Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chambani, Mheshimiwa Salim Hemed Khamis ambaye alifariki dunia leo baada ya kuanguka ghafla jana wakati akiendelea na vikao vya kamati za Bunge, ataagwa kesho saa 2:30 asubuhi kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwa ndege saa 4:00 asubuhi kwenda kuzikwa mchana nyumbani kwake Chambani kisiwani Pemba.
Taarifa kutoka ofisi ya Bunge zilieleza kuwa viongozi na wananchi wengine mbalimbali watapata nafasi ya kuuaga mwili wa mbunge huyo kesho na kuzikwa kisiwani Pemba baadaye mchana.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na makamu wake, Mussa Azan Zungu ni baadhi ya wabunge watakaokwenda Chambani kuhudhuria mazishi ya Mheshimiwa Salim Hemed Khamis.
Rais Jakaya Kikwete ametuma salam za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda na pia Chama cha Wananchi (CUF), kufuatia kifo cha mbunge huyo.
“Nimesikitishwa sana na kifo cha Mheshimiwa Salim Hemed Khamis, kifo chake kimetokea wakati ambao Bunge linamhitaji na wananchi wake wa Chambani kuwawakilisha katika vikao vya Bunge vinavyotarajia kuanza Aprili 9 kwa umakini mkubwa,” ilisema sehemu ya taarifa ya rais kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, leo.
TAARIFA ZA KIFO
Mheshimiwa Salim Hemed Khamis, ambaye aliugua ghafla jana wakati akihudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kilichokuwa kikiongozwa na mwenyekiti wake Lowassa, alifariki dunia jana baada ya kuanguka ghafla juzi na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Lowassa ndiye alikuwa wa kwanza kutoa taarifa ya msiba huo leo kwa wajumbe wa kamati yake wakati wakipitia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC).
Lowassa alimkatisha Mbunge wa Kikwajuni (CCM), Hamad Yusuf Masauni aliyekuwa akizungumza na kueleza kwamba mwenzao (Mheshimiwa Salim Hemed Khamis) amefariki duni.
Juzi, Lowassa na makamu wake, Mussa Azzan Zungu walikwenda kumtembelea mbunge huyo hospitalini na kuona kuwa bado alilazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU). Madaktari walibaini kwamba Mheshimiwa Salim Hemed Khamis alipata shinikizo la damu lililosababisha kupata kiharusi na kwamba mshipa mmoja wa damu kichwani mwake ulipasuka.
Chama cha Wananchi (CUF) kilisema leo kupitia taarifa ya kurugenzi yake ya habari: “Uongozi wa CUF unawapa pole wananchi wote, wanachama wa CUF na hasa wananchi wa Jimbo la Chambani kwa kuondokewa na mbunge wao kipenzi. Chama kipo pamoja nao katika wakati mgumu wa kumsindikiza mwenzetu."
Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alielezea pia kusikitishwa na msiba huo na kutuma salamu za pole kwa CUF na wanacnhi wa jimbo la Chambani na kuongeza kwamba makamu mwenyekiti wa chama chake, Mbunge wa Mpanda Said Arfi ametumwa kufuatilia kwa karibu ili kujua namna watakavyoshiriki mazishi.
Kabla ya kufariki leo, marehemu Salim Hemed Khamis aliwahi kuepelekwa India kwa matibabu.
No comments:
Post a Comment