| ||
Wananchi wakiangalia gari alilokuwamo Padri Mushi wa Zanzibar wakati akiuawa kwa kupigwa risasi tatu kichwani visiwani humo jana. |
Akina mama wakilia kufuatia kuuawa kwa Padri Mushi |
Mwili wa marehemu |
Gari la Padri Mushi lionavyoonekana baada ya kuparamia ukuta kufuatia mwenyewe kupigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana. |
Padri Mushi (wa pili kulia) enzi za uhai wake (Picha: Kwa hisani ya Francis Dande) |
Padri Mushi enzi za uhai wake |
Mauaji haya ni mfululizo wa hujuma dhidi ya viongozi wa dini visiwani Zanzibar na linatokea zaidi ya mwezi mmoja baada ya Padri Ambrose Mkenda, kujeruhiwa kwa kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika mwishoni mwa Desemba, mwaka jana, hadi leo waliotekeleza unyama huo hawajakamatwa.
Kiongozi mwingine wa kidini aliyekumbwa na masahibu visiwani Zanzibar ni Sheikh Soraga, ambaye alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.
Jana Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, aliitisha mkutano wa ghafla na waandishi wa habari Makao Makuu ya Polisi kutoa taarifa za mauaji ya Padri Mushi, mbali ya kuthibitisha unyama huo, alisema aliuawa na watu wasiofahamika majira ya asubuhi alipokuwa anakwenda kuendesha misa katika Kanisa Katoliki la Betras lililopo eneo la Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, alikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na baadaye alifariki dunia.
Mwema alisema kutokana na kujirudiarudia kwa vitendo vya kuwashambulia na kuwadhuru viongozi wa dini na uchomaji wa nyumba za ibada, jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limeanza uchunguzi kuwabaini waliohusika na matukio hayo.
Aidha, alisema watu watatu wanashikiliwa kwa kuhusishwa na tukio la jana na kwamba majina yao hayawezi kutajwa hivi sasa kwa sababu za kiusalama.
TIMU YA WATAALAM YAPELEKWA ZANZIBAR
Kufuatia kutokea kwa tukio hilo la mauaji, Mwema alisema ametuma timu ya wataalam waliobobea kwenye masuala ya upelelezi na operesheni kutoka makao makuu ya polisi itakayokwenda kushirikiana na wataalam walioko Zanzibar.
Aliwataja watu hao kuwa ni Naibu Kamishna wa Polisi Samson Kasara, atakayesimamia kazi ya upelelezi wa matukio hayo, Naibu Kamishna Peter Kivuyo, atakayesimamia ukusanywaji wa taarifa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Simon Sirro, atakayesimamia operesheni.
AOMBA UTULIVU
Kadhalika, IGP Mwema amewaomba wananchi haswa wa Zanzibar, wawe watulivu wakati suala hilo linaposhughulikiwa kuhakikisha wahalifu hao wanakamatwa na sheria inachukua mkondo wake.
Alisema Jeshi la Polisi limeimarisha doria maeneo yote nchini, kufuatilia mienendo na kuhakikisha kuwakamata watu wote wanaochochea, kufadhili, kuhamasisha na kushiriki katika vitendo vya uhalifu, vurugu na fujo.
Aliwaomba wananchi kushirikiana na polisi katika kuwabaini waliohusika na tukio hilo kwa kupiga simu kwenye namba 0754 785557 au 0782 417247, pamoja na kupiga namba za makamanda wa mikoa na vikosi ili kuhakikisha amani, usalama na utulivu vinadumishwa hapa nchini.
“Kama tumeweza kushirikiana na wananchi kwa majambazi wa kwenye mabenki, nina imani ushirikiano huo utaendelea katika kuwabaini waliohusika na tukio hili,” alisema IGP.
Alisema Jeshi la Polisi pia linachunguza tukio hilo ili kubaini kama linahusiana na masuala ya ugaidi, dini au siasa.
Hili ni tukio la pili katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja tangu Padri wa kanisa hilo, Ambrose Mkenda, kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika mwishoni mwa Desemba, mwaka jana.
Padri Mkenda alitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akitokea katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja visiwani humo baada ya kupigwa risasi katika taya na mgongoni.
Tukio la kupigwa risasi kwa Padri Mkenda, lilitokea miezi mitatu tangu Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, amwagiwe tindikali na watu wasiojulikana na kupelekwa kwenye matibabu nchini India.
Matukio ya viongozi wa dini kuhujumiwa yametanguliwa na matukio ya kuchomwa moto baa 12 na makanisa 25 katika maeneo tofauti visiwani Zanzibar.
Padri Mkenda alipigwa risasi saa 1:30 jioni nyumbani kwake. Alipigwa risasi na watu wawili wasiojukana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa kupitia kioo cha mbele ya gari lake aina ya Toyota Rav4 lenye namba za usajili Z 586 AW wakati akirudi nyumbani kwake baada ya kutoka kanisani kuhudhuria misa.
JK ATUMA RAMBIRAMBI
Rais Jakaya Kikwete, amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Mushi.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kwa vyombo vya habari jana ilimkariri Rais Kikwete akisema “nawapa pole nyingi na rambirambi za dhati ya moyo wangu Baba Askofu Augustino Shayo wa Jimbo Katoliki, Zanzibar na waumini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba huo mkubwa uliowakuta.”
Alisema ”Napenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha mpendwa Padri Evarist Mushi na kuwa msiba huu ni wa kwetu sote.”
“Nimeliagiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria…nimewaagiza Jeshi la Polisi washirikiane na vyombo vingine vya Usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji haya,” alisema Rais Kikwete.
POLISI WAELEZA ALIVYOUAWA
Akizungunza na waandishi wa habari makao makuu ya Jeshi la Polisi huko Ziwani, Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema kiongozi huyo wa kiroho alipigwa risasi tatu jana saa 12:45 asubuhi.
Alisema Padri Mushi alikuwa akitokea nyumbani kwake katika Kanisa la Minara Miwili mtaa wa Shangani akienda kuongoza misa ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Theresia eneo la Kibweni Zanzibar.
Mussa alisema Mushi akiwa katika gari aina ya Toyota Hilux Surff yenye namba za usajili Z162 AT, alipigwa risasi tatu kichwani kupitia dirisha la mlango wa kulia wa gari hilo.
Alisema watu hao walikuwa wamemtega mita chache kutoka kanisani na wakati akipinda kona karibu na eneo la kanisa, walifanya shambulio na kutoweka wakiwa na usafiri wa pikipiki aina ya Vespa.
Kamishna Mussa alisema baada ya kiongozi huyo kupigwa risasi, gari lake lilipoteza mwelekeo na kugonga ukuta wa nyumba ambayo ipo mita chache kutoka katika Kanisa la Mtakatifu Theresia.
“Walitoweka baada tu ya kumpiga risasi wakiwa na vespa na polisi tunaendelea na msako mkali kufuatia tukio hulo,” alisema Kamishina Mussa.
Upande wake, Dk. Msafiri Marijani, kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja alisema marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitibabu imeonekana alikuwa na majeraha matatu kichwani.
“Amepigwa risasi sehemu tatu tofauti na kuathiri ubongo wake,” alisema Dk. Marijani.
Hata hivyo, alisema walilazimika kwenda eneo la tukio kutafuta vitu muhimu kwa ajili ya kukamilisha hatua za uchunguzi wa tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema Rais Kikwete, ametoa kibali cha kuruhusu wapelelezi bingwa wa kimataifa kuja kusadia kazi ya kuwasaka watu wanaofanya vitendo vya hujuma dhidi ya viongozi wa dini Zanzibar.
Alisema watu wanaofanya vitendo hivyo ni magaidi na siyo majambazi na serikali imeamua kutumia gharama yoyote kuwasaka.
“Serikali itatumia nguvu zote kuwasaka magaidi hawa na lazima walipie udhalimu wao,” alisema Waziri Nchimbi.
Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alisema serikali imeliangiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwatambua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya hujuma dhidi ya viongozi wa dini na raia wasiokuwa na hatia visiwani Zanzibar.
ASKOFU HAFIDH: TUMECHOKA
“Tukio la kwanza unaweza kusema tumejikwaa kwa hili lazima serikali tuone inaondoa tatizo, tumechoka,” alisema Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Zanzibar, Michael Henry Hafidh.
Alisema Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ni kiongozi mzuri lakini anaangushwa na watendaji wake ambao wamekuwa wakifanya kazi huku wakichanganya siasa na dini kinyume cha misingi ya utawala wa sheria.
Baadhi ya waumini katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, walisema kabla ya tukio hilo, kulisambazwa vipeperushi vikiwa na ujumbe `Kama hatupati nchi yetu tutafanya tukio kubwa kuliko la kupigwa risasi Padri Mkenda’ walikariri vipeperushi waumini hao.
Tina Yohana, mkazi wa Dole, alidai kuwa vipeperushi hivyo vilisambazwa katika Kanisa la Katoliki Kianga kabla ya kutokea kwa tukio la kuawa kwa kiongozi huyo.
Alisema vipeperushi hivyo vilieleza kwa tukio litakalotokea waumini wa kanisa hilo hawatalisahau maishani mwao.
Mapema, waumini wa Kikristo walikusanyika kwa wingi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na wengi wao wakishindwa kujizuia kulia kufutia kuaawa kwa kiongozi wao.
TEC YAENDA ZANZIBAR
Msemaji wa Baraza la Maaskofu la Tanzania (TEC), Padri Anthony Makunde, jana alielekea visiwani Zanzibar kwenye tukio la mauaji ya Padri Mushi.
Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kwa maelezo kuwa amesafiri kwenda nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment