Monday, March 11, 2013

WAMILIKI WA TELEVISHENI WAITAKA SERIKALI IACHE KULAZIMISHA WATU KUTUMIA VING'AMUZI NA BADALA YAKE WARUHUSU KUREJEA KWA MFUMO WA ZAMANI... WASEMA HIVI SASA WANAPATA HASARA KUBWA NA KAMA SERIKALI IKIENDELEA KULAZIMISHA MFUMO WA SASA WATASIMAMISHA MATANGAZO YA TV ZOTE NCHINI ZIKIWAMO ZA ITV, STAR TV, CLOUDS TV, CHANNEL TEN, EATV...!


Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi akizungumza na waandishi wa habari jana kuelezea athari za agizo la serikali kuhusu urushaji wa matangazo kwa mfumo wa digitali. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Media Group Ltd (Star TV), Samwel Nyalla na kushoto ni Rugemalira Mutahaba ambaye ni  Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa Clouds Media Group.
Wamiliki wa vituo vya utangazaji nchini wameomba kuruhusiwa kwa muda matumizi ya mfumo wa utangazaji wa analojia na digitali ili wananchi wasiokuwa na uwezo waendelee kupata habari kupitia luninga.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, walisema kuwa kuharakishwa kwa uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya analojia nchini kunawakosesha wananchi wengi wa kipato cha chini haki ya kikatiba ya kupata habari kupitia televisheni kwa kushindwa kumudu bei ya ving’amuzi, huku vituo vya televisheni vikikabiliwa na hatari ya kufungwa kutokana na kupungua kwa kasi ya matangazo ya biashara.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi, alisema kuwa mfumo wa sasa wa digitali unaowalazimisha wananchi wote kupata matangazo ya televisheni kupitia ving’amuzi unawakosesha wengi matangazo hayo na matokeo yake, wamiliki wa vituo vya TV wanathirika kutokana na watangazaji kupunguza matangazo yao na hivyo kuvikosesha vituo hivyo fedha za kuendeshea shughuli zao kupitia matangazo ya kibiashara kama ilivyokuwa zamani.

Dk. Mengi ambaye alifuatana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Media Group Ltd (Star TV), Samwel Nyalla na Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, alisema ana matumaini kuwa kilio chao kitasikilizwa mapema ili kuwawezesha wananchi wa kawaida kupata habari na vituo vya televisheni kupata matangazo ya biashara ya kutosha yatakayowapatia fedha za kugharimia uendeshaji.

“Wananchi wengi ni walalahoi ambao hawana uwezo wa kulipia ving’amuzi. Sisi kama wamiliki wa vituo vya TV tunapata hasara kwani hatuapati matangazo ya kutosha tunapotazamwa na watu wachache,” alisema.

Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP inayomiliki vituo vya tv vya ITV, EATV na Capital TV, aliongeza kuwa bado wanaendelea kufanya taratibu za kuisihi serikali itekeleze yale wanayoomba na kwamba wataendelea kufanya subira kwa miezi kati ya miwili hadi mitatu kuanzia sasa na wakiona kuwa bado serikali iko kimya, watakachokifanya ni kufunga vituo vyao vyote vya televisheni na kuendelea na biashara nyingine.


“Tumekuwa tukijadiliana na wahusika kwa njia zisizo rasmi, lakini bado tatizo lipo. Miezi miwili au mitatu ijayo hatutaona tv labda TBC (TV ya Taifa). Kama huo ndiyo ulikuwa mpango wa kuondoa tv, basi wamefanikiwa. Lakini naamini lengo lao lilikuwa kuboresha matangazo ya tv. Kwanini ifanywe haraka hivyo?” alihoji Dk. Mengi.
Alisema kuwa wadau wa tv walishirikishwa na TCRA katika hatua za kuhama kutoka analojia kwenda dijitali, lakini hawakuhusishwa katika kuamua muda na utaratibu wa uzimaji wa mitambo ya analojia.

“Hatua ya kuhama ina madhara makubwa sana. Kinachosikitisha zaidi, nchi tajiri hawakufanya haraka kuingia katika mfumo huu, USA (Marekani) walitumia miaka 14, UK (Uingereza) miaka 11, Hispania miaka 10 na Japan miaka minane. Sisi tumetumia muda mfupi sana,” alisema.

“Hakuna msaada wowote unaotoka serikalini kuwawezesha Watanzania wenye hali duni kiuchumi kumudu gharama za ving’amuzi. Huku ni kuwanyima haki ya kupata habari wananchi ambayo ni ya kikatiba kwani Ibara ya 18 ya katiba yetu inatamka wazi kuwa wananchi wana haki ya kupata habari.

“Mambo yanayofanywa nchini lazima yaangalie hali halisi ya maisha ya Watanzania. Watanzania wametumbukia kwenye giza; giza la kutopata habari. Ombi letu kwa serikali ni kurudisha mfumo wa analojia uende sambamba na mfumo wa digitali wakati watu wanajipanga vizuri zaidi.”

MTENDAJI MKUU SAHARA
Kwa upande wake Nyalla alisema kuwa wameshangaa kuona Tanzania inazima mitambo ya analojia huku hali ya uchumi wa wananchi wake ikiwa duni na kwamba baadhi ya vituo vya tv hasa vya mikoani vimefungwa kwa vile haviwezi kumudu uendeshaji wa mfumo mpya wa utangazaji wa digitali.

Nyalla alisema kuwa kituo chake cha Stars TV, kimekumbwa na tatizo la kupungua kwa matangazo hali ambayo imeathiri shughuli za uendeshaji.
“Tumekimbilia kwenye digitali kwa faidi ipi hasa?” alihoji na kuongeza: “Tunajiuliza kwa nini hasa kuna kitu hiki. Hakuna ruzuku ambao sisi wamiliki wa vyombo wa habari binafsi tunaoupata kutoka serikalini kusaidia kuinua mipango ya vituo vyetu.”

Mkurugenzi huyo aliendelea kueleza kuwa idadi ya ving’amuzi ambavyo hadi sasa vimo nchini ni kati ya 500,000 na 600,000, idadi ambayo inamaanisha kwamba Watanzania wengi hawatazami tv kwani idadi ya Watanzania ni zaidi ya milioni 44 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka jana.

MKURUGENZI CLOUDS
Naye Mutahaba alisema vituo vya tv nchini bado havijaandaliwa vyema kukabiliana na ushindani wa habari na tv za mataifa ya nje katika mfumo mpya wa utangazaji wa digitali.

“Kutokana na hali halisi ya uendeshaji wa vyombo vyetu, bado hatuna uwezo wa kushindana na mataifa ya nje. Kulipia kodi ya matangazo ndani ya nchi yetu inakuwa vigumu,” alisema Ruge.
Kwa mujibu wa Ruge, gharama ya kupeleka matangazo ya tv kwa kila mkoa nchini ni Dola za Marekani 3,800 (Sh. milioni sita) kwa mwezi.

TCRA WANENA
Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema jana kuwa maamuzi ya Tanzania kuingia kwenye mfumo wa utangazaji wa digitali ni makubaliano ya kimataifa huku akisisitiza kuwa kila nchi lazima iingie katika mfumo.

“Suala la digitali ni la kimataifa, kila nchi lazima itumie mfumo huo. Ombi la wamiliki wa vyombo vya habari kuhusu analojia siwezi kulizungumzia kwa sasa kwa sababu ni la kiserikali, halipo kwenye mamlaka hii. Nafikiri waulize Maelezo (Idara ya Habari), wao ndiwo watatoa tamko la serikali,” alisema Mungy.

Alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala hilo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Maelezo, Assah Mwambene, alisema kuwa maombi ya wamiliki wa vyombo vya habari (TV) hadi jana saa 12:25 jioni yalikuwa hayajawasilishwa rasmi kwenye ofisi yake.

“Hatujapokea barua rasmi ya maombi yao. Wakituandikia tutawajibu,” alisema Mwambene.

Serikali ililazimisha kuanza urushaji wa matangazo kupitia mfumo wa ving’amuzi kuanzia Januari Mosi, 2013 na kuzima kwa awamu matangazo yote ya televisheni kupitia njia iliyokuwa ikitumika awali ya analojia isiyohitaji ving’amuzi bali antena za kawaida.

1 comment:

  1. Huu ni mradi mwingine wa mafisadi unaolenga kuwakamua maskini. Mafisadi wamekaba hadi penati, mwananchi wa kawaida hana pa kupumulia. Baada ya huu mradi kuanzishwa baadhi ya channel za nyumbani kama vile Clouds TV, CTN, C2C, Mlimani TV, Tumaini TV, Capital TV, DTV na channel zingine kibao tu hazipatikani kabisa! Tunalazimishwa kulipia visimbuzi vinavyoonyesha channel nyingi za kipuuzi na ambazo hazina mwelekeo wowote. Ni afadhali hawa wachumia tumbo wangetuacha tukae na madishi au antennae zetu za analogia kama ilivyokuwa kabla. Kwani lazima wote tuingie digitali?

    Hawa wachumia tumbo ni wepesi sana kuiga mambo ya kipuuzi kwa manufaa ya mafisadi wachache kuliko kuiga mambo yanayoweza kuwanufaisha wananchi wote. Hivi sasa karibu 70% ya maeneo yaliyokumbwa na huu upuuzi hawana mawasiliano ya TV. Wananchi wengi bado ni maskini (wanaishi chini ya dola moja kwa siku) halafu hawa “matumbo pakacha” wanakuja kuwaongezea ughali wa maisha kwa kuwalipisha pesa za vocha za visimbuzi kila mwezi? Matokeo yake wananchi maskini wameamua kurejea kwenye usikilizaji wa redio na kusoma magazeti na vipeperushi. Sasa ndio tumerudi analogia zaidi kuliko ilivyokuwa kabla huu mradi wa mafisadi haujaanza. Tafakari, chukua hatua!

    ReplyDelete