Tuesday, February 12, 2013

NYOTA EPIQ BONGO STAR SEARCH KUZURU MIKOANIMeneja Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, Awaichi Mawalla akizungumzia onesho la wasanii wa shindano la EBSS 2012 watakaoanza ziara yao Ijumaa hii mkoani Dodoma

Msanii Nsami Nkwabi akizungumzia ziara ya wasanii wa EBSS 2012 itakayoanza keshokutwa mkoani Dodoma. Kulia kwake ni Meneja Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, Awaichi Mawalla.

Meneja Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, Awaichi Mawalla akizungumzia onesho la wasanii wa shindano la EBSS 2012 watakaoanza ziara yao Ijumaa hii mkoani Dodoma

WASANII walioingia katika 'Top 10' ya mashindano ya kusaka vipaji vya kuimba ya Epiq Bongo Star Search watashiriki kampeni ya mikoani itakayoanza Ijumaa hii mjini Dodoma na kisha kufuatiwa na Dar es Salaam.

Ziara hiyo itajumuisha vijana Menina Atick, Nsami Nkwabi, Husna Nassor, Geofrey Levis, Wababa Mtuka, Norman Severino pamoja na mshindi wa Sh. milioni 50, Walter Chillambo.

Wasanii waalikiwa watakaotoa burudani kwenye ziara hiyo ni Barnaba, Ben Paul, Linah na Ali Nipishe.

Katika ziara hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2006, wapenzi wa muziki watapata fursa ya kumshuhudia mshindi wa Epiq BSS, Walter Chilambo ambaye atakuwa akizindua wimbo wake.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara hiyo, Afisa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan, alisema dhumuni la ziara hiyo ni kuwajengea vijana hao msingi katika kazi yao ya muziki baada ya shindano la Epiq BSS kuisha.

"Lengo letu kuu la kudhamini Epiq BSS haikuwa kumpa mshindi zawadi, la hasha, bali tulikuwa na mpango madhubuti wa kubadilisha maisha ya vijana hawa kupitia vipaji vyao," alisema Khan.

"Lakini pia dhumuni la Zantel ni kuonyesha kuwa kwa kufanya uwekezaji sahihi kila kitu kinawezekana, na hakika hilo litajionyesha kwa vijana hawa ambao kwa mara ya kwanza tangu mashindano ya BSS yaanzishwe hawajawahi kusaidiwa kwa kiasi hiki," alisisitiza Khan.

Kwa upande wao washiriki watakaokuwa kwenye ziara hiyo wameishukuru kampuni ya Zantel kwa kuwasaidia kurekodi nyimbo zao, kuzitangaza na sasa ziara hiyo.

"Hakika Zantel wameonyesha utofauti na makampuni mengine, kwani makampuni mengi hupotea baada ya kumalizika kwa shindano au tukio husika, ila Zantel wamekuwa nasi baada ya kuisha mashindano wakihakikisha tunarekodi nyimbo zetu na kuzitangaza, tunashukuru sana kwa hilo," alisema Nsami Nkwabi, mmoja wa washiriki watakaokuwepo kwenye ziara hiyo.

Ziara hii pia itawapa fursa kubwa Zantel na washiriki kutoa shukrani kwa mashabiki wa mziki waliowaunga mkono wakati wa mashindano.

Kwa upande wake mshindi wa Epiq BSS alisema mashabiki watarajie burudani kali kutoka kwake. "Nimejipanga sana kwa ajili ya kuwaonyesha Watanzania kuwa hawakukokosea kunipigia kura niwe mshindi," alisema Walter.

1 comment:

  1. 2013 bongo star search ipoooooooooooooooooooooooooo??

    ReplyDelete