kocha wa mwenzake wa Borussia Jurgen Klopp alikuwa muda wote amesimama pembeni ya uwanja akitoa maelekezo kwa wachezaji nini kifanyike.

Wachezaji waliopata alama chache katika mechi hiyo walikuwa Sergio Ramos (2.9), Xabi Alonso (2.2), Ozil (2.2), Higuain (2.9), Di Maria (2.8) na Benzema (2.1).

Orodha hiyo pia inawajumuisha Coentrao, ambaye alikuwa miongoni mwa waliopata alama nzuri akipata (3.3), wakati waliopondwa Khedira (2.5), Modric (2.2) na Kaka (2.0). Wastani wa jumla wa timu ulikuwa alama 2.9.

No comments:

Post a Comment