Tuesday, February 19, 2013

NI VITA SIMBA v PRISONS, AZAM v JKT RUVU, COASTAL v OLJORO


BAADA ya sare mbili mfululizo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Simba kesho (Februari 20 mwaka huu) wanashuka Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wakiwa wageni wa Tanzania Prisons.

Katika mechi zake mbili zilizopita, Simba iliondoka pointi mbili tu kati ya sita ilizokuwa ikizipigania. Ilitoka sare na timu za JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na baadaye sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Oljoro JKT.

Hiyo itakuwa mechi ya nne kwa Mfaransa Patrick Liewig tangu aanze kuinoa Simba huku akifanikiwa kuondoka na ushindi katika mechi moja dhidi ya African Lyon inayokamata mkia kwenye ligi hiyo. Simba iliilaza Lyon mabao 3-1.

Kwa upande wa kocha Jumanne Chale anashusha kikosi chake uwanjani kesho akiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo huo Februari 9 mwaka huu.

Hekaheka nyingine itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 25,000 utakapokuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na African Lyon. Wakati Lyon ikikamata mkia, Toto Africans yenye pointi 14 inashika nafasi ya 12 katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Mwamuzi Simon Mberwa wa Pwani atakuwa shuhuda wa mechi kati ya Coastal Union ya Tanga na Oljoro JKT ya Arusha itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na uimara wa timu zote mbili.

Nayo JKT Ruvu ambayo haijafanya vizuri msimu huu kulinganisha na minne iliyopita itacheza Azam kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam. JKT Ruvu chini ya kocha Charles Kilinda inakamata nafasi ya nne kutoka chini ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 15.

Iwapo itafanikiwa kushinda mechi hiyo, Azam itaendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga. Azam ambayo ni moja ya timu zenye safu kali ya ushambuliaji katika ligi hiyo ikiwa imefunga mabao 27 ina pointi 33.

No comments:

Post a Comment