Friday, March 29, 2013

MAITI ZAIDI YA 10 NA MAJERUHI 30 WADAIWA KUCHOMOLEWA KATIKA MABAKI YA JENGO LA GHOROFA 16 LILILOPOROMOKA JIJINI DAR ES SALAAM LEO NA KUWAFUNIKA WATU KIBAO WAKIWAMO MAFUNDI WALIOKUWA WAKIENDELEA KULIJENGA... NI JIRANI NA MSIKITI WA SHIA MAKUTANO YA MOROGORO ROAD NA INDIRA GANDHI... HARAKATI ZA KUCHOMOA MAJERUHI NA MAITI ZAIDI ZINAENDELEA... POLISI WASEMA WALIOKUFA NI WATATU... RAIS KIKWETE ATINGA ENEO LA TUKIO... SERIKALI YASITISHA UJENZI JENGO JINGINE LA JIRANI KAMA LILILOANGUKA LEO NA AMBALO MMILIKI WAKE NI YULEYULE NA MKANDARASI WAKE PIA NI YULEYULE WA JENGO LILILOZUA MAAFA LEO

Mashuhuda wakiangalia jengo lililoporomoka asubuhi hii katika makutano ya Morogoro Road na Indira Gandhi jijini Dar es Salaam leo asubuhi Machi 29, 2013.
 
 




Maafa makubwa yametokea jijini Dar es Salaam leo baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa likiendelea kujengwa kuporomoka na kudaiwa kuwafunika watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 60

Tukio hilo limetokea mishale ya asubuhi katika mitaa ya Posta, jirani na msikiti wa Shia katika eneo la makutano ya Morogoro Road na Indira Gandhi na awali ilidaiwa kuwa miili ya maiti 12 na pia majeruhi zaidfi ya 30 walishachomolewa; ingawa taarifa za polisi zilisema baadaye kuwa maiti waliopatikana ni watatu tu na hughuli za uokoaji zilikuwa zikiendelea.

Aidha, harakati zaidi za uokoaji zingali zikiendelea kufanywa na vikosi kadhaa vya uokoaji, kwa ushirikiano wa polisi na jeshi laulinzi. 


Katika eneo la tukio hilo, tayari viongozi kadhaa wa serikali na makamanda wa Polisi katika kanda maalum ya Dar es Salaam wamefika kusaidia shughuli za uokoaji, miongoni mwao akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete pia alifika katika eneo la tukio na kushuhudia maendeleo ya shughuli za uokoaji.
 
Baadhi ya mashuhuda wamedai kuwa mabaki ya jengo hilo yanaonyesha kuwa mchanga ulikuwa mwingi mno kulinganisha na saruji, hali inayodhaniwa kuwa ni miongoni mwa sababu za kuporomoka kwa mjengo huo uliogharimu mamilioni ya pesa.


POLISI WASEMA WALIOKUFA WATATU 

Hata hivyo, wakati kukiwa na madai kwamba waliokufa wamevuka idadi ya watu 10, taarifa zilizothibitishwa baadaye na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova zilisema kuwa maiti waliochomolewa ni watatu.

Aidha,  Professa Victor Mwafongo wa Muhimbili alisema kwamba maiti walizopokea hospitalini kwao kutokana na tukio la kuanguka kwa ghorofa ni tatu na majeruhi ni 13; huku akiongeza kuwa tayari walishakuwa na vifaa tiba na dawa za kutosha walizopata kutoka bohari ya madawa (MSD) ili kukabiliana na tukio hilo na kwamba, wamejipanga kuhudumia hata majeruhi 100 kwa wakati mmoja.

SERIKALI YAZUIA UJENZI GHOROFA JINGINE KAMA LILILOANGUKA
Wakati huohuo, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadick ameamuru kusimamishwa mara moja kwa ujenzi wa jengo jingine la ghorofa 16 linaloendelea jirani tu na eneo lilikoanguka jengo la leo na kutaka kwanza kufanyike kwa uchunguzi zaidi ili kujiridhisha kuwa hatua za kiusalama na ubora wa jengo hilo zimefuatwa ili kuepuka maafa mengine.

Akizungumza kupitia mahojiano yake na televisheni ya taifa, TBC1, Sadick alisema kuwa serikali imeamua kusimamisha jengo hilo baada ya kubaini kuwa linafanana kwa kila kitu na jengo lililoanguka leo, ikiwa ni pamoja na mmiliki wake na pia mkandarasi anayeendelea na ujenzi huo.


1 comment:

  1. Hayo ndiyo matokeo ya uchakachuaji ambao umekithiri hapa Tz kwa nyanja mbalimbali,Ee MUNGU uyaangalie maisha ya watanzania walio wengi hawajui hii nchi inaendaje kwani wasomi wanatumaliza hivi hivi kwa ULAKU uliokithiri usio na huruma.Katika haya wengine wamejilimbikizia mali ingali mishahara yao haindani na mali zao MUNGU nini wewe tu unajua thamani ya Wanadamu!Haya watanzania tujifunze kuhuzunikia matukio kama haya kwani wengi wa waliopoteza maisha yao hapo ni akina sisi kajamba tatu(Walala hoi)sasa unategemea nini?

    ReplyDelete