Monday, February 4, 2013

TIKETI STARS, CAMEROON KUANZA KUUZWA FEB 5


Tiketi kwa ajili ya pambano la kimataifa la kirafiki kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Cameroon (Indomitable Lions) zinaanza kuuzwa kesho (Febaruari 5 mwaka huu) katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Viingilio katika pambano hilo litakalochezwa Jumatano (Februari 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni ni sh. 5,000 (viti vya kijani), sh. 7,000 (viti vya bluu), sh. 10,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na sh. 30,000 VIP A.

Vituo vitakavyouzwa tiketi hizo kuanzia saa 2 asubuhi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio, Oilcom Ubungo, Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta Buguruni.

Vilevile tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi, na milango itafunguliwa saa 8 kamili mchana.

Wakati huo huo, kundi la kwanza na la pili la wachezaji wa Cameroon tayari limetua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Cameroon chini ya Kocha Jean Paul Akono itafanya mazoezi kesho saa 11 jioni Uwanja wa Taifa. Nayo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager yenyewe itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa leo saa 11 jioni.

No comments:

Post a Comment