Wednesday, March 20, 2013

KILIMANJARO YAWATAKA WATANZANIA KUJAA MECHI STARS v MOROCCO

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager inayodhamini Timu ya Taifa (Taifa Stars), George Kavishe, akibadilishana mawazo na wachezaji wa Taifa Stars wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Kilimanjaro Premium Lager Jumanne usiku.



Na Mwandishi wetu
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe amesema sasa hivi Timu ya Taifa (Taifa Stars) inauzika na kwamba watanzania wamerudisha imani katika timu hiyo.

Kavishe ambaye Bia yake ndio inadhamini Taifa Stars ameyasema hayo juzi usiku wakati wa chakula cha jioni pamoja na wachezaji wote na benchi la ufundi kilichoandaliwa kwa hisani ya Kilimanjaro Premium Lager ili kuwakaribisha wachezaji kambini.

Alisema wao kama wadhamini wamefarajika na matokeo ya Taifa Stars mpaka sasa na kuwa mwenendo ni mzuri na unaridhisha.

“Watanzania wengi sasa hivi wamerudisha imani katika timu hii kwa hivyo msiwaangushe,” alisema Kavishe na kusisitiza kuwa kwa sasa hivi Taifa Stars inauzika.

Alisema ushindi katika mechi ya Jumapili dhidi ya Morocco kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza katika Kombe la Dunia mwakani Brazil ni lazima na ni muhimu pia kupata ushindi katika mechi ya marudiano mwezi Juni.

Aliwaomba watanzania wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu yao kama walivyofanya wakati wa mechi  dhidi za Zambia na Cameroon.

Alimpongeza Kocha Kim Poulsen kwa kazi nzuri anayoifanya na kusisitiza kwamba anawapa watanzania burudani kwa kuleta ushindi.

“Kocha ameniambia ameiona Morocco ikicheza na wachezaji wake nyota na bila wachezaji nyota kwa hivyo ana mbinu zote za kuikabili Morocco Jumapili…yeye ameshafanya kazi yake ya intelijensia kwa hivyo tusimuangushe,” alisema Kavishe.

Naye kocha Kim Poulsen alisema wachezaji wako katika hali nzuri na tayari kupambana Jumapili ili kuibuka na ushindi.

Alisema udhamini mkubwa na wa uhakika wa Kilimanajro Premium Lager umekuwa chachu kubwa sana katika mafanikio ya Taifa Stars.

“Sasa hivi tuna uhakika wa kambi, wachezaji wanalipwa kwa wakati na pia tunafarajika kuona kuwa mdhamini yuko karibu sana na timu na anaithamini,” alisema Poulsen.

Wachezaji wote 23 wamesharipoti kambini na wanaendelea na mazoezi kila siku ili kujiandaa na mechi dhici ya Morocco itakayochezwa Jumapili saa tisa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Taanzania iko katika kundi moja na Ivory Coast, Gambia na Morocco. Kwa sasa Ivory Coast inaongoza kwa pointi 4, Tanzania 3, Morocco 2 na Gambia 1.

No comments:

Post a Comment