Sunday, February 17, 2013

WENGER: MSIMU WA ARSENAL HAUJAISHA

Kocha Arsene Wenger wa Arsenal akijiuliza baada ya timu yake kufungwa 1-0 dhidi ya Blackburn Rovers kwenye Uwanja wa Emirates mjini London, England Februari 16, 2013.

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema msimu wa timu yake haujaisha licha ya kutolewa nje ya Kombe la FA na timu ya daraja la kwanza ya Blackburn.

Arsenal hawajatwaa taji lolote tangu walipobeba Kombe la FA mwaka 2005 na wamebaki kuwania kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya tu wakati wakiwakabili Bayern Munich Jumanne.

Wenger alisema: "Inauma sana kupoteza mechi kama ile. Kilicho muhimu ni kuweka nguvu katika mechi inayokuja.

"Msimu haukamalizika. Kwenu labda, lakini siyo kwangu."

Wenger (63) aliongeza: "Kama tunajilaumu tutakuwa tunakosea. Tuna mechi kubwa Jumanne usiku na ni lazima tuonyeshe kwamba tunaweza kufanya mambo."

Arsenal, ambao ni wa tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, walitawala mechi kwenye uwanja wa Emirates huku Jack Wilshere, Theo Walcott na Santi Cazorla wakianzia benchi na wakaingizwa katika dakika ya 70.

Lakini dakika mbili baadaye goli la kushtusha kutoka kwa Colin Kazim-Richards' liliwapa ushindi usiotarajiwa wakati Arsenal wakipoteza mechi ya Kombe la FA dhidi ya timu ya daraja la chini kwa mara ya kwanza tangu 1996.

Arsenal walilala kwa timu ya Daraja la Tatu ya Bradford katika Kombe la Capital One Desemba.

Klabu ya Ujerumani ya Bayern Munich inaongoza kwa tofauti ya pointi 18 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Ujerumani na watakuwa wakiwania ubingwa wa tano wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakati watakapokuwa wageni wa Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates Jumanne kwa ajili ya mechi yao ya kwanza ya hatua ya 16-Bora.

No comments:

Post a Comment