Kevin-Prince Boateng (namba 10) akitoka uwanjani baada ya kukerwa na vitendo vya ubaguzi wa rangi. |
Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA)
limependekeza kwamba marefa wasimamishe mechi wakati kutakapokuwa na matukio ya
ubaguzi wa rangi na kuongeza kuwa “watawaunga mkono” wote watakaofuata ushauri
wao.
Katika maazimio yaliyofikiwa na Chama
cha Klabu za Soka za Ulaya (ECA) na Shirikisho la Wachezaji wa Kulipwa Duniani
(FIFPro), shirikisho hilo la soka la Ulaya likawakumbusha marefa kuwa
wameruhusiwa tokea miaka minne iliyopita kusimamisha mechi kukitokea tukio
lolote kubwa la ubaguzi wa rangi jukwaani au uwanjani.
Maazimio hayo pia yamewataka makocha
na wachezaji kukemea vitendo vya ubaguzi wa rangi hata kama wakijua kuwa
kufanya hivyo kunawakosoa “mashabiki na wachezaji wao wenyewe".
Maazimio hayo yaliandaliwa na Baraza
la Mikakati ya Soka (PFSC) na kupitishwa na kamati ya utendaji ya UEFA, iliyokutana Bulgaria Alhamisi. PFSC
inaundwa na wawakilishi kutoka UEFA, ligi za taifa, klabu za Ulaya na wachezaji.
Maazimio yanapendekeza na kuunga mkono
uamuzi wa kutaka marefa wasimamishe mechi kukitokea ubaguzi na pia kutaka vyama
vya soka na ligi kuu pia kutekeleza maazimio haya".
Mwaka 2009, UEFA ilitaja hatua tatu za
kufuata kabla ya kusimamisha mechi.
Iilisema kwamba refa ni lazima kwanza
asimamishe mechi na kuomba matangazo yatolewe kwa mashabiki. Hatua ya pili
itakuwan ni kuahirisha mechi kwa kipindi fulani na, mwishowe, kuvunja kabisa
mechi husika.
Hadi sasa, hakuna mechi yoyote
iliyoandaliwa na UEFA iliyowahi kuvunjwa na, licha ya maelekezo hayo, kumekuwa
na mechi kadhaa ambazo ziliendelea kuchezwa licha ya uzomeaji wa kibaguzi,
likiwamo tukio la hivi karibuni kwenye mechi ya ligi ya Europa kati ya Inter
Milan na Tottenham Hotspur.
Kevin-Prince Boateng wa AC Milan
alitoka uwanjani kwa hasira baada ya kufanyiwa vitendo vya ubaguzi na mashabiki
wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya timu inayoshiriki ligi ya daraja la chini
Italia ya Pro Patria Januari na baada ya hapo mechi hiyo ikavunjwa.
Maazimio hayo pia yameitaka UEFA, vyama vya soka vya
kitaifa na ligi kuu kutunga kanuni mpya zitakazotoa adhabu kali dhidi ya
vitendo vya ubaguzi.
No comments:
Post a Comment