Tuesday, March 12, 2013
KOMBE LA AMANI LILIVYOWAWEKA PAMOJA WAISLAMU, WAKRISTO BUSERESERE
Na Mwandishi Wetu, Geita
MICHUANO ya Kombe la Amani na Upendo ilimalizika Jumapili kwa kikosi cha Katoro kutangazwa mabingwa wapya wa michuano hiyo baada ya kushinda mechi yao ya fainali kwa penalti 5-4 dhidi ya Buseresere kwenye Uwanja wa Katoro mjini hapa.
Mashindano hiyo yalimalizika huku waumini waislamu na wakristo wakazi wa eneo la Buseresere na Katoro wakifikia mwafaka wa mgogoro mkubwa wa kidini uliosababisha maafa na watu kujeruhiwa.
Mhamasishaji Eric Shigongo aakiambatana na Mhariri Kiongozi wa gazeti la Championi, Saleh Ali, walifanya usuluhishi huo kwa kuwakutanisha Waislamu na Wakristo hadi mwafaka ulipofikiwa na pamoja wakasaini makubaliano ya kumaliza mgogoro huo na kukumbatiana.
Kabla, ilionekana mgogoro huo uliosababishwa kuuawa kwa mchungaji na Mwislamu mmoja kupigwa risasi ya mguu, kama ulishindikana.
Waumini wa Kikristo walitaka kupewa haki ya kuchinja, hali iliyozua tafrani kubwa miongoni mwao hadi kusababisha mauaji hayo, hali iliyozaa uadui mkubwa.
Wakuu wa mikoa, wilaya akiwamo Steven Wassira na baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda walijaribu kuusuluhisha bila ya mafanikio.
Waliendelea kuwa na mgogoro, kutopendana na hata katika misiba ya upande mmoja, walikuwa hawahudhurii, kitu kilichozidisha uadui mkubwa miongoni mwao.
Shingongo aliongoza mikutano miwili, akianza na wachungaji na baadaye masheikh, halafu baadaye kikafanyika kikao cha mwisho ambacho kiliwakutanisha pamoja na viongozi wa serikali akiwamo mbunge, Gaudencia Bukwimba.
Kikao cha mwisho kilichochukua zaidi ya saa nne, kilimalizika kwa mchungaji Isaya Ikiri na Sheikh Ismail Ibrahim kuwekeana saini ya makubaliano ya amani kati yao.
Kati ya makubaliano waliyofikia ni Waislamu kuendelea kuchinja, lakini Wakristo wanaweza kuchinja lakini nyama yao isiingie katika biashara. Wanapochinja wanaweza kugawana wao na kula majumbani mwao na si kuuza buchani.
Lakini pia walitakiwa kuwa makini, kwamba atakayekiuka makubaliano hayo achukuliwe hatua za kisheria kama yeye binafsi na si Wakristo kwa ujumla kuwa ndiyo wamekiunga mkono.
Baada ya hapo, kwa pamoja wakaungana na kwenda kwenye mechi ya fainali ambayo Katoro walitwaa kombe hilo.
Kabla ya kukabidhi kombe, masheikh na wachungaji walizungumza na kusisitiza sana suala la amani pia wakazungumzia mapatano yao baada ya kikao na mashabiki waliokuwa uwanjani hapo walishangilia sana.
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment