Sunday, February 17, 2013

LAMPARD AFUNGA GOLI LA 199... CHELSEA, MAN CITY ZAUA KOMBE LA FA

Lampard akipongezwa na kocha rafa Benitez leo
Yaya Toure akishangilia pamoja na Aguero wakati wa mechi yao dhidi ya Leeds leo

LONDON, England
FRANK Lampard alifunga goli lake la 199 kwa klabu ya Chelsea wakati mabingwa hao wa Kombe la FA walipoipiku timu yenye hamasa ya Brentford kwa kuishindilia magoli 4-0 katika mechi yao ya marudiano ya raundi ya nne kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, huku Manchester City pia ikiichakaza Leeds United 4-0 katika mechi ya raundi ya tano.

Muargentina Sergio Aguero alifunga mara mbili wakati mabingwa wa Kombe la FA wa mwaka 2011 Manchester City walipotinga robo fainali kwa soka la kujiamini tofauti na walipolala 3-1 kwenye Ligi Kuu dhidi ya Southampton wikiendi iliyopita.

Goli la mapema lililopikwa vyema la Yaya Toure liliwaweka Man City katika nafasi nzuri dhidi ya timu ya daraja la kwanza ya Leeds, Aguero akaongeza la pili kwa penalti kabla ya Carlos Tevez kufunga la tatu mara baada ya mapumziko na Aguero akakamilisha ushindi mnono katika dakika ya 74.

Magoli ya kipindi cha pili kutoka kwa Juan Mata, Oscar, Lampard na John Terry dhidi ya timu hiyo ya daraja la tatu, yaliipa Chelsea fursa ya kutinga raundi ya tano ya michuano hiyo ambapo sasa watachuana na timu ya daraja la kwanza ya Middlesbrough Februari 27.

Kiungo wa timu ya taifa ya England, Lampard, ambaye hatma yake Chelsea bado iko shakani huku mkataba wake ukimalizika mwisho wa msimu, alifunga katika dakika ya 71 na kuzidi kuikaribia rekodi ya muda wote ya ufungaji magoli mengi zaidi ya klabu hiyo inayoshikiliwa na Bobby Tambling aliyefunga magoli 202.

Goli hilo liliwafanya mashabiki wa Chelsea kuanza kuimba 'msajili' wakati mmiliki bilionea Roman Abramovich, aliyekuwa amekaa huku mikono yake ameizamisha mifukoni, akilazimika kutoa tabasamu.
Kocha wa muda Rafael Benitez alisema: "Timu ilicheza vizuri na Frank Lampard anafunga magoli, jambo ambalo ni zuri kwake na kwetu."

Chelsea mara mbili walilazimika kuzinduka kutoka nyuma kupata sare ya 2-2 katika mechi yao ya kwanza kwenye Uwanja wa Griffin Park na kwa mara nyingine katika kipindi cha kwanza jana walianza kwa kuchechemea dhidi ya wapinzani hao wa mji mmoja wa London.

Mata hatimaye alivunja ukuta mgumu wa Brentford katika dakika ya 54 wakati alipoikimbilia pasi ya Demba Ba kutokea katika mpira mrefu uliopigwa na kipa Petr Cech na kufumua shuti la mguu wa kushoto la umbali wa mita 20.

Oscar alifunga goli la pili dakika 14 baadaye akitumia krosi ya Branislav Ivanovic, na Lampard haraka akaongeza goli la tatu kwa shuti la kuunganisha kufuatia krosi ya Mata. Terry alifuga kwa kichwa na kufanya matokeo yawe 4-0 katika dakika ya 81.

"Kipindi cha kwanza walifanya mambo magumu kwetu, walikaa nyuma sana. Tulipopata goli la kwanza, la pili na la tatu yalionekana lazima yatakuja," Terry, aliyerejea baada ya kukosa mechi mbili kutokana na tatizo la goti, aliiambia ITV.

Terry alisema ripoti zilizotoka jana kwenye vyombo vya habari vya Uingereza kwamba yeye na Benitez waligombana katika chumba cha kuvalia zilikuwa ni "upuuzi mtupu".

"Kulikuwa na stori leo katika gazeti lakini ni uandishi wa kivivu," alisema beki huyo, akimaanisha habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Sun chini ya kichwa cha habari kilichosema "Vita".

No comments:

Post a Comment