Friday, April 26, 2013

CASILLAS: SINA MAHUSIANO MAZURI NA MOURINHO

Mourinho (mwenye shati jeusi kulia) akifuatilia mechi huku Casillas (kushoto) akiwa hana hata mizuka ya kufuatilia mechi iliyokuwa inaendelea kutokea katika benchi la Real Madrid

NAHODHA wa Real Madrid, Iker Casillas amekiri kwamba hana mahusiano mazuri na kocha Jose Mourinho.

Licha ya kuendelea kuachwa benchi mfululizo, Casillas amesisitiza kwamba wote wanaweka maslahi ya klabu kwanza.

Alisema: "Mahusiano yetu ya kikazi ni ya kiheshima kabisa lakini kwa upande wa mahusiano binafsi hiyo iko wazi kwanza hayako sawa.

"Xabi Alonso alishasema jambo kama hilo pia na sioni kama iko haja ya kuficha ukweli. Nitasema tena, juu ya kila kitu ipo klabu kwanza."

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 31 pia alithibitisha kwamba yupo fiti kwa asilimia 100 na akaahidi kuendelea kupigania namba yake kutoka kwa Diego Lopez.

"Nadhani iko wazi kwamba niko OK kucheza," aliendelea. "Daima niko tayari kuchaguliwa na kocha kikosini na kujaribu kuisaidia timu lakini mwenye maamuzi ya kuteua kikosi ni mtu mwingine, si mimi.

"Nina furaha kwa sababu kwa mwezi mmoja uliopita mkono wangu umepona kabisa na katika muda mrefu nitalazimika kusubiri fursa yangu na kuitumia itakapokuja.

"Baada ya miezi mitatu bila ya kucheza, nimekuwa kama mtoto ambaye anataka kucheza mechi yake ya kwanza kabisa.

"Sitapumzika hata kwa dakika moja. Ni nzuri kwa Diego Lopez kwa sababu nitaendelea kumsukuma na hatapumzika. Amekuwa na kiwango kizuri. Ameisaidia timu kufika hapa tulipo."

No comments:

Post a Comment