Monday, February 11, 2013

NIGERIA MABINGWA WAPYA AFRIKA 2013

Mfungaji wa goli la ushindi Sunday Mba (19) akishangilia pamoja na wenzake

Wachezaji wa Nigeria wakishangilia baada ya mechi yao ya fainali dhidi ya Burkina Faso

Patashika langoni mwa Burkinabe
 


NIGERIA imetwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika 2013 baada ya kuibwaga Burkina Faso kwa goli 1-0 katika mechi ya fainali mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Goli pekee kutoka kwa mchezaji anayecheza soka nchini Nigeria, Sunday Mba, alilofunga katika dakika ya 40 lilitosha kupeleka taji la tatu la Afrika nchini Nigeria.

Yalikuwa ni mafanikio mengine kwa kocha wa Super Eagles, Stephen Keshi ambaye wakati Nigeria ilipotwaa ubingwa huo kwa mwara ya mwisho mwaka 1994, alikuwa nahodha wa timu hiyo katika fainali zilizofanyika nchini Tunisia.

Nigeria ilitwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa Afrika mwaka 1980, wakati fainali hizo zilipoandaliwa nchini Nigeria.

Tuzo ya mchezaji bora wa michuano hiyo ilikwenda kwa Jonathan Pitroipa wa Burkina Faso, wakati Emmanuel Emenike wa Nigeria alishinda tuzo ya mfungaji bora, Moses Victor akiwa mchezaji bora wa mechi kati ya Nigeria na Burkina Faso.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alikuwa rasmi wa fainali hiyo akiwa sambamba na rais wa Fifa Sepp Blatter na rais wa CAF, Issa Hayatou, ambao wote walikuwapo kukabidhi medali za dhahabu kwa fedha kwa Burkinabe, za dhahabu kwa Nigeria na kombe kwa nahodha wa Nigeria, Joseph Yobo, ambaye aliingia akitokea benchi dakika mbili kabla ya mechi kumalizika.

Kutokana na beki wa kati veterani Yobo kupoteza namba yake katika kikosi cha kwanza, kipa Vincent Enyeama ndiye aliyekuwa akivaa kitambaa cha unahodha lakini kipa huyo alisema baada ya Super Eagles kutinga fainali wakati wakijiandaa kuikabili Burkina Faso: "Mimi si nahodha. Nahodha wa timu hii ni Yobo. Nitampisha akapokee kombe ikiwa tutalitwaa na tutalitwaa."

Wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi, Yobo alisema alijua kwamba baada ya michuano hii hataweza kucheza tena hivyo alikuwa akitaka kustaafu akiwa na tuzo hiyo ya heshima hivyo ana furaha sana kwani ametimiza ndoto yake baada ya kuitumikia Nigeria kwa miaka 12.

Keshi alisema umefika wakati sasa kwa mataifa kuwaamini makocha wazawa.

Fainali za Mataifa ya Afrika zilianza Januari 19 na zikafikia tamati yake Jumapili Februari 10.

No comments:

Post a Comment