Sitaki tena uongozi... nimechoka kutukanwa...! -- Kaburu |
Simba tena basi... nawapisha wengine! -- Zacharia Hanspope |
Hatua hiyo ya kubwaga manyanga kwa Kaburu, imekuja muda mfupi tu baada ya kujiuzulu leo hii pia kwa mjumbe wa kamati ya utendaji ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati yao ya usajili, Zacharia Hanspope.
Kaburu amesema kwamba ameamua kubwaga manyanga kwa vile anaona kuwa ni kazi ngumu kuongoza Simba kwani licha ya jitihada anazofanya katika kushirkiana na wenzake ili waifikishe mbali klabu yao, bado amekuwa akikumbana na matusi kila uchao na kuchoshwa na hali hiyo.
"Ni vigumu sana kuongoza klabu yetu. Viongozi tunatukanwa... sasa nimechoka," amsema Kaburu, huku akiwatakia kheri wanachama wengine watakaoongoza ili waifikishe mbali.
Hanspoppe amesema kuwa ameamua kujiuzulu kufuatia matokeo mabaya ya timu yao katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara na pia kipigo cha aibu walichopata katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuchapwa kwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, amekiri kupokea barua za kujiuzulu kwa Kaburu na Hanspope.
Wakati hayo yakitokea, mwenyekiti wa klabu hiyo inayoshikilia ubingwa wa Tanzania Bara, Ismail Aden Rage, bado yuko nchini India alikokwenda kwa matibabu.
Baadhi ya wanachama wa Simba wamekuwa wakishinikiza viongozi wao kuachia ngazi kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya, lakini Rage aliwahi kupuuza rai ya kutakiwa kujiuzulu kwa maelezo kwamba yeye siyo mchezaji wala kocha.
No comments:
Post a Comment