Sunday, February 3, 2013

WENYEJI BAFANA WAAGA KWA MATUTA... MALI, GHANA ZATINGA NUSU FAINALI

Hoi..... Wachezaji wa Bafana Bafana wakiwa hawaamini kilichotokea

Asante kaka wewe ni shujaa... Wachezaji wa Mali wakimpongeza kipa wao So Diakite kwa kuokoa penalti zilizowatoa wenyeji Bafana Bafana katika hatua ya robo fainali. Mali  
Wachezaji wa Ghana wakimpongeza mfungaji wa magoli yao yote mawili, Wakaso


MALI walitinga nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kuwatoa wenyeji Afrika Kusini kwa "matuta" 3-1 kufuatia sare ya 1-1 ya dakika 120.

Bafana Bafana walikosa penalti tatu, huku Lehlohonolo Majoro akipiga nje yake na kuwapa Mali ushindi.

Wenyeji walifunga goli la kuongoza katika kipindi cha kwanza, kupitia kwa straika Tokelo Rantie aliyetumbukiza mpira wavuni kutokea jirani na lango kufuatia krosi ya Thuso Phala.

Nahodha wa Mali, Seydou Keita aliisawazishia timu yake, akifunga kwa kichwa dhidi ya kipa wa Afrika Kusini, Itumeleng Khune kutokea jirani na goli.

Afrika Kusini walionekana kama vile wanalipa kisasi cha kufungwa na Mali katika hatua hiyo hiyo mwaka 2002, lakini Mali kwa mara nyingine walizima matumaini ya wenyeji, kama walivyoshinda kwa "matuta" dhidi ya wenyeji Gabon katika robo fainali mjini Libreville mwaka jana.

Katika mechi iliyochezwa mapema, Ghana ilikuwa ya kwanza kutinga nusu fainali baada ya Mubarak Wakaso kufunga penalti ya utata na goli la shambulizi la kustukiza katika ushindi wa 2-0.

Baada ya kipindi cha kwanza kilichodorora, Ghana walipata penalti wakati Asamoah Gyan alipoanguka baada ya kugongana mabega na Carlitos na Wakaso akafunga penalti hiyo.

Cape Verde walicharuka vyema na kipa wa Ghana, Fatau Dauda aliokoa kiufundi hatari kutoka kwa Platini, Djaniny na Heldon.

Lakini Wakaso alikimbia peke yake huku kipa wa Cape Verde akiwa amepigiliwa misumari sakafuni na kufunga la pili.

Ulikuwa ni mwisho mbaya kwa Cape Verde, ambao walikaribia kupata goli la kusawazisha ambalo walistahili kutokana na mizani sawa ya mechi hiyo katika kipindi cha pili.

Lakini walisambaratishwa na penalti ya "utata" na goli la dakika ya mwisho wakati walipompeleka kila mtu mbele kusaka goli la kusawazisha na itakuwa kumbukumbu mbaya katika fainali zao za kwanza za Mataifa ya Afrika.


Mechi za leo za robo fainali AFCON:
  • Ivory Coast v Nigeria saa 12:00 jioni
  • Burkina Faso v Togo saa 20::30 usiku

No comments:

Post a Comment