Wednesday, March 20, 2013

WAMOROCCO WAJA IJUMAA KUIVAA STARS


Timu ya Taifa ya Morocco (Lions of the Atlas) inatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa Ijumaa kwa ndege ya Emirates tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msafara wa timu hiyo yenye watu 58 wakiwemo maofisa 19 na waandishi wa habari 12 utawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.55 mchana na utafikia hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency.

Siku hiyo Morocco inatarajia kufanya mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, na Jumamosi itafanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa saa 9 kamili alasiri.

Wachezaji walioko kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Rachid Taoussi ni Nadir Lamyaghri, Anas Zniti, Yassine Bounou, Younnes Bellakhadar, Abdellatif Noussair, Abderrahim Achchakir, Zoheir Feddal, Younnes Hammal, Zakarya Bergdich na Abdeljalil Jbira.

Issam El Adou, Kamel Chafni, Salaheddine Saidi, Mohamed Ali Bamaamar, Abdelaziz Barrada, Salaheddine Aqqal, Abdessamad El Moubarky, Nordin Amrabat, Chahir Belghazouani, Abdelilah Hafidi, Youssef Kaddioui, Brahim El Bahri, Hamza Abourazzouk na Youssef El Arabi.

Wakati huo huo, tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa keshokutwa katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Uwanja wa Taifa na Dar Live Mbagala.

Milango siku ya mechi kwa ajili ya watazamaji itafunguliwa saa 6 kamili mchana.

No comments:

Post a Comment